Aliyojiri Kesi Ya Diddy

Aliyojiri Kesi Ya Diddy

Kati ya kesi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ni ya rapa kutoka Marekani Sean “Diddy” Combs ambapo mapema jana Mei 5,2025 kesi hiyo ilisikilizwa huku Diddy akikana mashitaka yote yanayomkabili.

Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali Marekani, zimeripoti kuwa wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo Combs alikana mashitaka yote aliyofunguliwa na shirikisho, yakiwemo ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya biashara za ngono.

Mbali na hilo Combs alikiri shitaka moja tu la kufanya vurugu lililotokea mwaka 2016, ambapo mwishoni mwa mwaka jana ilisambaa video ikimuonyesha akimshambulia aliyekuwa mpenzi wake Cassie katika korido ya hoteli huko Los Angeles.

Jaji mkuu anayesimamia kesi ya Diddy, Arun Subramanian aliwahoji majaji wapatao 36 ambao watasaidia kuchunguza kesi hiyo. Aidha jaji huyo aliwapa majaji watarajiwa maelezo mafupi kuhusu mashtaka ya usafirishaji wa ngono dhidi ya Combs, akiwafahamisha kuwa amekana mashtaka hayo na kwamba anachukuliwa kuwa hana hatia hadi pale itakapothibitishwa.

Hata hivyo, mchakato huo haukuenda sawa kutokana na majaji hao wapya kupungua hadi kufikia nusu huku sababu ikitajwa ni sababu za kibinafsi, kama vile kutoweza kumudu kiuchumi kushiriki kesi inayotarajiwa kudumu kwa miezi miwili pamoja na kutokuwa na uzoefu.

Aidha mchakato huo unaendelea ambapo majaji wengine wapatao 36, wanatarajiwa kuhojiwa siku ya Jumanne, huku jopo kamili la majaji likitarajiwa kukamilika kabla ya Jumatano.

Siku nzima ya jana Jumatatu, Combs, mwenye umri wa miaka 55, alikaa pamoja na mawakili wake akiwa amevaa sweta jeusi pamoja na suruali ya kijivu mavazi ambayo yaliruhusiwa na jaji badala ya nguo za jela.

Tangu kukamatwa kwake Septemba mwaka jana, amekuwa akishikiliwa katika gereza la shirikisho lililo na mazingira magumu huko Brooklyn. Huku baadhi ya wambea wakidia kuwa msanii huyo ni kama amezeeka kwani nywele na ndevu zake zimekuwa nyeupe kabisa.



Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, Diddy alionekana mwenye hofu huku akiomba kwenda msalani kujisaidia “Jaji nina wasiwasi kidogo nahitaji kwenda msalani,”alisikika akisema Combs.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags