Peter Akaro
Je, huwa unajifunza nini pindi unapotazama video za muziki?, au kwako ni kama kufurahisha macho yako tu?, ila una paswa kujua kuna nyimbo ambazo video zake zinabeba maana zaidi ya kile unachosikiliza na moja wapo ni yake AY, Dan'hela (2020).
Hata hivyo, kwa bahati mbaya video nyingi za muziki kwa sasa hazina stori yoyote ndani tofauti na hapo awali, waandaji (music directors) na wasanii wenyewe wamejikita zaidi kwenye ubora wa picha na rangi za kuvutia.
Katika video hiyo ya AY ambayo imeongozwa na Director Kenny, ndani yake kuna noti (AY0042290) ambayo ina matumizi mengi na pia inatupa somo fulani la uchumi.
Wimbo huo pamoja na video hiyo vinaeleza jinsi fedha ilivyo kitu cha kumtesa binadamu katika kuitafuta hadi kuipata, AY anaitaja hela kama mwanamke aliyempa jina la 'Dan'hela' ambaye anautesa moyo wake na hajui ni siku gani atafurahi naye.
Vilevile ameonyesha jinsi hela inavyohama kwa mtu mmoja na kwenda kwa mwingine na kila moja akiwa na matumizi yake, huyu anaitafuta kwa ajili ya kula, yule kwa ajili ya anasa.
AY akiwa anaimba mtaani, watu mbalimbali wanavutiwa na muziki wake na kimtunza fedha nyingi, kati ya hizo anapatiwa noti inayotambulika kama AY0042290 na kuitia kibindoni.
Baada ya kumaliza kutumbuiza, bila kujua AY anaenda dukani na noti hiyo kununua maji ya kunywa, mwenye duka naye anatoa noti hiyo kwa mke wake ambaye anaenda feri kununua samaki.
Aliyeuza samaki jioni anafunga biashara na kurejeaa nyumbani, anaitoa noti hiyo kwa konda wa daladala, naye konda anaenda kukabidhi noti hiyo na nyingine kwa bosi wake, yaani mmiliki wa dadadala.
Naye bosi anachukua noti hiyo na nyingine na kutoka usiku kwa ajili ya kwenda kupata burudani viwanja, huko anamkuta AY akitoa buradani, anavutiwa na muziki wake na kuamua kumtunza, anampatia noti hiyo na nyingine kadhaa.
Mwishoni AY anazichukua na kundoka zake, kesho yake anaenda kanisani kutoa shukrani kwa kupata riziki, anatoa noti ile ya mwanzo kabisa 'AY0042290 aliyonunulia maji kwenye chombo cha sadaka na kuondoka zake, na huo unakuwa mwisho wa video hiyo.

Leave a Reply