Nyuma ya pazia majina ya mastaa wa Bongo Fleva

Nyuma ya pazia majina ya mastaa wa Bongo Fleva

Na Peter Akaro

Kwa miaka mingi tumekuwa tukisikiliza muziki wao na kutazama mitindo yao ya maisha lakini kuna mengi yametokea nyuma ya pazia hadi wasanii hao wa Bongo fleva kupata majina yao ambayo ni chapa kwao kwa sasa.

 Makala haya kwa leo katika sehemu yake ya kwanza itaangazia ni wapi hasa wasanii hao walipopata majina yao ambayo wanayatumia katika sanaa hadi kuwa chimbuko la umaarufu wao.

 Kwa asilimia kubwa wapo waliopewa majina na wasanii wenzao, wadau, familia huku wengine wakitohoa kutoka katika majina yao ya asili, hivyo kuja na kitu kipya cha kuvutia zaidi. Karibu.

 

  1. Chege

Jina alilopewa na wazazi wake ni Said Juma Hassan, hilo la Chege amelitoa katika kitabu cha The River Between (I995) alichokisoma shule na kuvutia na uhusika wa mtu aliyetumia jina hilo katika kitabu hicho kilichoandikwa na Ngugi wa Thiong’o kutokea Kenya.

Chege aliyeanza muziki katika kundi la TMK Wanaume Family mwaka 2002 na kutoka na wimbo wake, Twenzetu (2003) akiwa na Mh. Temba, Ferooz na YP, alipenda upekee wa jina la Chege na akaanza kulitumia tangu akiwa shule hadi katika muziki wake.

 

  1. Mwana FA

Rapa huyu aliyepita makundi ya Black Skin, Quite Gangsters Chronic (QGC) na East Coast Team, alipewa jina la Mwana FA na DJ Bonny Luv ambaye ndiye alirekodi wimbo uliomtoa kimuziki, Ingekuwa Vipi (2002) akimshirikisha Jay Moe chini ya Mawingu Studio.

Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, alipewa jina hilo kufuatia kurekodi wimbo uitwao ‘Mwanafalsafa’ uliochochea ujio wa albamu yake ya kwanza, Mwanafalsafani (2002), kisha ya pili, Toleo Lijalo (2003).

 

  1. Billnass

Ni rapa aliyepita Rada Entertainment, L.F.L.G (Live First Live Good), Rooftop Entertainment kisha kufungua lebo yake, Mafioso Inc, jina la Billnass amelitoa katika jina lake la William Nicholaus, yaani William (Bill) na Nicholaus (Nass) ambalo ni la Baba yake.

 

Alichofanya Billnass aliyetoka na kibao chake, Raha (2014) akiwashirikisha TID na Naziz, mwanachama wa kundi la Necessary Noize kutokea Kenya, hakina tofauti na kile walichofanya kina Bill Clinton na Bill Gates ambao wote majina yao ya mwanzo ni William.

 

  1. Professor Jay

Wakati anajiunga na kundi la Hard Blasters Crew (HBC) mwaka 1995 akiwa kidato cha tano, katika muziki alitumia jina la Nigga J, hilo la Professor Jay alipewa baadaye na John Dilinga ‘DJ JD’ ambaye alitohoa jina lake la kuzaliwa na Joseph Haule.

 

Wawili hao walifanya kazi pamoja na katika moja ya shoo za DJ JD, ndipo Professor Jay alimuona Jay Moe kwa mara ya kwanza kisha kuja kumshirikisha katika wimbo wake ‘Tathimini’ kutoka katika albamu yake ya kwanza, Machozi Jasho na Damu (2001).

 

  1. Shaa

Hadi anashinda Coca-Cola Popstar 2004, bado alikuwa anatumia jina alilopewa na wazazi wake la Sarah Kaisi katika muziki, ila Ngwea aliyefariki Mei 2013 ndiye alikuja kumpa jina la Shaa ambaye ni msanii wa kwanza wa kike kusainiwa MJ Records.

