Jinsi Ya Kupika Nyama Ya Foil

Jinsi Ya Kupika Nyama Ya Foil

Nyama ya foil ni aina ya mboga inayopendwa na watu wengi zaidi hasa wakienda katika migahawa mikubwa. Nyama hiyo hupikwa kwa kutumia foil na sio sufuria kama ambavyo watu wamezoea, imekuwa ikiwakosha wengi kutokana na ladha yake. 

Licha ya msosi huo kuuzwa sehemu mbalimbali na kwa bei ya juu bado una nafasi ya kujifunza kupika ukiwa nyumbani kwako kwa muda mchache tu, lakini pia inaweza ikawa fursa ya biashara kwako wewe msomaji wetu. 

MAHITAJI

  1. Nyama kilo moja au zaidi
  2. Foil kubwa ya kutosha
  3. Soya Sosi
  4. Vitunguu maji vikubwa kuanzia 5-10
  5. Mafuta ya kupikia robo
  6. Vitunguu swaumu 3, tangawizi kubwa mbili na ndimu au limao za kutosha
  7. Hoho na karoti za rangi tofauti
  8. Chumvi kiasi na vinegar
  9. Viungo vya mchuzi kijiko kimoja 

Katika upikaji wa nyama ya foil kuna aina nyingi ambapo wengine wanaanza kwa kuchemsha nyama halafu wanaitengeneza huku wengine wakiimarinate na baada ya muda wanaipika.

NAMNA YA KUTENGENEZA  

Hatua ya kwanza: Chukua viungo vyako ambavyo ni vitunguu maji kiasi, tangawizi, kitunguu swaumu chote, viungo vya mchuzi, pilipili manga utaongeza mafuta kiasi kisha utasaga mchanganyiko wako na utauweka pembeni. 

Hatua ya pili: Utachukua nyama yako utaiosha vizuri kisha utatia chumvi kiasi, ndimu ya kutosha utachukua mchanganyiko wako ambao umeusaga uweke kwenye nyama, baada ya hapo utachanganya mpaka viungo viingine kabisa. Kisha utaifunika kwenye chombo ambacho hakipitishi hewa kwa saa kuanzia 6-8 au hata kwa usiku nzima. 

Hatua ya tatu: Baada ya kuimarinate nyama yako utawasha oven ili lianze kupata moto lakini kama hauna unaweza kuwasha jiko lako la mkaa na uliache lipate moto kabisa. Kisha kata foil kubwa anza kuweka vitu vyako kwa mpangilio. 

Anza kwa kuweka vitunguu vya kutosha chini kisha weka nyama yako, ukishaweka nyama yote juu weka tena vitunguu, hoho na karoti, vile vile utaongezea maji ya ndimu au limao, pilipili ya kuwasha kiasi, soya sosi pamoja na chumvi kiasi.

Baada ya hapo kunga foil yako vizuri hakikisha haipitishi mvuke sehemu yoyote kisha utaiweka jikoni na upike kuanzia dakika 30-45, na mpaka kufikia hapo nyama yako ya foili itakuwa tayari kwa ajili ya kula na kitu chochote kile ugali, wali, ndizi na hata chipsi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags