Ukiachana na kile alichoamua kukiamini, kukiishi na kukipigania nje ya muziki kwa lengo kupata haki anayodai kuporwa, hakuna ubishi kuwa Dudu Baya ni miongoni mwa wasanii walioipa Bongofleva heshima kubwa.
Ni Dudu Baya aliyepata umaarufu kupitia nyimbo zake kama Mwanangu Huna Nidhamu, Mpenzi (Tentemente), Nakupenda Tu, Cheka Kidogo, Nimeondoka, Mpangaji, Kunguru Hafugiki na kadhalika. Mfahamu zaidi.
Dudu Baya alianza muziki 1999 kwa kuachia wimbo wake 'Kaza Buti' ambao haukufanya vizuri sana ila huo ukawa ni mwanzo wa kuachana na kazi za ujenzi alizokuwa anafanya tangu anasoma chuo huko Morogoro kabla ya kuhamia Dar es Salaam.
Wakali wa hip hop kutoka Marekani, Tupac Shakur '2Pac' aliyefariki dunia Septemba 13, 1996 na Earl Simmons 'DMX' aliyefariki Aprili 9, 2021 ndio hasa waliomvutia Dudu Baya hadi kuingia katika muziki wa rap uliokuja kumpatia umaarufu.
Hadi sasa 2Pac anakumbukwa na mashabiki wengi duniani kupitia albamu yake ya nne, All Eyez on Me (1996), wakati DMX alifunika kupitia albamu yake ya pili, X (1999) iliyojumuisha wimbo wake maarufu, Party Up (Up in Here).
Mwaka 2000 Dudu Baya akaibukia MJ Records zamani MJ Production na hapo akakutana na Master J ambaye alimtengenezea mdundo wa wimbo wake maarufu 'Mwanangu Huna Nidhamu' lakini hakufanikiwa kurekodi kutokana na ufinyu wa nafasi.
Baadaye alikwenda na mdundo huo studio za Sound Crafters kwa Enrico Figueiro na kuurekodi, na ulipotoka ukafanya vizuri na hadi sasa ni moja ya ngoma kali za hip hop kuwahi kutokea Bongo. Hiyo ni kinyume na albamu ya kwanza ya Hard Blasters, Funga Kazi (2000) ambayo yote ilirekodiwa MJ Records, lakini midundo yake yote ilitengenezwa katika studio nyingi nchini Marekani na Profesa Ludigo ambaye ndiye alisimamia mradi wote huo.
Master J ambaye kati ya 1996 hadi 2010 studio yake ya MJ Records ilirekodi albamu zaidi ya 500, ndiye mtayarishaji wa muziki Bongo aliyerekodi kazi nyingi zaidi za Dudu Baya muda wote.
Na pale Bongo Records kwa P Funk Majani ambapo walikuwa wanarekodi hadi nyimbo 300 kwa mwaka kipindi hicho, Dudu Baya alifanikiwa kurekodi nyimbo zake mbili ambazo ni 'Mimi ni Mpangaji Wako' na 'Sikutana' akimshirikisha Stara Thomas.
Muziki ulimpatia umaarufu ila ugomvi wake na Mr Nice kuna fursa ulimkosesha, mathalani kesi aliyofunguliwa ilimzuia kutoka nje ya nchi, hivyo kushindwa kuhudhuria shoo mbili Uingereza ambazo alipaswa kwenda na Ray C, Mandojo na Domo Kaya.
Dudu Baya alianzisha Dar Skendo na mmoja wa wasanii waliowahi kufanya nao kazi ni Nyandu Tozzy wakati huo akitumia jina la Dogo Hamidu. Huyu kabla ya kujiunga na Dar Skendo alikuwepo katika kundi la Hotpot family liloongozwa na Soggy Doggy.
Mwaka 2003 akiwa anasoma huko Nairobi, Kenya, ndipo aliandika wimbo 'Mpenzi (Tentemente)' na aliporejea Bongo akaurekodi na kumshirikisha Vivian Tillya huku mtayarishaji akiwa ni Miikka Mwamba aliyefanya kazi FM Studio kati ya 1999 hadi 2004.
Cheni aliyovaa Dudu Baya katika video ya wimbo huo uliotoka 2004 chini ya Masai Studios ni ya dhahabu na aliinunua kwa Sh800,000, wakati huo zilikuwa fedha nyingi sana kwa msanii wa Bongofleva. Ukitaka kujua zilikuwa nyingi, chukua mfano huu video ya wimbo wa Ferooz, Starehe (2004) chini ya Benchmark Production yake Madam Rita iligharimu Sh1 milioni na inatajwa kuwa miongoni mwa video za mwanzo Bongo kwa msanii kuwekeza fedha nyingi.

Leave a Reply