Yaliyojiri kwenye sherehe ya Hamisa, Aziz Ki

Yaliyojiri kwenye sherehe ya Hamisa, Aziz Ki

Historia imeandikwa. Ni katika sherehe ya harusi ya msanii na mfanyabiashara Hamisa Mobetto na mumewe kiungo wa Yanga Stephane Aziz Ki. Ambao jana Februari 19,2025 walifanya sherehe ya funga dimba ya ndoa yao waliyofunga Februari 16,2025.

Wawili hao ambao awali walianza mahusiano kama sinema za kwenye runinga, sasa ni mume na mke. Katika sherehe yao wamefanikiwa kuwakutanisha mastaa mbalimbali nchini kutoka sekta mbalimbali ikiwemo burudani na michezo.

Kuanzia saa 2 usiku wageni waalikwa walianza kuonekana katika ukumbi wa The Superdome. Huku kila mmoja akiwa kwenye vazi la kuvutia. Na hapa ndipo unadhihirika msemo wa usichague mke/mume siku ya sherehe kwani kila mmoja anakuwa amependeza.

Kati ya walijitokeza katika mwonekano bomba ni Ally Kamwe, Jackline Wolper, Marioo, Nandy, Yammi, Giggy Money,Haji Manara, Christian Bella bila kumsahau Wema Sepetu ambaye wengi walimuona kama sapraizi kwenye sherehe hiyo.

Utakumbuka Wema na Hamisa wamewahi kudaiwa kuwa kwenye mgogoro uliosababishwa na wivu wa mapenzi. Kwani wote wamewahi kuwa kwenye mahusiano na nyota wa muziki Diamond Platnumz. Hata hivyo mwaka 2022 Hamisa alikanusha madai hayo na kuweka wazi kuwa hana kinyongo chochote na Wema Sepetu.

Akizungumza katika sherehe yake Hamisa alisema awali hakuwa na uhakika kama anataka kuolewa lakini mawazo yake yalibadilika baada ya kukutana na mchezaji huyo.

"Wewe ni kila kitu nilichokiomba. Wewe ni zaidi ya hivyo. Unajua, kabla ya sasa, sikuwa na uhakika sana, kama nilitaka kuolewa. Lakini tangu nilipokutana na wewe, nilijua kama huyu ndiye mume wangu. Huyu ndiye baba wa watoto wangu. Huyu ndiye kila kitu kwangu.

"Asante sana kwa kunichagua. Na nataka kusema asante kwa kuona uwezo wangu mara ya kwanza. Kama hukuhitaji nafasi ya pili. Hukuhitaji nafasi ya tatu. Kuanzia mwanzo, ulikuwa unajua mimi ndiye niliyefaa, nakupenda sana Mungu akubariki. Mungu akulinde aondoe vikwazo vyote kwenye njia yako. Ufanikiwe katika maisha. Shetani asikufikie. Ufanikishe malengo yako yote,"alisema Hamisa

Pamoja na hayo Hamisa alimuahidi mumewe kuwa naye katika shida na raha wakati wote. Hata hivyo kwa furaha aliyokuwa nayo Aziz Ki alionekana akimwaga machozi ukumbini mbele ya wageni waalikwa.

Aidha katika sherehe hiyo mwanamuziki Nandy alisema ndoa ni kitu kizuri hivyo Hamisa anatakiwa kufurahia

"Kila kitu kina wakati wake. Ndoa siyo kitu cha kuvutiwa na mtu, ni maamuzi yanatakiwa yafanyike kwa usahihi sana," alisema Nandy

Nandy ambaye alifika pekeyake kwenye sherehe hiyo, na kudai mumewe Billnass anarekodi video ya wimbo wake mpya. Alifunga ndoa miaka miwili iliyopita. Hadi sasa wamebarikiwa kupata mtoto mmoja.

Naye Wema Sepetu Wema Sepetu amemtaka Hamisa aishi maisha yenye furaha kwenye ndoa yake, na kama hatopata furaha amemshauri aondoke.

"Kitu naweza kumshauri aishi maisha yake. Siwezi kumshauri sana kwa sababu hiyo ni kazi ya masomo lakini kama dada natamani kumuona anafuraha na kama ataona haipati furaha aondoke,"alisema Wema

Pia licha ya watu wengi kuwazawadia maharusi hao lakini klabu ya Yanga, iliwapatia wawili hao Sh 50 milioni.

“Nataka kuliweka hili sawa. Hii sio ahadi kiasi cha Sh 50 milioni kimeshaingizwa kwenye akaunti ya Aziz Ki, na Hamisa kitu cha kuzingatia ni kujua paswedi maana pesa tumeshaitoa,” amesema Ally Kamwe






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags