Tukio hilo limefanyika usiku wa kuamlia leo Mei 6,2025 likiwa limesheheni matukio mbalimbali, ikiwemo vituko na mengineyo. Fuatilia zaidi
Rangi nyeusi kutawala
Katika tukio la Met Gala 2025, rangi nyeusi ilitawala, ikiwa na maana ya kipekee na kusisimua. Dhamira ya mwaka huu ilikuwa “Superfine: Tailoring Black Style”, ambayo ililenga kusherehekea ustaarabu na mchango wa watu weusi katika mitindo ya mavazi hasa dhana ya Black Dandyism.

Rangi nyeusi haikuwa tu chaguo la mitindo ya usiku huo, bali ilibeba ujumbe mzito wa kihistoria na kitamaduni. Iliwakilisha nguvu, hadhi, na heshima kwa urithi wa watu weusi. Huku ikionesha jinsi mavazi yanavyoweza kuwa chombo cha kujieleza na kuenzi utambulisho wa mtu.
Aidha, rangi hiyo ilionekana kuwa chaguo kuu kwa wageni wengi waliovutia macho ya watu duniani kote, akiwemo: Kim Kardashian, Kylie Jenner, Hailey Bieber, Nicki Minaj, Usher, Cynthia Erivo, Kendall Jenner, Rihanna, Doja Cat, Shah Rukh Khan na wengineo.

Kwa ujumla, Met Gala 2025, ilidhihirisha jinsi rangi nyeusi ilivyoweza kuunganisha mitindo ya kisasa na historia ya mitindo ya watu weusi kwa ubunifu mkubwa.
Shah Rukh Khan ndani ya Met Gala
Shah Rukh Khan ameweka historia kuwa mwigizaji wa kwanza wa kiume kutoka India kuhudhuria Met Gala. Khan alijitokeza akiwa na vazi maalumu lililobuniwa na mbunifu maarufu wa India, Sabyasachi Mukherjee, huku akitupia vito vya kifahari ikiwemo mkufu wenye herufi 'K' iliyopambwa kwa almasi, ishara ya jina lake la utani "King Khan".
Alivaa mkufu mwingine wenye herufi 'SRK', Akiwa ameshika fimbo ya dhahabu, pamoja na saa, pete za almasi.
Katika mahojiano na Time, Shah Rukh Khan alieleza furaha yake ya kushiriki katika Met Gala na kupongeza dhamira yake ya mwaka huu ambayo imelenga kusherehekea mitindo ya mavazi ya watu weusi na mchango wao katika sanaa na utamaduni.
Vituko Met Gala 2025
Moja ya kituko ambacho kimewavutia watu wengi ni kufuatia rapa kutoka Marekani André 3000, kuwasili na piano kubwa mgongoni. Akionesha ubunifu wa hali ya juu huku akiachia EP yake mpya wakati wa tukio hilo.
Wasanii wa Afrika Met Gala 2025
Ikiwa Met Gala ya mwaka huu inalenga kuwapa heshima watu weusi. Wasanii kutoka Afrika nao hawakukaa kinyonge walijitokeza na mitupio mbalimbali.

Mastaa hao ni pamoja na Tyla (Afrika Kusini), Tems (Nigeria), Ayra Starr (Nigeria), Cynthia Erivo (Nigeria/Uingereza), Lupita Nyong’o (Kenya) pamoja na Burna Boy (Nigeria).
Vazi la msanii Diljit Dosanjh kukubalika zaidi
Diljit Dosanjh mwanamuziki na mwigizaji kutoka Punjab, naye alihudhuria kwa mara ya kwanza katika Met Gala 2025, huku vazi lake likitajwa kuwa vazi bora kuwahi kutokea katika maonyesho hayo.
Katika mitandao ya kijamii mashabiki na wadau mbalimbali walilisifia vazi la Diljit lililotawaliwa na rangi nyeupe huku wengi wao wakilitaja kuwa vazi bora kuwahi kutokea kwenye Met Gala.
Ingawa hakuweka wazi jina la mbunifu wa vazi lake, ripoti zinaonyesha kuwa alivalia vazi la kipekee lililobuniwa na Prabal Gurung, mbunifu maarufu ambaye pia alibuni vazi la Alia Bhatt kwa ajili ya Met Gala ya mwaka 2024.
Ushiriki wa Diljit katika Met Gala 2025 unaashiria hatua kubwa katika safari yake ya kimataifa, baada ya mafanikio yake katika matukio kama Coachella na Paris Fashion Week. Kwa mashabiki wake, hili ni tukio la fahari linaloonyesha jinsi wasanii wa India wanavyoendelea kung'ara katika majukwaa ya kimataifa.
Rihanna kufichia ujauzito wake
Mbali na tukio hilo kuwa la kipekee huku rangi nyeusi ikiwa kama heshima kwa watu weusi, pia tukio jingine ambalo limeishangaza dunia nzima ni kufuatia na mwanamuziki Rihanna kutangaza ujauzito wake.
Akivali mavazi yenye mchanganyiko wa nyeusi na nyeupe msanii huyo alifichua ujauzito akionesha tumbo lake huku mpenzi wake Asap Rocky akithibitisha kuwa wanandoa hao wanatarajia kupata mtoto wa tatu ambapo kwa sasa wawili hao wana watoto wawili ambao ni RZA Athelston Mayers na Riot Rose Mayers.
Leave a Reply