Kolabo Zatajwa Kuwapeleka Wasanii Wa Afrika Kimataifa

Kolabo Zatajwa Kuwapeleka Wasanii Wa Afrika Kimataifa

Mojawapo ya sababu kuu zinazochochea ukuaji wa muziki wa Afrika katika soko la kimataifa inatajwa kuwa ni ushirikiano ‘kolabo’ kati ya wasanii wenyewe kwa wenyewe kutoka katika eneo husika. Huku ikitajwa kuwa huwenda ikawa chachu ya kuleta Grammy nyingi Afrika.

Suala hilo limetiliwa mkazo na Mkuu wa Muziki wa Spotify kwa Afrika Kusini na Jangwa la Sahara, Phiona Okumu, katika ripoti mpya ya ‘Spotify Global Impact 2025 in Sub-Saharan Africa’.

Phiona alieleza kuwa wasanii wa Afrika wameonyesha kuwa mafanikio yanapatikana katika kufanya kolabo na sio kushindana.

“Kwa kufanya kazi pamoja ‘kolabo’, hawabadili tu sauti ya muziki wa kimataifa bali pia wanaonyesha utofauti na vipaji vya Afrika kwa hadhira ya dunia nzima," alisema.

Aidha aliongeza kuwa Afrika sasa imepata sura mpya katika muziki duniani hivyo wasanii wanatakiwa kuwekeza nguvu katika mshikamano kati ya wasanii.

Miongoni mwa mifano iliyoainishwa kwenye ripoti hiyo ni wimbo wa "Komasava" kutoka kwa Diamond Platnumz, aliowashirikisha wasanii wa Afrika Kusini Chley na nyota wa Amapiano Khalil Harrison.

Wimbo mwingine ukiwa ni "One Call" wa DJ na mtayarishaji wa muziki Spinall, akiwa na Tyla, nyota chipukizi wa Afrika Kusini, na mwimbaji kutoka Nigeria Omah Lay. Vilevile kolabu ya Tyla na Tems, wimbo uitwao "No 1", ambao umefanya vizuri na kuvuma kimataifa, ukisikilizwa takribani mara milioni 36 duniani kote.

Mbali na nyimbo hizo zilizoorodheshwa lakini pia ngoma nyingine ambazo zinaendelea kufanya vizuri ni pamoja na ‘Continental’ wa King Promise aliomshirikisha Shallipopi kutoka Nigeria, ambao umejipatia nafasi kwenye orodha ya Global Impact.

Mwingine ukiwa ‘DIGII III Trailer’ kutoka kwa Mr Tee, Tenorboy, na mtayarishaji wa muziki Chacha, ndio wimbo unaosikilizwa zaidi kimataifa kutoka Kenya, ikionyesha jinsi muziki wa Afrika unavyozidi kushika kasi duniani.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags