Msanii wa muziki wa hip-hop nchini, Conboi ambaye kwa sasa anatamba na ngoma ya 'Tilalila' aliyomshirikisha Marioo, ameelezea sababu ya kuchelewa kutoka kwa wimbo huo licha ya kutangazwa kwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwananchiscoop leo Aprili 15, 2025 amesema Tilalila ilichelewa kwa sababu ya maandalizi ya muda mrefu.
"Unajua namna ya kutangaza wimbo inatakiwa iwe wiki mbili na zaidi, ili ifike kwenye majukwaa yote kwa wakati, ili iweze kupitiwa vizuri. Ni mambo ya maandalizi ya wimbo tu, lakini pia ukiangalia tulikuwa kwenye Kwaresma na Ramadhani kwa hiyo watu wakiwa katika mfungo inakuwa ngumu ngoma kufanya vizuri zaidi," amesema Conboi.
Conboi ameongezea kuwa kolabo hiyo ina maana kubwa kwani Marioo ni msanii namba moja kwa sasa.
"Kwangu ina maana kubwa sana kwa sababu Marioo anafanya kazi nzuri, kwangu ni msanii namba moja. Mashabiki wangu walikuwa wanategemea kumuona Conboi akishirikiana na wasanii tofauti tofauti kwa sababu ukiangalia katika katalogi yangu huwezi kuona nimeshirikiana na wasanii wengi.
"Nimekuwa nikifanya hip-hop zaidi, lakini kwahivi sasa nimeona nianze kuwapa watu kwa angle tofauti tofauti katika utumbuizaji, muonekano na hata mimi binafsi," amesema.
Licha ya mafanikio katika mapambano yake Conboi amesema, bado hana meneja anayesimamia kazi zake.
"Sina meneja mpaka sasa mtu yeyote ambaye nafanya naye kazi na kushirikiana sio meneja wangu. Lakini namshukuru Mungu vitu vinanyooka kama hivi," amesema Conboi.

Leave a Reply