Nyota wa muziki nchini Diamond ameeleza namna anavyotumia muziki wake kupenya kimataifa huku akifunguka kuachia albamu mpya itakayotoka Septemba, iliyosheheni kolabo mbalimbali za kimataifa.
Akizungumza na Billboard kuhusu safari yake ya muziki, Simba ameweka wazi njia anazotumia kutaka kuteka soko la kimataifa huku mojawapo akiitaja ni kutengeneza nyimbo za kufurahisha.
“Nilikuwa nafanya nyimbo nyingi za kutendwa, nilijulikana kwa kuandika nyimbo za huzuni lakini nyingi zilikuwa kwa lugha yangu, Kiswahili. Na watu walinipenda kwa jinsi nilivyoandika. Ilikuwa inawagusa hadi wengine wanalia, kama vile nawapunguzia maumivu yao.
Lakini baadaye nikagundua kuwa nyimbo hizo zilikuwa zinanizuia, kwa sababu, kwanza kabisa, ili mtu aelewe ninachokiimba, lazima aelewe lugha yangu. Nikasema, kama nataka kuteka soko la kimataifa, lazima nitafute njia ya kuwafikia watu wote duniani,”amesema.
Ameongezea kuwa “Watu wanataka kuwa na furaha, wanataka kufurahi. Kwa hiyo nikaanza kuja na mawazo ya kutengeneza nyimbo za furaha, sherehe, dansi nyingi, pamoja na kutengeneza challenge kwa ajili ya mitandao ya kijamii hasa TikTok,” amesema Diamond.
Akizungumza kuhusu kutamani kutoa nyimbo za hisia, amesema anatamani kufanya hivyo lakini kwa sasa mashabiki wengi wanamuangalia katika upande mwingine wa kutoa nyimbo za kufurahisha.
“Namiss sana kutoa nyimbo hizo maana ndipo nilipotoka. Nina nyimbo nyingi sana za maumivu ya moyo ambazo nahangaika kutafuta namna ya kuziachia, lakini sipati nafasi. Kwa sababu nahisi, nitakuwaje naangalia tu watu wachache walioko nyumbani kwangu, ilihali dunia nzima inaningojea niwape kitu fulani?
"Najaribu kuleta uwiano, ni kazi ngumu sana. Sitaki kudanganya, haijalishi ni mara ngapi natoa nyimbo hizi za furaha, zile nyimbo za hisia ndiyo nyimbo ninazozipenda sana. Nikiwa chumbani kwangu, nasikiliza hizo nyimbo. Kwa hiyo wakati mwingine unaweza kuwa na wimbo unaoupenda mno, lakini inasikitisha kwamba huoni kabisa ni lini utapata nafasi ya kuuachia,”ameeleza Diamond
Hata hivyo, ameeleza uzoefu wake na utofauti wa kufanya kazi na wasanii kutoka Afrika na Marekani kama Ne-Yo na Alicia Keys.
“Utofauti upo mkubwa sana, kwa sababu nina mistari kwa ajili ya jamii yangu, nina mistari kwa ajili ya bara la Afrika, na nina mistari kwa ajili ya dunia nzima. Kwa hiyo kila msanii ninayefanya naye kazi, lazima niwe makini, kwa sababu haiwezi kuwa sawa kwa wote.
Ukifanya kitu kwa ajili ya watu wa Kiswahili ni rahisi sana, lakini kama unataka kuwa nyota wa kimataifa, basi lazima uwe makini sana na kila unachofanya. Nikifanya wimbo wa kimataifa, lazima unufaike pande zote wote wapende na dunia nzima pia ipende,”amesema Diamond.
Aidha ameendelea kwa kueleza kuwa anapoamua kufanya wimbo kwa ajili ya kimataifa huwa anatumia Kiingereza, Kiswahili na melodi yoyote ya kimataifa, huku akitumia Kiswahili cha kimkakati ambacho hata shabiki asipoelewa basi ataupenda wimbo husika akitolea mfano wimbo wa ‘Komasava’.
Akizungumza kuhusiana na ushindani katika muziki wa Afrobeat Diamond ameeleza …
“Kitu cha kwanza ni kuwa na utambulisho wako. Mimi huwa siruhusu mtu aniingilie kwenye aina yangu ya muziki au mtazamo wangu. Naamini kila msanii ana kitu chake cha kipekee, kwa hiyo mimi hujitahidi kuwa mimi, kujua watu wangu wanapenda nini na kulingana na hilo, najua ni kitu gani ninaweza kutoa duniani ambacho hakijafanana na mtu mwingine yeyote.
Hilo ndilo linalonisaidia kusimama tofauti na wengine.Jambo la kipekee kwangu ni kwamba nafanya muziki kwa Kiswahili hiyo ndiyo utofauti wangu. Najua kuna wasanii wengi tofauti, lakini mimi na mitindo yangu, Mimi ndiye msanii pekee wa Kiafrika ambaye naweza kufanya aina zote za muziki kutoka duniani kote. Ukiangalia Amapiano, nimefanya kali sana. Nina nyimbo kali sana za Kikongo. Ninajitahidi kuhakikisha natumia kila upande wa sauti yetu ya Kiafrika, ili iendelee kuwafanya watu wetu wajivunie,”amesema Diamond.
Mbali na hayo ameeleza namna anavyochagua kolabo zakufanya huku akiweka wazi kuwa kama wimbo hauamini hawezi kuutumia kwa msanii wa kimataifa.
“Kama siamini wimbo, siutumi kwa msanii kama najua naweza kumtumia Chris Brown wimbo na akaweza kuufanya, kwa nini nitume wimbo wa hovyo? Lazima nipate wimbo sahihi, wa kimataifa kabisa, ili tukiufanya, tufikie malengo.
"Halafu inakuwa rahisi zaidi mara ya pili kwa Chris Brown kukuamini tena kufanya wimbo mwingine. Msanii mmoja anaweza kuona maono ya wimbo lakini mwingine asione, kwa hiyo kama wasanii tunaheshimiana, si ndiyo? Kwa hiyo ukimtumia mtu wimbo halafu usifanye vizuri, anaweza asitake kushirikiana tena na wewe,”amesema.

Leave a Reply