Basata yafuta kibali cha shindano la Miss Tanzania

Basata yafuta kibali cha shindano la Miss Tanzania

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limefuta kibali cha Kampuni ya The Look kuendesha shindano la Miss Tanzania.

Taarifa ya kufutwa kwa kibali hicho imetolewa Juni 25,2025 na Baraza hilo huku likieleza kuwa uamuzi huo umetolewa baada ya kampuni hiyo kushindwa kutekeleza maagizo halali ya Baraza licha ya kupewa maelekezo kwa nyakati tofauti kupitia barua yenye kumbukumbu namba AE/90/90/03/16 ya Aprili 15, 2025, na AE.90/90/03/19 ya Mei 09, 2025.

"Kushindwa kuhuisha kibali cha kufanya kazi za sanaa kwa zaidi ya miezi sita bila sababu ya msingi, kinyume na Kanuni ya 39(g) ya Kanuni za BASATA za mwaka 2018. Kukaidi agizo la Baraza kwa kutowasilisha nyaraka muhimu kama nakala ya cheti/leseni ya kushiriki shindano la Dunia, kinyume na Kanuni za 39(f), 37(2)(a) na 36(2)," taarifa ya Baraza imeeleza sababu kuu zilizopelekea hatua hiyo.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza: "Kushindwa kuandaa shindano la Miss Tanzania kwa mwaka 2023/2024 na kutokuwasilisha mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya dunia kwa mwaka 2024/2025, bila kutoa sababu za msingi, jambo linalokiuka Kanuni ya 39(i). Kwa mujibu wa Kanuni ya 40(2) ya Kanuni za BASATA za mwaka 2018, kampuni hiyo imeondolewa sifa ya kuendelea na shughuli hiyo.

"Kampuni ya The Look Company Limited inayo haki ya kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ndani ya siku 21 tangu kupokea taarifa hii.

"BASATA linaendelea kusimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu katika tasnia ya sanaa ili kulinda heshima na ufanisi wa mashindano ya kitaifa kama Miss Tanzania."






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags