Show ya Halftime ya Super Bowl imekuwa ikifanya vizuri miaka yote, ikianza kama tukio dogo la maandamano ya kutumia bendi na kisha kuwa tamasha kubwa linalowavutia mastaa wa muziki pamoja na mamilioni ya watazamaji.
Ilipoanzishwa mwaka 1967, show ya halftime ilihusisha, miongoni mwa vitu kama Bendi ya Symphonic ya Chuo Kikuu cha Arizona ikicheza "The Sound of Music" na "When the Saints Go Marching In" mambo ambayo yalikuwa yakipendelewa kutumika katika michezo ya mipira ya miguu.
Mambo yalibadilika baada ya tamasha lililofanywa na marehemu mkali wa Pop Marekani Michael Jackson mwaka 1993, ambapo show yake iliibua hisia za wengi huku akibadilisha mtazamo kwa waandaaji wa tamasha hilo na kuwafanya waandaaji waanze kuchagua mastaa wakubwa kwa ajili ya kutumbuiza katika fainali za mchezo huo.
Na hawa ndio mastaa 10 bora waliofanya vizuri katika onesho hilo la Halftime ya Super Bowl.
1. Prince (2007)
Moja ya staa ambaye ameupiga mwingi licha ya kukabiliwa na kashfa nyingi kwa mwaka huo lakini alifanya makubwa katika show yake ya Super Bowl jambo ambalo lilipelekea mashabiki na wadau kusahau kama mwamba huyo alikabiliwa na matatizo ya kisheria.
Ubunifu wake katika uimbaji na upigaji wa gitaa uliwakosha mashabiki wengi katika tamasha hilo ambapo alitumbuiza nyimbo kama Purple Rain, "Proud Mary," "All Along the Watchtower", Let’s Go , 1999, Crazy na nyinginezo. Msanii huyo alifahamika kutokana na mchanganyiko wake funk, rock, pop, R&B, na soul. Prince Rogers Nelson, alizaliwa 7 Juni 1958 na alifariki 21 Aprili 2016.
2. U2 (2002)
Ikiwa imepita miezi mitano tangu mashambulizi yalivyotokea Septemba 11, 2001, nchini Marekani hasa katika miji New York, Washington, D.C., na Pennsylvania, kundi la wasanii la U2 ambalo limewashirikisha wasanii kama Bono, The Edge, Adam Clayton na Larry Mullen Jr liliingia jukwaani 2002 katika tamasha hilo la Super Bowl huku wakikonga nyoyo za mashabiki kwa kwa kutoa heshima kwa waathirika.
Wakati walipokuwa wakitumbuiza wimbo wa "Where the Streets Have No Name," waliibua hisia za mashabiki waliokuwepo uwanjani baada ya kuonesha majina ya wahanga wa waliopoteza maisha kutokana na shambulio hilo.
3. Dr. Dre & Friends (2022)
Baada ya miaka mingi kupita hatimaye hip-hop ilipata nafasi katika onyesho la Halftime Show ambapo mwanamuziki Dr Dre aliwaalika mastaa wenzie ambao walilichakaza jukwaa hilo kwa kutoa burudani ya aina yake akiwemo Snoop Dogg, Mary J. Blige, Kendrick Lamar, Eminem, 50 Cent na Anderson .Paak.
Kutokana na mastaa hao kukiwasha zaidi onyesho hilo lilikuwa la Super Bowl Halftime Show la kwanza kabisa kushinda tuzo ya Emmy katika kipengele cha programu bora ya burudani ya moja kwa moja (Outstanding Variety Special - Live).
4. Beyoncé (2013)
Februari 3, 2013, mwanamuziki Beyonce naye alionesha umahiri wake ambapo alipanda katika jukwaa hilo alitumbuiza nyimbo kama "Love on Top," "Crazy in Love," "End of Time," na "Baby Boy. Huku tamasha likipata shangwe zaidi baada ya Destiny's Child, Kelly Rowland na Michelle Williams, kuungana naye katika kutoa burudani.
Onyesho hilo lilipokelewa vyema na watazamaji na wakosoaji, na lilivutia takribani watazamaji milioni 104 kwa usiku mmoja.