Baada ya ushindi huo aliungana na washindi wenzake, Witness na Langa na kuunda kundi la Wakilisha ambalo ni muunganiko wa majina yao. Wakilisha ndio walikuwa washindi kutokea Tanzania, huku Kenya wakiwa ni kundi la Sema na Uganda wakiwa ni Blu 3.

 

  1. Navy Kenzo

Kundi la Navy Kenzo linaloundwa na Nahreel na Aika, jina hilo limekutanisha maneno mawili kutoka nchi mbili tofauti, kwanza ni ‘Navy’ neno la Kiingereza lenye maana ya Jeshi, pili ni ‘Kenzo’ neno lenye asili ya Japan likiwa na maana ya Busara, Afya na Akili.

Navy Kenzo ambao wametoa albamu tatu, AIM (Above Inna Minute) (2016), Story Of The African Mob (2020) na Most People Want This (2023) tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013, wasanii wake walikuwa sehemu ya kundi la Pah One lilosambaratika.

 

  1. Danny Msimamo

Wazazi wake walimpa jina la Daniel Kamili, hilo la ‘Msimamo’ lilikuja alipoanza muziki, kupambana katika tasnia kisha kurudia shule na baadaye kurejea tena kwenye muziki, akaona kujiita ‘Danny Msimamo’ itafaa zaidi kutokana alisimamia kile alichoamini.

 

Ila Danny aliyetoka na wimbo, Mic (2005) uliotengenezwa Mr. Ebbo chini Motika Records, utasikia watu wengine wakimuita ‘Danny Msimamo, Kijana wa Makamo’, hiyo ilikuja tu akitafuta vina katika nyimbo zake, haina maana yoyote katika uhalisia wa maisha yake.

 

  1. OMG

OMG ni kundi linaloundwa na Young Lunya, Conboy na Salmin Swaggz, walipewa jina hilo na mwanachama wa zamani wa kundi la Rockaz, Quick Rocka aliyetoka ngoma yake, Bullet (2010) akimshirikisha Q Jay baada ya kusainiwa MJ Records.

OMG waliotamba na wimbo wao, Uongo na Umbea (2017) wakiwa na Barakah The Prince, Quick Rocka aliwaita OMG (Ooh My God) kufuatia kukubali uwezo wao kimuziki na kuwasaini wote katika lebo yake, Switch Music Group (SMG).

 

  1. Gangwe Mobb

Kundi la Gangwe Mobb linaloundwa na Inspector Haroun na Luteni Kalama tangu mwaka 1994, jina hilo walipewa na DJ Bonny Luv ambaye aliwaona katika mashindano ya rap na kuibuka washindi katika viwanja vya Don Bosco, Upanga jijini Dar es Salaam.

 

Gangwe Mobb walioanza muziki baada ya kuvutiwa na LWP Majitu, wimbo uliowatoa ni Ngangari (1999) ulitengenezwa na Rajabu Marijani, P-Funk Majani na DJ Bonny Luv aliyewapa jina hilo kutokana na ustahimilivu wao katika muziki maana walimtafuta sana.

 

  1. Shilole

Mwimbaji huyu jina lake la Shilole alipatiwa na bibi yake na maana ya jina hilo katika kabila lao la Wanyamwezi ni kioo, hiyo ni kutokana alipokuwa mdogo wakati akilia bibi yake alikuwa akimpatia kioo, na pindi alipojiangalia, basi mara moja alinyamaza.

 

Shilole aliyetoka kimuziki na wimbo wake, Nakomaa na Jiji (2013) baada ya kuonekana katika video ya wimbo wa 20 Percent, Tamaa Mbaya (2011), amekuwa akitumia jina lake katika biashara zake, mfano Shilole Entertainment, Shishi Gang na Shishi Food.

                            






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags