'255 Champion Boy' Mbwana Samatta, hakupewa sapoti ya kutosha na wadau. Wachache walisapoti harakati zake kwa upekee. Siyo wadau pekee hata wachezaji na viongozi wao pia hawakutoa sapoti.
Kama utani akatemana na Simba kibabe. Akataka gari waliloahidi kumpa ndipo awachezee Simba. Ikawa kama utani mara paa miezi 6 dogo anakula zake mbilimbi tu Mbagala huko. Kaigomea Simba.
Wakampa gari lake. Wakampa nafasi ya kucheza. Tp Mazembe ile ya moto akaiburuza kama mikia ya farasi. Moise Katumbi 'Tajiri', akasema msinitanie lete hiyo mali hapa. Akasajiliwa.
Ukawa mwanzo na mwisho wa Samatta kuhangaika na viwanja vya Bongo. Uwanja alioendelea kuutumia ni uwanja wa ndege tu. Wakati akija na kuondoka zake. Leo hii ni milionea kweli kweli siyo wa kubahatisha.
Hawakutumia uwepo wa Samatta TP Mazembe kumpeleka Mwinyi Kazimoto. Mwinyi Kazimoto naye hakupatwa na hasira ya kutoka nje ya mipaka kama Samatta. Ni kama Samatta alienda 'pikiniki'.
Thomas Ulimwengu pekee. Ndiyo aliyejenga upacha na Samatta pale TP Mazembe. Naye dakika za mwishoni akamaucha Samatta aende zake. Samatta akaenda zake Ulaya, Ulimwengu akabaki zake Lubumbashi.
Samatta aliendelea na uyatima wa upweke kwenye viwanja vya watu. Wakati airport wenzake wakipeana salama. Ule msimu wa kurudi kuzitumia timu za taifa. Samatta alikuwa yeye kama yeye. Upweke.
Hakuna mchezaji nje ya Samatta aliyekuwa na hasira za kufika au kuelekea kule aliko Samatta. Hata walioendelea wengi waandishi kuliko wachezaji na viongozi wa soka. Samatta akaendelea kuwa yatima wa soka letu.
Wamekuja kina Miroshi baadaye. Samatta akiwa tayari anapaswa akale pensheni zake au akajaze akaunti kule Arabuni. Kimsingi Samatta katubeba muda mrefu kwenye mabega yake bila sapoti.
Sapoti siyo kushangilia akipiga mtu kanzu na tobo. Sapoti ni kuwajaza kina Samatta wengine wengi kule aliko Samatta. Bahati mbaya wapigaji pesa wanaojiita watu wa mpira, ni wengi kuliko mawakala.
Tunapenda kupokea wachezaji wa kigeni utadhani watalii vile. Hawa wanakuja kubeba pesa zetu na kwenda kujenga makwao. Na sisi tupeleke vijana wetu nje wakabebe pesa waje kuijenga Tanzania.

Leave a Reply