Alianza kufanya vizuri kwenye muziki akiwa bado ni kijana mdogo, uwezo wake wa kuandika mistari kwenzi na kuichana vilivyo ulimpatia umaarufu kwa wasanii wengine hasa wa Hip Hop Bongo kabla ya mashabiki kumjua.
Huyu ni mshindi wa tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2014 kama Msanii Bora Chipukizi, na miongoni mwa wasanii wa Hip Hop waliofanya vizuri kwenye Fidstyle Friday Show mwaka 2012. Na huyo ndiye Young Killer.
Kabla ya kuanza kutumia jina la Young Killer mwanzoni alikuwa akitumia jina la Lil K, hivyo rapa huyo ni miongoni mwa wasanii waliokuja kubadili majina yao ya awali. Wasanii wengine ambao wameshafanya hivyo ni kama Sugu (2Proud), Joh Makini (Rapcha), Professor Jay (Nigga Jay) na Nyandu Tozzy (Dogo Hamidu).
Ndoto kubwa ya Young Killer kimuziki ni kufanya kolabo na msanii wa Marekani Bow Wow, huku Rosa Ree ndoto yake ni kufanya na Jay Z kutokea Marekani pia. Cha kuvutia ni kwamba Young Killer na Rosa Ree wameshafanya kolabo na marapa wakubwa kutoka Afrika Mashariki ambao ni Fid Q na Khaligraph Jones.
Wakati Young Killer akitumia jina Lil K alitoa wimbo, Winner (2012) ambao alimshirikisha Barakah The Prince, hiki ni kipindi ambacho Barakah alikuwa akijiita Dogo Baraka, hivyo hawa wote walikuja kubadili majina yao.
Wimbo huo uliotengenezwa na Maprodyuza wawili ambao ni Duke Tachez na Deey Classic, wakati wakushuti video yake mara ya kwanza Dogo Baraka alikataliwa kushuti baada ya kuibuka location akiwa amepaka rangi kwenye nywele.
Baada ya Young Dee kujitoa kwenye kundi la Mtu Chee, Young Killer ndiye aliyechukua nafasi hiyo, wimbo wa kwanza kushiriki ndani ya kundi hilo alilokuwepo Stamina na Country Boy, unaitwa Mtu Tatu (2015).
Kwenye video ya wimbo huo Jux hakuonekana ambaye ndiye aliyeimba kiitikio cha wimbo huo, hiyo ni mara ya pili kwa Young Killer kukutana na kitu kama hicho, kwani video ya wimbo wake, 13 (2014) ambayo Belle 9 aliimba kiitikio hakuonekana pia.
Katika wimbo, Mrs Superstar (2013), Young Killer anaamini hawezi kuwa na Vanessa Mdee maana; 'hawezi kuishi KISELA', miaka minne baadaye Vanessa akatoa wimbo uitwao Kisela (2017) akimshirikisha Mr. P (P-Square) wa Nigeria.
Na kati ya warembo wote aliyowataja katika wimbo huo akielezea kutamani kuwa nao, ni Mwasiti pekee ndiye anaendana naye kutokana huyu amewahi kushinda tuzo ya TMA 2006 kama Msanii Bora Chipukizi sawa na Young Killer kwa mwaka 2014.
Vesi aliyochana Young Killer kwenye wimbo wa Diamond Platnumz 'Pamela' kutoka katika albamu yake ya tatu, A Boy From Tandale (2018), ilimchukua siku tatu kuiandika hadi kukamilika.
Hata hivyo, si utaratibu wake kutumia muda mrefu hivyo kwenye kuandika bali ni kutokana na uzito wa nafasi aliyopewa na staa huyo wa WCB Wasafi na mshindi wa MTV EMAs mara tatu.
Pia Young Killer mwenye albamu moja, Super Nyota (2022) alitumia dakika 45 pekee kuandika wimbo wake, True Boya (2017) ambao ulikuwa ni diss kwa Nay wa Mitego aliyemchana kwenye ngoma yake, Moto (2017).
Ukiachana na muziki, Young Killer ni mchezaji mzuri wa mpira wa miguu, hiyo ni sawa na Alikiba ambaye alicheza hadi Ligi Kuu Soka Tanzania Bara akiwa na Coastal Union, pia Ruby aliyeichezea Young Twiga Stars.
Young Killer na Nandy ni miongoni mwa wasanii wachache Bongo wanaotumia mkono wa kushoto kuandika, hivyo maishairi unayoyasikia katika nyimbo zao yameandikwa na mkono wa kushoto.
Wasanii wengine duniani wanaotumia mkono wa kushoto kuandika ni pamoja na Justine Bieber, Angeline Jolie, David Bowie, Paul McCartney na Lady Gaga, mshindi wa Grammy mara 14 huku akiuza rekodi zaidi ya milioni 170 duniani kote.

Leave a Reply