Jiongeze: Kasoro Zenye Kasoro

Jiongeze: Kasoro Zenye Kasoro

Aiseee! Hapana hii sasa imekuwa ‘tuu machi’ kwa wasanii wetu. Hivi hawa wamerogwa wajiimbie mapenzi tu? Wamerogwa wacheze tamthiliya na filamu za mapenzi tu? Wamerogwa wazalishe skendo za mapenzi tu?


Imekuwa kero sana kwa sasa. Yaani masikio na macho yamechoka aiseee. Kila mwanamuziki ukitaka kusikiliza au kutazama goma lake, ni mapenzi tu. Ukitaka kusikia au kusoma habari zake ni za mapenzi. "Mapenziniani'.


Ndivyo ilivyo hata kwa wasanii wale wa filamu. Ukitaka kutazama filamu ya msanii wa Kibongo, utakutana na hadithi za mapenzi. Ukitaka kutazama tamthiliya zao ni mapenzi tupu. Hata posti zao mitandaoni ni mapenzi.


Basi utaona isiwe tabu wacha nisome habari zake tu. Kwa udaku wa kurasa za mitandaoni. Ni habari za mapenzi tu. Yaani kila kitu ni mapenzi mwanzo mwisho. Huyu kamtaka yule, na yule wa yule karudi kule kwa yule wa yule na huyu.


Jamani kuna vitu na mambo mengi ya kusikitisha, kufurahisha hata kuhuzunisha. Pia kuna mambo kibao ya kuelimisha, ambayo yanaweza kuwa mbadala wa nyimbo na filamu zenu. Yaani matukio ni mengi yenye mashiko nje ya mapenzi.


Unaweza kutoka Mtwara mpaka Arusha, kisha Mwanza, Kigoma mpaka Rukwa. Ukatokea Tunduru hadi Mtwara, ukisikiliza nyimbo za wasanii ni mapenzi tu. Ngoma za wanetu hizi binafsi nimechoshwa sana kwenye ubongo wangu.


Siwezi kulaumu sana hilo. Pengine watanzania ni watu wa mapenzi tu. Ndiyo kitu wanachopendelea kukiona na kukisikia. Maana haiwezekani hata kwenye habari zao za kila siku ni za kuhusu mapenzi mwanzo mwisho.


Inawezekena kikaonekana kama kitu cha kawaida. Lakini niwakumbushe tu kuwa bolingo, taarabu, mnanda na vitu kama hivyo. Ilikuwa juu kinoma noma kama ilivyo Bongo Fleva. Lakini ikafika wakati kila kitu kikatoweka.


Taarabu ya sasa siyo ya wakati ule. Bolingo ya leo siyo ile ya miaka ile. Na hata 'zouk' haipo tena kwenye ramani ya muziki. Kuna haja ya kupambana ili kuwafanya watu wasichoshwe na aina moja ya kelele. Kelele zilizopangiliwa.


Na bahati mbaya zaidi, waandishi wa magazeti, runinga, blogs na redio. Nao wote wakimfanyia mahojiano msanii, lazima wamuulize maswali ya kingono ngono. Huko ndiko tulikofikia. Yaani tumeacha mapenzi yatushikie akili kwetu.


Jaribu kupoteza muda siku mbili hizi. Sikiliza nyimbo mpya za mwaka huu na mwaka jana. Bongo Fleva yote ni mapenzi matupu kwenye nyimbo zao.
Bongo Movie ni mapenzi tupu kwenye filamu zao. Hivi hakuna maisha nje ya mapenzi?


Kinachoshangaza kuna wasanii na wanamuziki wanaoimba mapenzi. Na pia hawana umri wa kushwishi mtu akaelewa. Kwamba huyu kijana kweli anayajua mapenzi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags