Chama cha Usambazaji Filamu Tanzania kimeungana rasmi na Chama cha Maktaba za Video Tanzania kwa lengo la kutoa huduma ya usambazaji wa filamu kwa wananchi katika ngazi zote, wakiwemo wale wasio na simu janja ‘kiswaswadu’.
Ushirikiano huo umezinduliwa Agosti 14, 2025 jijini Dar es Salaam, katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya filamu nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Chama cha Maktaba za Video Tanzania, Peter Zakaria amesema muungano huo utasaidia kukuza soko la filamu ndani na nje ya nchi pamoja na kupambana na wizi wa kazi za wasanii
“Watengenezaji wa filamu watapata hadhira kubwa zaidi na kupunguza uharamia wa kazi za kisanaa. Pia watu wa maktaba watanufaika kwa kupata kipato halali kupitia muungano huu," amesema Zakaria.
Kwa upande wake Katibu Kiongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Fadhili Mfate amesisitiza kuwa mafanikio ya Ushirikiano huo yatategemea mshikamano miongoni mwa wanachama.
“Jambo lolote ili ufanikiwe linahitaji umoja. Tukiwa na umoja kila mmoja atapata kile anachotarajia, kwa sababu tumeanza kwa umoja nina imani tutafika kama tulivyopanga," amesema Mfate.
Aidha Mfate amehimiza umuhimu wa kila mwigizaji kuwa mwanachma wa chama cha filamu ili kurahisisha usambazaji wa kazi zao na kuimarisha ulinzi wa haki zao za kimtandao na kifedha.
Muungano huo unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuinua tasnia ya filamu Tanzania kwa kuzingatia mabadiliko ya Teknolojia na uhitaji wa soko.

Leave a Reply