Mwanamuziki nguli kutoka Benin na bara la Afrika kwa ujumla, Angelique Kidjo, ameandika historia kwa kuteuliwa kuwa miongoni mwa wasanii watakaopata nyota katika Hollywood Walk of Fame kwa mwaka 2026.
Tuzo hiyo kubwa inakuja kama heshima kwa mchango wake mkubwa katika muziki wa kimataifa, utetezi wa haki za binadamu, na kuendeleza utamaduni wa Afrika kupitia kazi zake za sanaa kwa zaidi ya miongo mitatu.
Kidjo, ambaye ni mshindi wa tuzo tano za Grammy, anakuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika ya Magharibi kupewa heshima hiyo kwa upande wa muziki.
Akitangaza orodha ya walioteuliwa, kutunukiwa tuzo hizo Julai 2,2025 Hollywood Chamber of Commerce ilisema, “Kidjo ni sauti ya dunia, mwanamke mwenye uthubutu, anayewakilisha Afrika kwa fahari kupitia ubunifu wake, anastahili heshima hii,”
Wasanii wengine ambao watatunukiwa nyota hiyo ya heshima ni pamoja na Emily Blunt, Timothée Chalamet, Chris Columbus, Marion Cotillard, Keith David, Josh Groban, Grupo Intocable na wengineo.
Kwa zaidi ya miaka 30, Angelique Kidjo amekuwa na mchango mkubwa katika muziki wa dunia, akitoa radha mbalimbali katika muziki wa Afrobeat, jazz, funk na miziki ya asili ya Afrika huku akitumia lugha kama Kiyoruba, Kifaransa na Kiingereza.
Mbali na muziki, Kidjo ni balozi wa UNICEF na mwanzilishi wa ‘Batonga Foundation’, taasisi inayowezesha wasichana wa vijijini barani Afrika kupata elimu na uongozi.
Kidjo anatambulika kupitia ngoma zake mbalimbali ikiwemo Agolo (1994), We We, Wombo Lombo, Batonga (1991), Afirika na nyinginezo nyingi.

Leave a Reply