5. Bruce Springsteen & the E Street Band (2009)
Baada ya kukataa mualiko kwa miaka kadhaa hatimaye msanii huyo ilikubali kuonyesha uwezo wao ambapo walifanikiwa kutumbuiza nyimbo nne maarufu kwa mashabiki, huku tukio lililowavutia zaidi mashabiki ni pale Springsteen, aliponaswa na kamera ya televisheni akikata mauno ya uzazi wakati alipokuwa akitumbuiza wimbo wa “10th Avenue Freeze Out.”
6. Madonna (2012)
Akiwa na amsha amsha la kutosha la kukaribia kuachia albamu yake ya MDNA, Madonna aliingia kwa kishindo kwenye tamasha la Super Bowl XLVI Halftime Show kama nahodha wa kishujaa wa kikosi ambacho kilijumuisha mastaa wengine kama LMFAO, Nicki Minaj, M.I.A., na CeeLo Green.
Onyesho hilo la dakika 12 lilikuwa la kipekee kutokana na msaii huyo kuonesha mbwembwe na manjonjo ya hapa na pale jambo ambalo lilipelekea kupata shangwe kutoka kwa mashabiki.
7. Lady Gaga (2017)
Hii lilikuwa moja ya onyesho la halftime lenye mandhari ya kuvutia zaidi na la kupigiwa makofi kutokana na uwezo wake wa uimbaji katika historia ya Super Bowl na namna alivyomaliza onyesho lake ambapo lilitajwa kuwa bora zaidi katika historia ya shoo hiyo.
Gaga alitumia dakika 12 kuwapatia kile mashabiki walichokuwa wakikihitaji ambapo alifanikiwa kutumbuiza ngoma kama Poker Face, Born This Way, Bad Romance, God Bless America” na “This Land Is Your Land.
8. Michael Jackson (1993)
MJ alifanya onyesho la kipekee la Halftime katika Super Bowl XXVII Januari 31, 1993, ambalo lililofanyika katika Rose Bowl huko Pasadena, California. Onyesho hili linakumbukwa kama moja ya matukio muhimu katika historia ya Super Bowl, likileta mabadiliko makubwa katika muundo wa onyesho la Halftime.
Katika onyesho hilo, Jackson alitumbuiza nyimbo zake maarufu kama “Jam,” “Billie Jean,” “Black or White,” na “Heal the World ambapo alitumia burudani hiyo kutuma ujumbe kwa jamii kuhamasisha umoja na upendo duniani kote.
9. The Rolling Stones (2006)
Zali la mentali liliwandondokea kundi la The Rolling Stones ambapo walifanikiwa kufanya onyesho lililovutia watazamaji milioni 89.9, idadi kubwa zaidi kuliko watazamaji wa tuzo za Oscars, Grammys, na Emmy Awards kwa mwaka huo. Huku wakitumbuiza vigongo vyao vitatu ambavyo ni Start Me Up, Rough Justice, na (I Can't Get No) Satisfaction.
10. Rihanna (2023)
Baada ya miaka mitano kupitia mwaka 2023 onyesho la Rihanna ‘Riri’ lilioneshwa kwa mara ya kwanza moja kwa moja (live) na kulifanya onesho hilo kupata ufuatiliaji zaidi ambapo ilitajwa kutazamwa na zaidi ya watu milioni 121.017, ndani ya dakika 15 za Halftime Show, na kuwa onyesho la Halftime lilioangaliwa zaidi katika historia ya Super Bowl.
Akiwa amevaa mavazi mekundu, Rihanna alitumbuiza nyimbo zake maarufu kama “Where Have You Been,” “Only Girl (In the World),” “We Found Love,” “Rude Boy,” “Work,” “Wild Thoughts,” “Pour It Up,” “Umbrella,” “Diamonds,” na nyinginezo. Mbali na hilo aliwavutia wengi zaidi kwa kufichua ujauzito wake wa mtoto wa pili wakati wa onyesho hilo.
Mbali na mastaa hao ambao wameweka historia katika onyesho hilo linalofanyika kila mwaka wengineo ni pamoja na Paul McCartney (2005), Katy Perry (2015), Janet Jackson & Justin Timberlake (2004), Coldplay, Beyoncé and Bruno Mars (2016), Usher Raymond (2024) na mwaka 2025 jukwaa likitawaliwa na Kendrick Lamar.

Leave a Reply