Peter Akaro
Mama mzazi wa mwanamuziki Beyonce, Tina amefunguka jinsi ndoa yake na aliyekuwa mume wake, Mathew Knowles ilivyokuwa na migogoro mingi iliyochochewa na usaliti hadi mwisho wa siku wakafikia hatua ya kutalikiana.
Katika wasifu wake mpya ujulikanao kama 'Matriarch' uliotoka mapema wiki hii Amazon, Tina ameandika mengi katika kitabu hicho akikumbushia safari yake ya ndoa ilivyoanza kwa misukosuko ila akachagua kuvumilia.
Tina anasema baada ya kufunga ndoa na Mathew mwaka 1980 aliona dalili zote za matatizo katika uhusiano wao, alifahamu wazi kuwa mwenzake hajatulia kabisa kwani ana vimada wengi huko nje lakini bado upendo kati yao ulikuwepo.
"Mwaka huo wa kwanza tayari kulikuwa na matatizo katika ndoa yetu lakini mashaka niliyokuwa nayo yangeondolewa na yeye, ukweli ni kwamba upendo wetu bado ulikuwa na nguvu zaidi kuliko kuchukua uamuzi wa kuachana," alisema Tina.
Hatimaye wanandoa hao walijaliwa mtoto wao kwanza ambaye ni Beyonce mwaka 1981, Tina anasema wakati huo akiwa kama mke na mama, bado mambo yaliendelea kuzoroto kutokana na mumewe kukosa uaminifu ndani ya ndoa yao.
Kipindi akiwa na ujauzito wa mtoto wao wa pili na wa mwisho, Solange mwishoni mwa 1985, Tina alikuwa akifikiria kuwa ni muda sahihi wa kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kupata talaka kutoka kwa Mathew ambaye usaliti wake ulishamchosha.
"Ndoa ilikuwa ikizorota kwa haraka kuliko vile ningeweza kutafuta njia ya kusuluhisha mambo au kuifanya kuendelea kuwepo licha ya kuwa na ujauzito," alisema na kuongeza.
"Nilikuwa nimezoea hali hizi mbili, kuwa na furaha mnapofanya jambo zuri katika maisha yenu, kisha kuchukizwa na kuhuzunishwa na udanganyifu wake ulivyokuwa," alisema Tina.
Licha ya misukosuko hiyo, hatimaye ndoa ilianza kuwa na wakati mzuri baada ya Tina kuanza kufanya kazi kwa ukaribu na mumewe katika kumsimamia Beyonce kimuziki chini ya kundi la R&B la Destiny's Child.
Mathew alipokuwa akilisimamia kundi hilo, Tina alikuwa mbunifu wa mabinti hao kuanzia mitindo ya nywele hadi mavazi, na polepole maisha yao yakaanza kubalika, kutoka migogoro ya ndoa hadi biashara ya muziki.
Kundi la Destiny's Child lililoundwa mwaka 1990 likiwa na wasanii kama Beyonce, Kelly Rowland na Michelle Williams, lilifanya vizuri kupitia nyimbo zao kama Bills, Bills, Bills (1999), Say My Name (1999), Survior (2001) n.k.
Hata hivyo, mwaka 2009, ndoa ya Tina ilikumbwa na aibu kubwa, baada ya yeye na ulimwengu kugundua kuwa Mathew ana mtoto nje ya ndoa ambapo alizaa na muigizaji wa zamani Alexsandra Wright.
"Nilipiga kelele, 'ondoka! ondoka!', ni kana kwamba alikuwa pepo fulani. 'Nakuchukia!' ... ulimwengu wangu wote ulikuwa umelipuka kwa hasira," alielezea Tina jinsi alivyopokea habari hiyo.
Baaada ya talaka yao kutoka rasmi mwaka 2011, Tina anasema,"Nilihisi huzuni sana, si kuhusu yeye bali kuhusu ndoa. Nilihisi kama nimeshindwa. Tulishindwa sisi, watoto wangu na mimi mwenyewe. Ilikuwa ni sisi dhidi ya ulimwengu, kuchukua kile ambacho maisha yalituletea,".
Mwaka uliopita Beyonce akiongea na jarida la Essence na kutangaza ujio wa bidhaa zake za nywele, alisema aliamua kuja na mradi huo kwa sababu mama yake Tina alianza kazi ya saluni akiwa na umri wa miaka 19 na kufanya kazi ya kutengeneza vipodozi.
Leave a Reply