Mambo muhimu yakuzingatia kwa wanafunzi wa chuo ( part 2)

Mambo muhimu yakuzingatia kwa wanafunzi wa chuo ( part 2)

Oyaaaweeeh! Wanangu sana kama kawaida yetu tunaendelea pale tulipo ishia, wiki iliopita bwana tumezungumzia kuhusiana na maswala mazima ya mambo muhimu ya kuzingatia kwa mwanafunzi wa chuo.

Kama kawaidia katika segment yetu tunajuzana yale yote ambayo baadhi yao hawayafahamu na wale wanao yafahamu basi wanaongeza uelewa kupitia hilo, sasa wiki hii tunaendelea na kumalizia yale mambo muhimu ambayo mwanafunzi wachuo anatakiwa kuyazingatia…

  • Kufanya maamuzi sahihi

Katika maisha si kila jambo linawezekana kwa wakati ule ule." Maisha yako chuoni si zaidi ya miaka mitano (yamkini kuna wengine wanaosoma zaidi ya miaka hiyo).

Hivyo tambua kuwa unapokuwa mwanafunzi wa chuo si kila jambo au wazo linalokuja katika akili yako ulipaparikie. Fanya uchambuzi yakinifu, jiridhishe, jisadikishe na upange kwa usahihi kwa kila jambo unalolifanya na pia usitende jambo kwa sababu umeambiwa na mtu fulani ulifanye.

Kumbuka kuwa mwisho wa siku kila jambo unalolifanya litakurudishia majibu chanya au hasi unaweza ukapata wazo la biashara, jiulize kama ni wazo sahihi kwa wewe kulifanya.

Tambua kuwa haya ni maisha yako unayoyajenga kwa ajili yako na kizazi chako lakini pamoja na hayo yote, usiogope kuchukua au kukamata fursa pale inapojitokeza.

  • Jifunze zaidi kuhusu kuweka akiba

Hata ukifanikiwa kuweka kiasi kidogo cha pesa, kitakusaidia katika siku ambazo una uhitaji zaidi ya leo wengi wa wanafunzi wa chuo ni wafujaji wazuri zaidi ya kuwa wawekezaji.

Simaanishi kuwa hautakiwi kuwa na matumizi mengi, kuwa na matumizi yenye tija na kiasi kidogo utakachoweza kukiweka akiba, weka katika 'Fixed Deposit' na kitaweza kukusaidia pale utakapohitaji zaidi.

Kwa maana mkopo ulio nao leo, kesho unaweza usiwepo msaada wa kiuchumi unaoufaidi leo kesho utaisha, je utafanya nini iwapo ulitumia vyote na hukujua kuwekeza. Kuwa mjasiriamali wa pesa zako, zitengenezee namna ambayo zitakuheshimu na hazitakufanya uwe na mihemko katika kuzitumia.

  • Jua kuwa cheti kizuri sio kufanikiwa katika maisha

Sikuvunji moyo unayetafuta kuwa mwanafunzi bora au kuwa na cheti cha 'first class' au 'highest GPA’, bali ni kukujulisha kuwa 'utaishi katika mafunzo ya vitendo ni jambo ambalo uchumi wa karne ya ishirini na moja inahitaji.

Jitahidi ujue soko lako linahitaji nini na sio kuwa na matokeo mazuri katika maandishi ila ubovu katika vitendo. Iwapo itatokea hivyo, ni wazi kuwa unaishusha hadhi yako, hadhi ya elimu yako na hadhi ya mahali kote ulipopitia.

Ofisi za siku hizi, ziwe za Uhasibu au Uhandisi, sio za kujizungusha kwenye kiti cha ofisi, bali ni za vitendo na kulielewa soko linalo kuzunguka.

  • Usimdharau mtu yeyote kwa muonekano wake

Hapa sasa naona kama nawaonea watu ila usiwe mpiga umbea kwa kujiaminisha kuwa wewe ni bora zaidi, au wewe ni mwenye uwezo zaidi ya wengine na usipende kuwasema wengine kwa kuwalinganisha na mafanikio uliyoyafikia au kwa kufaulu kwako katika masomo au jambo lolote.

Kwa maana ni hakika kuwa unajua ni wapi mtu atokapo, ila hujui aendako. Kama una shaka na mtu yeyote kuhusu mwenendo wa mtu, msahihishe kwa maana hayo ni maisha ya muda mfupi tu, yamkini utakutana na mtu huyu akiwa juu yako. Wazungu wanasema, "Humble yourself, never exalt yourself above anybody else. Just let others exalt you. For the world is still spinning."

  • Cha mwisho cha kuzingatia Zaidi ni kuwa bado hujachelewa.

Hata kama umebakiza muda mfupi kumaliza masomo yako, tengeneza sehemu ya kutokea. Wengi wamekosea ila walipojua ni wapi walikosea, waliinuka na kujua wapi wanaanzia.

Tafuta njia sahihi ili upate kile ambacho unakitaka kwa vyovyote vile ulivyo, usijaribu kujilinganisha na mtu mwingine halafu wewe ukajiona mjinga, unachotakiwa ujue ni kwamba umechelewa tu na bado una nafasi ya kusimama ili kufikia malengo yako. Jitahidi, simama na hata ukianguka, jua jinsi ya kusimama.

Yeieeeeeh! Tukutane next week katika mada nyingine!!!

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags