Kabla ya kuwa mastaa walifanya kazi hizi

Kabla ya kuwa mastaa walifanya kazi hizi

Maisha yanachangamoto zake, na siyo kila tajiri au mtu maarufu alizaliwa katika mazingira hayo. Wengi wao walianza kujitafuta chini lakini sasa wameuteka ulimwengu kwa majina yao, fahamu zaidi kazi za mastaa hawa kabla hawajauteka ulimwengu

Nicki Minaj (muhudumu wa mgahawa)
Wakati sasa akijivunia umaarufu na mafanikio yake ambayo yametokana na muziki wa Hip Hop. Minaj alipokuwa shule ya upili alifanya kazi kama muhudumu wa mgahawa wa ‘Red Lobster’.

Mwanamuziki huyo alikuwa akifanya kazi hiyo baada ya kutoka shule, kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake na familia yake. Hata hivyo, alifukuzwa kazi katika mgahawa huo baada ya kuwatolea ishara ya matusi wateja waliomuibia kalamu yake.

“Ilikuwa ni suala la msimamo, ninapenda kushughulika na watu, lakini sipendi ujinga mwingi. Hivyo labda huduma kwa wateja haikuwa kazi bora kwangu,” Minaj aliiambia GQ mwaka 2014.

Cardi B (muhudumu wa duka la vyakula)

Maisha hayakuwa marahisi kwa staa Cardi B licha ya kufanya vizuri katika shule ya upili huku akijiunga katika chuo cha Jamii. Lakini baada ya kumaliza muda wa darasani alifanya kazi kama muhudumu wa duka la vyakula kwenye ‘Amish Market’.

Rapa huyo aliyewahi kunyakuwa tuzo mbalimbali wakati alipokuwa kwenye mahojiano na Fader mwaka 2016, alikumbushia jinsi alivyohangaika kufanya kazi ambazo zingempa ujira mdogo.

“Nilikuwa nikifanya kazi wiki nzima na bado nilikuwa napata kama dola 250 tu.” Akiwa na uhitaji wa pesa zaidi, alihamia kufanya kazi katika klabu ya usiku kabla ya kuwa mmoja wa marapa wa kike waliopata mafanikio makubwa zaidi katika historia.

Dwayne Johnson ‘The Rock’ (Kuosha vyombo mgahawani)

Maisha ya nyota wa filamu ya The Fast & Furious franchise, The Scorpion King, Jumanji: Welcome to the Jungle hayakuwa mepesi. Kwani kabla ya kupata umaarufu na kujipata alikuwa akifanya kazi ya kuosha vyombo katika migahawa.

Mwezi Novemba 2015, kabla ya hajaweka wazi suala hilo katika kipindi chake cha ‘Oprah’s Masterclass’, The Rock alichapisha picha akiwa anaosha vyombo, huku akiandika kwenye Twitter, “Kazi yangu ya kwanza ilikuwa nikiwa na miaka 13, nikiosha vyombo kutoka saa 9 alasiri hadi 5:30 usiku kila siku. Ndiyo, hata siku hizi bado naosha kila chombo,”aliandika

Mwigizaji huyo aliacha kazi hiyo na kwenda kuwekeza nguvu katika kujifunza mpira wa miguu lakini ndoto yake ya kuwa mcheza soka ilikufa na kuhamia katika ulimwengu wa wrestling (mapigano ya kitaalamu). Ambapo alifanya jina lake kuwa maarufu.

Alifanikiwa sana katika WWE (World Wrestling Entertainment), na baadaye akaanza kuigiza katika filamu na kuwa mmoja wa nyota wakubwa wa Hollywood.

Will Smith (kusambaza magazeti)

Kabla hajawa nyota mkubwa katika filamu mbalimbali zinazofanya vizuri duniani. Kazi yake ya kwanza alikuwa akimsaidia baba yake kuuza na kutengeneza majokofu. Licha ya kupambana katika biashara hiyo ndipo akaamua kuanza kusambaza magazeti kama kazi ya pili ili aweze kupata kipato cha ziada.

Uzoefu huo unaelezwa kuwa ulimfundisha thamani ya kufanya kazi kwa bidii kabla ya kuanza taaluma ambayo imempatia mafanikio na kutambulika zaidi ambayo ni muziki na uigizaji.

Kanye West (kuuza nguo)

Akitangazwa kuingia katika orodha ya mabilionea kutokana na mafanikio yake katika muziki, na biashara kazi ya kwanza ya mwanamuziki Ye ilikuwa ni muuzaji wa nguo katika duka la ‘Gap’.

Katika mahojiano ya 2015 na Paper, alifunguka kuwa kazi hiyo ilimpa mtazamo wa ubunifu huku ikiwa daraja katika safari yake ya biashara ambapo kwa sasa anamiliki kampuni ya mavazi ya ‘Yeezy’.

50 Cent (muuzaji wa madawa ya kulevya)
Kabla ya kujiingiza katika muziki miaka ya 2000 mwakamuziki Curtis James Jackson III ‘50 Cent’alikuwa akifanyabiashara mitaani akiuza dawa za kulevya.

Msanii huyo aliishi katika mazingira magumu katika mtaa wa Queens, New York, hata hivyo alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha miezi michache kwa kosa la kumiliki madawa ya kulevya.

Baada ya kutolewa jela, alijikita kwenye muziki, ambapo alijulikana sana baada kutoa albamu yake maarufu ya ‘Get Rich or Die Tryin' mwaka 2003. Albamu hiyo ilimfanya kuwa mmoja wa wasanii maarufu wa hip-hop duniani kote.

Mastaa wengine ni pamoja na Kevin Hart (muuzaji wa viatu pamoja na mshauri wa mazoezi katika gym), Harrison Ford (mchonga mbao), Eminem (muoshaji wa vyombo migahawani), Taylor Swift akifanya kazi shamba la miti ya Krismasi lililomilikiwa na baba yake.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags