Dokumentari iliyopewa jina la 'Whitney Houston in Focus' imeibua mengi kuhusu mwanamuziki huyo wa Soul, RnB na Pop kutokea Marekani ikielezea maisha yake kabla ya kuwa maarufu kupitia nyimbo zake kuanzia miaka ya 1980.
Mradi huo unatokana na kitabu cha mpiga picha, Bette Marshall aliyefanya kazi na Whitney kabla ya umaarufu wake mkubwa chini ya usimamizi wa Clive Davis kupitia lebo ya Arista Records.
Moja ya mambo yaliyoibuliwa katika makala hayo, ni jinsi Mkurugenzi wa CBS Records, Al Teller ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa Clive alivyopoteza nafasi ya kumsaini Whitney wakati bado akiwa kijana mdogo na kusema anahitaji kukua zaidi kimuziki.
Kulingana na mtandao wa Page Six, dokumentari hiyo inadai kuwa Whitney akiwa na kiu kubwa ya kufanya muziki, aliwahi kufanya jitihada nyingi ili asainiwe na CBS Records lakini kwa bahati mbaya Teller alimkataa.
"Huo huenda ulikuwa uamuzi alioujutia zaidi Teller maishani mwake, kuwa sehemu ya mwanzo wa safari ya Whitney ilikuwa ni zawadi kwake," alisema Marshall katika dokumentari hiyo.
Dokumentari ya Whitney In Focus, imeandikwa na kuongozwa na Benjamin Alfonsi na kutayarishwa kwa ushirikiano na Audra McDonald ambaye ni mwigizaji na mwanamuziki huko Marekani.
Kwa mara ya kwanza ilionyeshwa katika tamasha la Doc NYC 2023 na sasa inapatikana kupitia majukwaa ya televisheni ya Starz na kwingineko.
Mbali na mahojiano, dokumentari hiyo pia inajumuisha picha ambazo hazijawahi kuonekana hapo awali za Whitney akiwa bado binti zilizopigwa na Marshall kuanzia mwaka 1982 hadi 1986.
Ikumbukwe Whitney baada ya kusainiwa Arista Records na Clive Davis, alianza kufanya vizuri na albamu yake ya kwanza, Whitney Houston (1985) ambayo ilishika namba moja katika chati ya Billboard 200 kwa muda wa wiki 14.
Vilevile albamu hiyo ilitoa nyimbo zake maarufu kama Saving All My Love, How Will I Know na Greatest Love of All ambazo zilishika namba moja Billboard Hot 100, ikiwa ni albamu ya kwanza na msanii wa kwanza wa kike Marekani kufikia rekodi hiyo.
Baadaye alitoa filamu, The Bodyguard (1992) iliyokuja na wimbo wake 'I Will Always Love You' ulioshika namba moja Billboard Hot 100 kwa wiki 14, ukishinda tuzo mbili za Grammy 1994 na hadi sasa unatambulika kama wimbo uliouza zaidi duniani kwa muda wote.
Na baada ya miaka mingi ya mafanikio katika tasnia, Februari 11, 2012, Whitney alifariki akiwa na umri wa miaka 48 huko Los Angeles, mwili wake ulikutwa katika chumba cha hoteli ya Beverly Hills, huku matumizi ya dawa za kulevya yakitajwa kusababisha kifo chake.
Leave a Reply