Diamond kutoana jasho na Burna Boy, Asake, Trace Music Award

Diamond kutoana jasho na Burna Boy, Asake, Trace Music Award

Moja ya tukio ambalo linasubiriwa kwa hamu Zanzibar kisiwani Unguja ni ugawaji wa Tuzo za Trace ambazo zinatarajiwa kutolewa kesho Februari 26,2025.

Tukio hilo ambalo lilianza mapema jana Februari 24, 2025 linatarajiwa kuendelea kuwakaribisha mastaa kutoka mataifa mbalimbali.

Katika usiku huo jukwaa litatawaliwa na wasanii wazawa akiwemo Diamond Platnumz, Jux, Zuchu, Harmonize, Alikiba, Marioo, Abigail Chams, Mbosso, Lunya, Bella Kombo na Nandy. Mbali na hao wapo wasanii kutoka nje ya Tanzania kama Rema, TitoM & Yuppe, Joé Dwèt Filé, Fally Ipupa, Didi B, Tyler ICU, Qing Madi, Bien, Innoss’B, Yemi Alade, Black Sherif na wengineo.

Hivyo basi tuzo hizo zitawakutanisha wasanii zaidi ya 300 wa kimataifa huku wakitoana jasho katika vipengele mbalimbali. Ambapo Diamond anakuwa msanii pekee kutoka Bongo anayewania tuzo katika kipengele cha 'Song Of The Year' kupitia ngoma ya 'Komasava'.

Diamond atachuana na Tyler ICU & Tumeloza ft. DJ Maphorisa, Nandipha808, Ceeka RSA, Tyron Dee – Mnike, Asake & Travis Scott – Active, Tam Sir ft. Team Paiya, Ste Milano, Renard Barakissa, Tazeboy, PSK - Coup Du Du Marteau, TiTom & Yuppe - Tshwala Bam, Tems - Love Me Jeje, Burna Boy – Higher, Rema & Shallipopi - Benin Boys na Tyla – Jump.

Hata hivyo, kwa upande wa kipengele cha Msanii Bora Afrika Mashariki wasanii nane watavimbiana huku wasanii wanne wakiwa kutoka Tanzania ambapo wanaowania ni Bien, Zuchu, Rophnan, Diamond Platnumz, Joshua Baraka, Harmonize, Nandy na Marioo.

Lakini pia msanii Young Lunya atatoana jasho na mastaa kutoka mataifa mbalimbali kupitia kipengele cha Best Hip-Hop ambapo anashindanishwa na wasanii kama Suspect 95, Sarkodie, Odumodublvck, Nasty C, Maglera Doe Boy na Didi Bi.

Vilevile katika kipengele cha Best Male Artist in Afrika, Diamond pia atatoana jasho na mastaa kama Asake, Burna Boy, Wizkid, Rema, Fally Ipupa, Stonebwoy na Dlala Thukzin. Lakini pia katika kipengele cha Best Artist in Tanzania wanaoshindanishwa ni Diamond, Zuchu, Nandy, Harmonize, Alikiba, Marioo, Jux na Mbosso.

Aidha vipengele vingine ni pamoja na Album Of The Year, Best Music Video, Best Dj, Best Dancer, Best Collaboration, Best Newcomer, Best Producer, Best Live, Best Gospel Artist na vinginevyo.

Tuzo za Trace zilianza mwaka gani?

Trace Awards & Festival ilianzishwa mwaka 2023 na Trace Group ili kusherehekea maadhimisho ya miaka 20 ya kituo cha televisheni cha muziki cha kulipia cha Ufaransa, Trace TV. Toleo la kwanza la tuzo hizi lilifanyika 21 Oktoba 2023 katika BK Arena, Kigali, Rwanda. Huku toleo linalofanyika Visiwani Zanzibar likiwa la pili tangu kuanzishwa kwake.

Historia ya Trace Music
Trace Music ni sehemu ya Trace Group, kampuni ya kimataifa inayojihusisha na vyombo vya habari, burudani, na tamaduni za vijana, hasa barani Afrika na katika jamii za watu weusi duniani kote.

Trace ilianzishwa mwaka 2003 na Olivier Laouchez, mfanyabiashara wa Kifaransa mwenye asili ya Martinique. Ilianza kama kituo cha televisheni kinachojikita kwenye muziki wa Hip-Hop, R&B, na Afro-urban huku lengo kuu lilikuwa kukuza na kuonyesha vipaji vya muziki kutoka Afrika na diaspora ya Waafrika.

Aidha baada ya mafanikio ya Trace Urban, kampuni ilipanua huduma zake kwa kuzindua vituo vingine kama Trace Africa ( iliyojikita kwenye Afrobeats, Bongo Flava, na Amapiano). Trace Naija (inayoangazia muziki hasa wa Nigeria na mastaa wake kama Davido, Burna, Tiwa na wengineoi), Trace Mziki (Bongo Flava, Gengetone, na Afro-fusion) na Trace Gospel (Kituo cha muziki wa Injili kutoka Afrika na sehemu nyingine za dunia).






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags