Jaivah alivyoikamilisha kolabo ya Wurld na Marioo

Jaivah alivyoikamilisha kolabo ya Wurld na Marioo

Mwanzoni mwa wiki hii msanii wa Afrobeat kutokea nchini Nigeria, Wurld alichapisha video kwenye ukurasa wake wa Instagram ikimuonesha yupo studio na wakali wa Bongo Fleva, Marioo na Jaivah. 

Video hiyo ilisindikizwa na maneno yaliyosadifu kuwa wakali hao wana kazi ya pamoja inayotarajiwa kutoka hivi karibuni. 

Wiki hii Mwananchi Scoop  imepiga stori na Jaivah  na ameeleza walivyokutana na kufanyakazi na msanii huyo wa Nigeria. 

"Kama ilivyo kawaida sisi ni wasanii na tunakutana mara nyingi. Wurld alikuwa Bongo na aliwasiliana na Marioo na walitamani niwepo pia kwenye huo mradi. Japo sijafanya kitu kikubwa, Marioo ndio ameimba sana," amesema Jaivah.

Jaiva ameendelea kusema katika ngoma hiyo amehusika kwa kiasi kidogo ambapo ameshiriki kupiga mluzi na kuandaa baadhi ya melody za wimbo huo. 

"Katika kusaidiana kama wasanii. Mimi nimehusika kwa kupiga mluzi kwenye hiyo ngoma, kuna mluzi ambao unasikika mimi ndio nimeupiga lakini pia baadhi ya melody na kuwekana sawa kama wasanii nimehusika," amesema Jaiva. 

Ameongezea kuwa ngoma hiyo imeandaliwa hapa nchini mwaka 2024 

"Wurld kafika mwaka jana, kipindi kile ambacho alikuja Bongo ndiyo tulifanya naye kazi hiyo na alipofika alimcheki Marioo kwaajili ya kushirikina kwenye ngoma ya pamoja. Marioo pia aliona umuhimu wangu wa kushiriki humo hivyo akanisanua na mimi nikajiunga kwenye ngoma hiyo," amesema Jaivah.

Jaiva amesema yeye na Marioo wamekuwa na muunganiko mzuri pindi wanapokutana kwenye ngoma ya pamoja hivyo wanafikiria kuja na album au Ep ya pamoja. 

"Yeah tumewaza kama wasanii ambao tuna muunganiko mzuri pindi tunapokutana, na tayari kazi zipo kwahiyo kama itawezekana zitatoka bila shida yoyote. Lakini hapa mwanzo kuna nyimbo ziliongozana, pia tuliamua kuzitoa moja moja baadala ya kutoa kama EP,” amesema Jaiva. 

Hata hivyo, msanii huyo ambaye anatamba na wimbo wake wa Kautaka ambao umetoboa zaidi mpaka nchi za magharibi mwa Afrika, amesema mtindo wake wa kuimba ndiyo unawabamba mashabiki. 

"Nadhani ni style tu ambayo nimekuwa nayo kwenye muziki inawabamba sana. Lakini nadhani Melodies zangu ni kali kwa hiyo zinawavutia zaidi na wanatamani kunisikiliza, muda mwingine ni maneno ambayo mara nyingi nimekuwa natumia kama 'Kautaka' na baadhi ya maneno ambayo yanafanana na tamaduni zao," amesema Jaivah.

Amesema mafanikio ambayo amekuwa akiyapata ni pamoja na koneksheni kutoka kwa wasanii wengine wakubwa na kuusambaza muziki wake ulimwenguni. 

"Nazungumzia kikazi zaidi nadhani ‘connection’ ni kubwa zaidi kwasababu kazi zangu zinapokuwa zinatambulika sehemu kubwa za duniani inakuwa rahisi mimi kufanya shughuli zangu za kimuziki," amesema Jaivah. 

Hata hivyo Jaivah amesema kati ya mipango yake kwa 2025 kuachia albumu yake ya kwanza. 

"Nimepanga kuachia album mwaka huu. Album hiyo itakuwa na nyimbo tofauti tofauti na hiyo itakuwa imelenga  soko la muziki wa kimataifa,"

Amesema album yake imechukua muda mrefu kutoka baada ya Ep yake ya kwanza ya 'Vibe Ep' ya 2021. Sababu alitaka kutengeza mashabiki waelewe mtindo wake wa muziki. 

"Kila kitu kinaenda kwa muda sahihi na mipango kwahiyo hakuna kuchelewa lakini kubwa nilitaka mshabiki waelewe aina na mtindo wangu wa muziki na nimefanikiwa kwa hiyo ni muda sahihi kuwabariki album.

"Hivyo basi watarajie tu muziki mzuri na ukuaji kwangu kwa sababu napambana ili kufikisha muziki wetu mbali zaidi," amesema Jaivah.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags