Maokoto yanavyowafanya wasanii wa vichekesho kukimbilia YouTube

Maokoto yanavyowafanya wasanii wa vichekesho kukimbilia YouTube

Siku za hivi karibuni huwenda mambo ni rahisi kwa wasanii wa vichekesho baada kuyakimbiza maudhui yako katika mitandao ya kijamii kama YouTube tofauti na ilivyokuwa zamani.

Akizungumza na Mwananchi, Mchekeshaji Ndaro amesema sababu ya maudhui yao kuyahamishia katika mitandao ya kijamii ni kutokana na wasanii wengi kutekwa na utandawazi.

“Ukiangalia karibia wasanii wote wametekwa na utandawazi hasa sisi wa vichekesho na tunafanya hivyo kwa sababu sasa hivi dunia inatutaka tufanye hivyo na mashabiki wetu wengi wamekuwa wakitumia simu janja ambao tuaamini ni rahisi wao kuona kazi zetu,” amesema Ndaro.

Aidha ameeleza kuwa kupitia mitandao inawasaidia kupata faida kwa haraka kuliko kufanya kama zamani ambapo kazi zao zilikuwa zikinunuliwa na matajiri.

“Kupitia mitandao imetusaidia siku hizi maudhui yetu hatuuzi mara moja au kwa mtu mmoja kama zamani, kuna wachekeshaji ambao walikuwa wanawauzia matajiri halafu huyo bosi ndiyo ayapeleke sokoni, hapo faida alikuwa anaipata yeye.

"Hivyo kuja kwa mitandao imerahisisha kuuza kazi zetu sisi wenyewe halafu sio mara moja kwa sababu kila mtu ana muda wake wa kuangalia kazi yangu mtandaoni kwa hiyo kila inapoangaliwa ndiyo nazidi kujikusanyia maokoto," amesema.

Hata hivyo, Ndaro ameeleza ingawa mitandao imeleta faida kwao lakini kuna kundi la watu vijijini ambao bado hawana utaalamu wa kutumia simu janja sambamba na kuwa na uwezo mdogo wa kununua mabando hali ambayo inawalazimu kuandaa shoo za mikoani ili kuwafikia kirahisi.

“Ingawa kuna muda inatulazimu kufanya shoo za mikoani ili kuwafikia mashabiki wetu ambao imekuwa changamoto kwao kutumia simu janja, huenda ikawa changamoto ya kununua mabando kila siku ili kututizama sisi na kazi zetu maana si unajua maisha ya kijini na mjini tofauti japo kuna mikoa mabayo imeendelea," amebainisha.

Kwa upande wa MC Mboneke ambaye ni mchekeshaji ambaye amewateka watu kutokana na kuigiza kwa kubana sauti, ameeleza kuwa wachekeshaji wanaweka nguvu YouTube kwa sababu ya kipato.

“Ukiona wasanii wanakimbilia sehemu moja tu kuweka maudhui yao ni kwa sababu ya kipatao na sio vinginevyo, YouTube sasa hivi imekuwa ikiwalipa wasanii wengi wa vichekesho ndiyo maana msanii hana muda wa kutoa DVD au kupekeleka kichekesho chake kwenye televisheni ambapo mambo yanakuwa mengi sana hasa ulipaji wake,” amesema MC Mboneke.

Pia ameelezea kuwa kuna changamoto kupeleka kazi YouTube akibainisha kwamba kuna muda wanashindwa kupata madili ya matangazo au ubalozi wa kutangaza bidhaa za kampuni mbalimbali ukilinganisha na kuweka kazi TikTok na Instagram.

“Kila kitu kina faida na hasara ingawa YouTube inatupatia manufaa ya kupata pesa lakini kuna muda tunashindwa kupata ‘Endorsement’ au madili ya kuwa mabalozi kwa sababu ili mtu akuone akupe dili lake haangalii YouTube unafanya nini kwa sasa bali anaangalia  TikTok na Instagram,” amesema.

Abdul Hussen Chacha maarufu Head Master, ameiambia Mwananchi Scoop kuwa wakati umebadilika na mashabiki wengi wa vichekesho wamekuwa wakikimbilia katika mtandao huo.

“Naamini zamani kulikuwa na kizazi ambacho ukitoa kanda au DVD wanaona sawa lakini sasa hivi watu hawako huko kabisa ndiyo maana 'comedian' wote wameamua kuweka 'full movie' za vichekesho kama wanavyofanya kina Clam Vevo,” amesema.

Hivi sasa wasanii wa komedi wanaofanya vizuri na kuwateka mashabiki wao katika Mtandao wa YouTube ni Mkojani, Clam Vevo, Steve Mweusi, MC Mbonike na wengine wengi.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post