Alichokifuata Mac Voice kwenye shoo za Chaka to Chaka

Alichokifuata Mac Voice kwenye shoo za Chaka to Chaka

Ni wazi kuwa mkombozi wa wasanii wengi ambao hawapati usikivu kwa kiasi kikubwa, kwa sasa ni shoo za 'chaka to chaka' yaani zile zinazofanyikia vijijini.

Licha ya kuwa zilikuwa zikifanyika tangu awali lakini utambulisho wake kwa ukubwa ulianza baada ya mwanamuziki Rich Mavoko kuzifanya mwaka 2024.

Yes, ni Rich Mavoko yule aliyejiunga na lebo ya WCB mwaka 2016, akiwa msanii wa nne kuingia kwenye lebo hiyo na ilipofika 2021 akatemana nayo kisha kwenda kufungua ya kwake iliyoitwa Billionea Kid.

Hata hivyo baada ya msanii huyo kuonekana akifanya shoo ya aina hiyo yaliibuka maneno mengi kwenye mitandao ya kijamii. Yakihusisha kujishusha hadhi kutokana na aina ya shoo anayofanya kutoendana na ukubwa wa jina lake.

Licha ya maneno hayo Mavoko aliwahi kusema 'chaka to chaka' ni shoo iliyomlipa pesa zaidi kuliko zote alizowahi kufanya.

"Ilikuwa poa kwangu, shoo zilikuwa na pesa katika maisha yangu sijawahi kupiga shoo Jumatatu hadi Jumapili mfululizo. Hadi najiuliza, mimi mwenyewe nilipagawa kila asubuhi nagongewa napewa kitita(pesa). Haikuwa mbaya mambo mabaya ni mtandaoni,"alisema

Hata hivyo guu la saka nyoka vijijini halikuishia kwa Mavoko, zikasambaa tena video zikimuonesha msanii Mo Music akizunguka na gari vijijini kutangaza kuwa atakuwa na shoo.

Mo Music ni yule aliyewahi kutamba na ngoma kama Basi Nenda, Nitazoea, Bajaji na nyinginezo. Komenti za wananzengo ni bora ya zile zilizotumwa kwa Mavoko kwani yeye walidai kapoteza mvuto kwani hata huko kijijini anapotangaza shoo wadau wanaonekana kutomfahamu yeye ni nani.

Licha ya maneno hayo Mo aliwahi kusema ufanyaji wa shoo hizo siyo kuishiwa bali kwenda kutambua mipaka ya kazi zao zilipofikia.

"'Chaka to chaka' ni jina tu ni sehemu ambazo sisi tunatakiwa twende tukaangalie sehemu ambazo muziki wetu umefika. Unatakiwa ukatizame ndani muziki umefika kwa namna gani, wasanii wengi wanafanya ni vile tu hawaposti iheshimiwe ni sehemu ya chumba cha kupiga hela kama wote tukipiga shoo Dar unafikiri nani atapata na nani atakosa,"alisema

Licha ya wakali hao kufanya hivyo Machi 25, 2025 iliibuka sintofahamu baada ya video ya mwanamuziki Mac Voice anayetambulika kama msanii anayesimamiwa na Rayvanny kuonekana akipiga shoo za 'chaka to chaka'.

Utakumbuka mwaka 2021 Rayvanny alizindua lebo yake inayoitwa Next Level Music na ndipo alimtambulisha MacVoice. Kutokana na video hizo maswahi mengi yameibuka kwa mashabiki wakidai je Rayvanny ameshindwa kumsimamia msanii huyo?

Hata hivyo akizungumza Mwananchi mtayarishaji wa muziki nchini Joachim Marunda 'Master Jay' amesema watu wanadharau shoo hizo lakini zinatajwa kuwa na faida.

"Watu wanadharau sana hizo shoo za 'chaka to chaka' lakini ni shoo ambazo zinawapatia watu fedha nyingi wasanii wakubwa wamezoea shoo moja wanapiga hela nyingi.

"Lakini 'chaka to chaka' unapiga shoo nyingi na hela nyingi sema tu wasanii wengi wakubwa hawazipendi kwa sababu hazina content za social media, mazingira yake siyo mazuri, hawapandishwi ndege, hawana stage kwa hiyo wasanii wakubwa shoo kama hizi haziwavutii,"amesema Master J

Hivyo basi unaweza kusema alichokifuata Mac Voice kwenye shoo za chaka to chaka ni pesa, hasa ikizingatiwa hajaachia kazi kwa muda mrefu sasa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags