Mwanamuziki Diamond Platnumz tayari amemaliza ziara yake nchini Uingereza baada ya kupiga shoo tatu kwenye miji mikubwa nchini humo ambayo ni London, Manchester na Glasgow ambapo sasa kituo kinachofuata ni Marekani.
Diamond alianza ziara hiyo Ijumaa, Juni 13,2025 jijini London, katika ukumbi wa Royal Albert wenye uwezo wa kuchukua mashabiki zaidi ya 5000, na kumfanya msanii huyo kuweka historia mpya ya kuwa wa kwanza kutoka Afrika ya Mashariki kuujaza ukumbi huo ambapo mamlaka ya ukumbi huo ilimkabidhi cheti kama sehemu ya pongezi kwake.
Siku iliyofuata Jumamosi, Juni 14, 2025, mkali huyo wa Bongo Fleva aligawa dozi ya burudani jijini Manchester, katika ukumbi wa Manchester Academy. Pia Jumatatu, Juni 15, 2025, alikiwasha Glasgow katika ukumbi wa Swag3.
Mapokezi ya shoo zake zote tatu yalikuwa makubwa, akiwaburudisha mashabiki na nyimbo zake hit za kuanzia miaka ya 2015 mpaka 2025 kama vile Fire, Marry You, Make Me Sing, Shuu, Waah na Komasava.
Hatahivyo, Diamond Platnumz baada ya kukata kiu ya mashabiki wake nchini Uingereza, jana Jumanne, Juni 17, 2025, aliambatana na timu yake kuelekea nchini Marekani kwaajili ya Tamasha kubwa la mzuki la HOT 97 Summer Jam 2025.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Ijumaa, Juni 20, 2025, katika ukumbi wa Prudential Center Arena, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 16,755.
Diamond ataungana na mastaa wengine wakubwa kutokea sehemu mbalimbali duniani wakiwemo Boogie, Gunna, GloRilla, Muni Long, Asake, Ayra Starr, Ja Rule, Kash Doll, Bobby Konders & Jabba ft. Masicka, Jim Jones, Cash Cobain, 41 (Kyle Rich, Jenn Carter, Tata).
Msanii wa kwanza tokea Afrika kutumbuiza kwenye Hot 97 Summer Jam alikuwa Davido mwaka 2018. Pia alitumbuiza tena mwaka mmoja baadaye na kumfanya kuwa msanii wa kwanza wa Kiafrika kutumbuiza kwenye Summer Jam mara mbili.
Tamasha la Hot 97 Summer Jam kwa mara ya kwanza lilifanyika Juni 21, 1994, kwenye Uwanja wa Brendon Byrne ambao sasa unafahamika kama Meadowlands Arena huko Mashariki ya Rutherford, New Jersey, likiongozwa na kituo cha habari cha hip-hop kutokea New York cha Hot 97.
Utakumbuka, katika ziara yake katika nchi hizo, Diamond Platnumz ameongozana na baadhi ya wanafamilia yake pamoja na wanamuziki wakiwemo Jux, Ommy Dimpoz na Babalevo.

Leave a Reply