Wasichana tuendelee Kupiga Vita Rushwa ya Ngono

Wasichana tuendelee Kupiga Vita Rushwa ya Ngono

Wakati wanawake Machi 8 ya kila mwaka dunia uadhimisha siku yao, bado wadau wamesema rushwa ya ngono ni tatizo linalotafuna ndani kwa ndani.

Baadhi ya wadau hao ni Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN).

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Machi 8, 2022 na TAMWA, ilisema kinaangalia usalama wa wanahabari wanawake katika vyumba vya habari nchini kutokana na kuwapo kwa mwendelezo wa matukio, ushahidi na ripoti za kitafiti zinazoonyesha kuwa wanahabari wanawake bado wanapitia unyanyasaji wa kingono katika vyumba hivyo.

Ilisema maadhimisho ya Siku ya Wanawake kwa mwaka huu, yamebebwa na kaulimbiu isemayo; “Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu” ambapo imesema kauli hiyo ni kutaka kuweka usawa katika vyumba vya habari baada ya kubaini kuna mdudu anayetafuna tasnia ya habari kimya kimya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utafiti uliofanywa na Asasi ya Wanawake katika Habari Afrika (WIN) ulibaini kuwa, asilimia 41 ya wanawake wanahabari waliwahi kufanyiwa unyanyasaji wa kingono wakiwa katika maeneo ya kazi.

Chama hicho kimesema wakati Siku ya Wanawake Duniani ikiadhimishwa, TAMWA inahimiza wamiliki wa vyombo vya habari, watunga sera, serikali na wanahabari wote kwa ujumla kutupia jicho unyanyasaji na ukatili wa kingono unaofanywa ndani ya vyumba vya habari.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben alieleza kuwa unyanyasaji wa kingono kwa wanahabari iwe ndani au nje ya vyumba vya habari, una madhara makubwa katika chombo cha habari, taaluma ya habari, aina ya habari zitakazoandikwa na hata katika maendeleo ya nchi yenyewe.

Alisema, udhalilishaji wa kingono kwa wanahabari wanawake, unachagiza wanahabari wengi wa kike kuikimbia tasnia na hilo limesababisha kupoteza vipaji lukuki ambavyo vingekuzwa kama kusingekuwa na bughudha hiyo.

Alisema katika utafiti uliofanywa na TAMWA kwa kushirikiana na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) mwaka 2021, kuhusu hali ya rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari, ilibainika kuwa wanahabari wanawake wamewahi kukutana na udhalilishaji huu, kimwili, kimaneno na hata baadhi walifukuzwa kazi.

Kwa upande wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), ilitoa wito kwa serikali, sekta binafsi na taasisi mbalimbali kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi za uongozi kwenye taasisi hizo sawa na wanaume.

Lakini pia rushwa ya ngono si tu katika vyumba vya habari kwani  katika utafiti uliofanywa hivi karibuni na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika kipindi cha Januari na Februari mwaka huu ulibaini mmomonyoko wa maadili chanzo cha rushwa ya ngono vyuoni.

Utafiti huo pia ulibaini matumizi mabaya ya madaraka pia ni moja ya vyanzo vya kuwapo kwa rushwa kubwa ya ngono katika vyuo vikuu viwili nchini- Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Akielezea kwa kina matokeo ya utafiti huo, mwendesha mashitaka wa Takukuru, Denis Lakayo alisema kuwa utafiti huo ulihusisha wahojiwa 589, ambapo 352 walitoka UDSM na 237 kutoka Udom.

Alisema utafiti huo ulibaini zaidi ya asilimia 50 ya wahojiwa walieleza kuwapo kwa rushwa ya ngono katika vyuo vikuu hivyo.

“Katika waliohojiwa ambao walionyesha uelewa wa rushwa ya ngono kwa kuitofautisha na nyingine, walisema madaraka yalitumiwa vibaya na wahusika kama nyenzo ya kusukuma wapate wanachokitaka”alisema Lekayo na kuongeza.

“Huku mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi pia ukitajwa kuwa sababu ya kuendelea kuwapo kwa vitendo hivyo”alisema.

Alitolea mfano kilichotolewa ushuhuda na mhadhiri mmoja ambaye alimwita mzazi wa mwanafunzi kujadiliana naye kuhusu mavazi na mwenendo wa kijana wake.

“Alipokuja mzazi ilibidi mhadhiri amsalimie tu badala ya kumweleza alichomuitia kutokana na namna alivyovaa, yeye alikuwa zaidi ya kijana wake” alisema.

Lekayo alisema baadhi ya maeneo walibaini yameoza kabisa, kwani yule aliyepaswa kumsaidia mwanafunzi anayedaiwa rushwa ya ngono, naye hakuwa na msaada.

Yote hayo yaliopo katika utafiti na yaliyoelezwa na TAMWA pamoja na MISA TAN, yanajithirisha wazi kuendelea kukithiri kwa rushwa ya ngono hapa nchini.

Pamoja na hayo yote nami naunga mkono kuwa ufinyu wa kutoa taarifa kutoka kwa wahusika moja ya chanzo kinachosababisha  kuendelea kuwepo kwa rushwa ya ngono na hii inatoka na jamii kukosa utayari.

Jamii hasa wahusika wanaofanyiwa vitendo hivi wakiwa tayari kwa kutoa taarifa mahali husika ni wazi kuwa tunaweza kupiga hatua katika mapambano haya ya rushwa ya ngono.

Ni ukweli uliowazi kuwa jamii inajukumu kubwa la kutoa taarifa na kuhabarishana kwa sababu rushwa ya ngono inamadhara makubwa ikiwemo maambukizi ya maradhi ya uogonjwa wa Ukimwi.

Suala hili la kufanya tafiti ni nzuri na mimi nasisitiza tuendelee kwani mapambano haya yanahitaji tafiti ili kujua ni wapi tunaweza kuanzia katika kupambana hayo.

Maadili kwa sasa yamebadilika na tekonolojia inakua kwa kasi hivyo ni vyema tukaendelea kupiga vita rushwa ya ngono na unyanyasaji mwingine wa kijinsia kwa kuwaomba wadau wote kuunganisha nguvu kwa pamoja.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags