Aidha hilo linajionesha katika juhudi zake za kuonesha heshima kwa wasanii wa Congo hasa wale wa zamani kama Koffi Olomide na Fally Ipupa, ambao wamechangia sana muziki wa Congo kukua.
Wakati alipokuwa kwenye mahojiano, miaka michache iliyopita aliwahi kuweka wazi kuwa wakati alipokuwa mdogo alipendelea zaidi kusikiliza wasanii kutoka Congo. Akiwemo Koffi Olomide, Papa Wemba, JB Mpiana, na Werra Son, huku akidhihirisha kuwa hiyo ndiyo sababu ya kupenda kutumia sauti za rhumba kwenye nyimbo zake.

Hata hivyo mbali na kuonesha heshima kwa muziki huo na wasanii wake lakini pia amekuwa daraja katika kuunganisha wasanii wa Congo na Tanzania huku akijikita zaidi katika kufanya nao kolabo ambazo zimekuwa zikifanya vizuri ndani na nje ya nchi.
Jicho lake la kuunganisha muziki wa Bongo Fleva na Rhumba ya Congo lilianza kwa msanii Fally Ipupa akimshirikisha kupitia wimbo ‘Inama’ ambao umefanikiwa kutazamwa zaidi ya mara milioni 148 kupitia mtandao wa Youtube.
Wimbo huo uliokuwa mchanganyiko wa Bongo Fleva na Afro-Rhumba ulivuma sana katika nchi za Afrika Mashariki, Magharibi, na hata Ulaya huku challenge yake ikikubalika zaidi kutokana na mtindo wake wa uchezaji.
Harakati zake za kuufanya muziki wa Bongo Fleva kusambaa na kupata ushawishi mkubwa uliendelea mwaka 2019 alipojitosa tena kufanya kolabo na kijana mdogo anayekimbiza katika muziki wa Rhumba Innoss’B wakitoa wimbo uitwao ‘Yope Remix’.

'Yope Remix' ni moja ya kolabo kubwa zaidi za Diamond Platnumz na msanii kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Innoss’B. Wimbo huo ni remix ya wimbo wa awali wa Innoss’B ulioitwa 'Yope', lakini baada ya Diamond kushirikishwa, ngoma hiyo ilipata mafanikio makubwa zaidi na kuvuma kimataifa.
Ikiwa na miaka mitano mpaka kufikia sasa Yope Remix imetazamwa zaidi ya mara milioni 246 katika mtandao wa YouTube.
Hakuishia hapo wakati wa janga la Covid-19 mwaka 2020 Diamond aliachia wimbo akiwa na Koffi Olomide 'Waah'. Wimbo huo ulifanikiwa kuondoka na rekodi zake ikiwemo kutazamwa mara milioni 1.2 ndani ya saa 8, ikifikisha milioni 10+ kwa siku 7 huku kwa sasa umetazamwa zaidi ya mara milioni 130 YouTube.
Aidha Diamond na Koffi Olomide, walirudi tena studio mwaka 2023 ambapo waliachia kolabo ya pili iitwayo ‘Achii’. Baada ya kupata mafanikio makubwa kwenye ‘Waah’ wimbo huo ukipata milioni 1+ ndani ya saa 24, na kuwa trending Afrika Mashariki na Kati. Hata hivyo mpaka kufikia sasa ngoma hiyo ikiwa imetazamwa mara 40.

Diamond ameendelea kuiaminisha jamii kuwa yeye si msanii wa kawaida bali ni nguzo muhimu katika muziki wa Afrika. Ushirikiano wake na mastaa wa Congo kama Fally Ipupa, Innoss’B, na Koffi Olomide umeimarisha nafasi yake katika soko la kimataifa huku ukionesha jinsi anavyoheshimu na kuthamini muziki wa Soukous na Lingala.
Leave a Reply