DOGO ELISHA: Siamini kwenye kutoa album

DOGO ELISHA: Siamini kwenye kutoa album

Msanii wa muziki wa Singeli hapa nchini Elisha John Daffa maarufu Dogo Elisha ameeleza sababu za yeye kutopenda kutoa album ya nyimbo zake akidai kuwa kufanya hivyo ni kuzuia kusikika kwa nyimbo nyingine.

Akizungumza na jarida la Mwananchi Scoop wakati akifanya mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya Elisha amedai kuwa kwa sasa hafikirii kabisa kutoa album ya nyimbo zake.

“Album kwangu mimi binafsi naona ni kitu ambacho kinanipotezea muundo kwa sababu unaweza ukajikuta unatoa nyimbo nane halafu zisiende zote ikaenda moja au mbili ambazo zimebeba album,” anasema na kuongeza kuwa.  

“Tunaona kwa wasanii wa bongo fleva mtu anaweza akatoa album nzima lakini zikasikika nyimbo chache tu na sio zote.”

Aidha amesema kuwa wasanii wangeamua kuzipa nafasi nyimbo ambazo wanataka kuzitoa zingeweza kuwatambulisha zaidi na kuwasaidia kuongeza kipato kupitia kazi zao.

“Kuna nyimbo ambazo tangu nimerecord Wapoloo hadi sasa hivi zipo studio hazijatoka lakini nina mpango wa kuziachia ila ningesema niachie album watu mngeijua Wapoloo hizo nyimbo zengine zisingesikika,” anasema.

Dogo Elisha ambaye amejizolea umaarufu kupitia muziki wa Singeli katika nyimbo yake ya kwanza iliyomtambulisha kwenye tasnia hiyo inayofahamika kwa jina la ‘Wapoloo’ akiwa amemshirikisha Kiluza Fanani.

Nyimbo hiyo ambayo aliiachia mwaka 2019 ndiyo nyimbo ambayo imeonyesha uwezo wake kwenye tasnia ya muziki huo na kumpa utambulisho mzuri kwa jamii.

“Kiukweli ni nyimbo ambayo ilisababisha vyombo vya habari kuniamini ilikua kila ukisikilza kwenye redio  ndiyo nyimbo ya singeli pekee ambayo 2019 ilikaa Top 10 na kushika nafsi ya kwanza kwa miezi kadhaa  kama ingepatikana nafasi ya kutoa tunzo basi ningepata kwa mwaka huo,”anasema.

Msanii huyo ambaye ana mtindo wa kipekee wa namna anavyoachia ngoma  zake kwa mashabiki zake mara nyingi huachia nyimbo nne kwa kila wiki.

“Huo ndio mtindo wangu na ndivyo ninavyofanya na nina uhakika kila nikitoa nyimbo zangu zinafika sehemu ambayo nimeikusudia ila kama ningetoa album watu wangeifahamu sana hiyo kuliko nyimbo zengine ambazo zingekuwepo,” anasema

Hata hivyo dogo Elisha anaimba Singeli za mitindo yote ikiwemo mfumo wa segere, singeli bakora, pamoja na mtindo wa vinanda ambao huo mfumo wake unakuwa wa taratibu.

“Mimi naimba kila mtindo mwaka jana niliachia wimbo ambao upo kwenye mfumo wa segere unaitwa ‘Nijimwage’ pia nikaachia wimbo wa ‘unanikosha’ nimeonyesha hivyo ili watu wajue kuwa nina uwezo wakuimba kwa mtindo wowote ninaoutaka,” anasema

Vilevile dogo Elisha amebainisha kuwa yeye hajawahi kufikiria kufanya kolabo na msanii yeyote yule wa muziki wa Singeli.

“Mimi ni mtu ambaye sijawahi kufikiria kufanya kolabo na msanii yeyote yule mkubwa wa Singeli au bongo fleva nimefanya na Balaa kipindi ambacho mitaa haimjui Balaa ni nani,” anasema na kuongeza kuwa.

“Zipo ngoma ambazo tulifanya mimi na Balaa ambazo nikiziachia jamii itaelewa nishafanya na Kilunza Wapoloo ikaenda lakini sijafanya kolabo na msanii yoyote yule wa Singeli ambaye ni mkubwa.”

Changamoto inayoikabili Tasnia hiyo kwa sasa

Ameelezea hali ilivyo katika muziki wa Singeli amesema kuwa kwa sasa mambo sio mabaya na hatua iliyofikia ni kubwa sana huku akiviomba vyombo vya habari kujifunza kuweka usawa kwani tasnia hiyo haifanani na mpira wa miguu.

“Muziki sio mchezo wa mpira au ngumi unakuwa na usawa kwenye uzito kwamba huwezi kumpiga mwenzio sehemu fulani ataumia embu mtu ambaye anafanya vizuri apewe nafasi basi aonyeshe uwezo wake,” anasema na kuongeza kuwa

“Sio kwa sababu mtu fulani anatoa pesa kwenye media anapewa nafasi halafu huyu ambaye anafanya vizuri kwenye ngoma yake anawekwa pembeni, jua kabisa unaua kipaji cha mtu,” anasema.

Vilevile ameeleza kuwa kama vyombo vya habari vitazingatia hayo na kuacha ku-balance muziki wa Singeli itasidia  kufikisha muziki huo mbali zaidi kwenye tasnia hiyo.

Hata hivyo dogo Elisha ameweka wazi kuwa hatoweza kuimba muziki mwengine wowote tofauti na Singeli.

“Kwenye masuala ya muziki hata mikoani nyimbo zinazopigwa sana ni Singeli hivyo ni muziki ambao unapewa nafasi kubwa sana mtaani tofauti na bongo fleva,” anasema na kuongeza kuwa

“Ndiyo maana hakuna show ambayo itawekwa bila kuitwa wasanii wa Singeli kwa sababu wanajua umuhimu wa muziki huu,” anasema.

Matarajio yake katika muziki wa Singeli

Vilevile msanii huyo ameweka wazi matarajio yake katika muziki huo  kuwa anahakikisha anafika mbali zaidi na kuwa mkubwa kuliko msanii yeyote yule kwenye tasnia hiyo.

“Nataka watu wajue zaidi kipaji changu na uwezo nilionao ili tuweze kuufikisha kwenye kiwango cha juu muziki wa Singeli,” anasema.

Dogo Elisha ni msanii ambaye anatunga mashairi ya nyimbo zake mwenyewe na jumla nyimbo zake alizoandika hadi sasa ni zaidi ya 20.

Hata hivyo msanii huyo amewaomba wasanii wa tasnia ya muziki wa Singeli kuacha kutumika kupitia show mbalimbali ambazo zinaandaliwa na watu wakubwa.

“Tunajua kama tunatumiwa sana wakiandaa project zao tunaenda ili kusogeza muziki wetu sehemu fulani lakini hakuna mtu ambaye anafurahia kutumika,” anasema

Vilevile amesema kuwa kwa  sasa wanafanya kazi  kwa kuandaa project zao binafsi ili kuhakikisha na wao wanapata kipato chao binafsi pasi na kubugudhiwa na mtu.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post

Latest Tags