Derek Dixon amemfungulia mashitaka muigizaji mwenzake na mtayarishaji maarufu wa filamu kutoka nchini Marekani, Tyler Perry kwa madai ya unyanyasaji wa kingono, huku akitaka kulipwa fidia ya dola milioni 260 (Sh674 bilioni za Kitanzania).
Dixon anadai kuwa Perry alimtengenezea mazingira ya kumtumia kingono, akisema kwamba mwaka 2019 baada ya kukutana naye kwenye hafla moja, alimuita na kuchukua namba yake ya simu na kumuahidi angempa nafasi ya kutokea kwenye moja ya filamu zake ambapo baadaye alipata nafasi ya kuigiza kwenye Episode mbili za filamu ya Perry iitwayo 'The Oval and Ruthless'.
Pia Dixon anadai kuwa Januari 2020, Perry alimualika nyumbani kwake, baada ya kulewa sana alilazwa chumba cha wageni ambapo akiwa usingizini muigizaji huyo aliingia chumbani na kuanza kumshika mapajani, kisha akaanza kupokea jumbe za kingono kutoka kwa Perry.
Malalamiko hayo kutoka kwa Dixon yanaendelea kwa kusema kuwa Perry alimuahidi kumpatia maendeleo ya kazi yake pamoja na fursa za ubunifu, ikiwemo kumsaidia kutengeneza filamu zake mwenyewe na kumpa nafasi zaidi kwenye filamu nyingine, lakini badala yake alimnyanyasa kingono, kumpiga na kumshambulia, baadaye kumlipa pesa baada ya Dixon kukataa kutii matakwa yake ya kingono.
Kwa mujibu wa malalamiko hayo, hali hiyo ilipelekea Dixon kukosa fursa nyingine za kazi na kumharibia sifa yake kwenye tasnia ya burudani, jambo lililomlazimu kuchukua hatua za kisheria na kudai haki yake.
Hata hivyo, upande wa Tyler Perry umekanusha vikali tuhuma hizo kupitia wakili wake, Matthew Boyd, ambaye ametoa taarifa akisema kuwa Derek Dixon ni mtu aliyeingia kwenye maisha ya Perry kwa nia ya kupanga utapeli.
"Huyu ni mtu ambaye alijipenyeza karibu na Tyler Perry kwa jambo ambalo sasa linaonekana kuwa si kitu kingine ila mpango wa utapeli," amesema Boyd.
Mwanasheria huyo ameongeza kuwa Perry hawezi kuyumbishwa na mipango hiyo ya kumuangusha na haitofanikiwa.
"Perry hawezi kuyumbishwa na mipango ya kumuangusha itagonga mwamba," amesema Boyd.

Leave a Reply