Kundi la Wagosi wa Kaya linaloundwa na Dk John na Mkoloni linakumbukwa na wengi kwa nyimbo zao maarufu kama Wauguzi, Tanga Kunani, Kero, Bei Juu, Fat na Soka, Dereva, Trafiki, Walimu na kadhalika.
Wagosi wa Kaya wanasifika kwa mtindo wao mzuri wa kuwasilisha ujumbe wa maana katika njia ya kufurahisha au mzaha kitu ambacho kinawatofautisha na wasanii wengi wa rap ndani ya Bongofleva. Wafahamu zaidi.
1. Kabla ya Mkoloni kukutana na Dk John na kuanzisha kundi walishakutana wakati wakichana kwenye viwanja huko Tanga miaka ya 1995/96, baadaye Mkoloni akaanzisha kundi (Hood Tanga Line) na Danny Msimamo ambalo halikudumu.
Ikumbukwe wimbo uliokuja kumtoa Danny Msimamo kimuziki ni 'Mic' ambao ulipangwa kurekodiwa Bongo Records kwa P-Funk Majani ila ikashindika. Majani alimpa Danny ofa ya kurekodi baada ya kumsikia katika nyimbo za Wagosi wa Kaya ambazo zilikuwa hazijatoa.
2. Waliamua kutumia jina la Wagosi wa Kaya ili kuonyesha wanawakilisha kule wanapotokea, Tanga. Ila awali walianza kwa kujiita 'Wagosi wa Ndima'. Neno 'kaya' kwa Kisambaa lina maana ya 'nyumbani' na neno 'ndima' (jina la awali) lina maana ya kazi, hivyo wakaona ikiwa 'Wakosi wa Kaya' itakuwa na maana zaidi.
3. Dk John ndiye alianza kuandika wimbo wao 'Tanga Kunani' kwa lafudhi ya Kidigo naye Profesa Jay akamshauri kuendelea na mtindo huo kwa kutumia lafundhi hiyo. Wakati huo kundi la Wagosi wa Kaya bado halijaundwa.
4. Baadaye Dk John akakutana na Mkoloni mkoani Tanga baada ya kupotezana kwa takribani miaka miwili. Dk John alipomchania vesi mbili ambazo tayari alikuwa ameandika kwa ajili ya wimbo 'Tanga Kunani' ndipo Mkoloni akapenda na kuomba ashirikishwe.
5. Kipindi wanafanya mazoezi ili kwenda kurekodi wimbo huo ndipo Mkoloni akaja na wazo la kuanzisha kundi, Dk John akakubali na kutoa lile jina la awali 'Wagosi wa Ndima' ila Mkoloni akaliboresha na kuwa 'Wagosi wa Kaya' hadi sasa.
6. Kisha wakaenda ofisi aliyokuwa anafanyia kazi Profesa Jay huko Tanga. Jay akachukua kalamu na karatasi na kuwachorea ramani ya kufika studio kwa Prof Ludingo, Dar es Salaam. Maelezeo yalikuwa mkifika mwambieni Profesa Jay amewatuma.
Huyu Prof Ludingo ndiye alitengeneza midundo yote ya albamu ya kwanza ya Hard Blasters Crew (HBC), Funga Kazi (2000). Kazi hiyo aliifanya akiwa Marekani na alipokuja Bongo ndipo kina Profesa Jay wakarekodi albamu hiyo pale MJ Records.
7. Baada ya kupata ramani ya kuja Dar kwa Prof Ludigo, fedha ya usafiri na kurekodi ikawa hakuna ndipo rafiki yao mmoja, Fred akajitolea kuwalipia tiketi mbili za basi - changamoto ikabaki upande wa fedha ya kurekodi ambayo ilikuwa ni takriban Sh50,000.
Ndipo Dk John akaamua kwenda kuvunja kibubu cha mke wake ili ipatikane fedha ya kurekodi. Katika kibubu akachukua takriban Sh14,300 hivi ili mke asijue kama kuna fedha imechukuliwa. Baadaye rafiki yao Rogers akawaongezea fedha.
8. Kufika Dar asubuhi yake wakaamkia kwa Prof Ludigo na bahati nzuri wakakutana naye getini akiwa na kikombe chake cha chai wakampa maelekezo waliyopewa na Profesa Jay. Akawauliza mnaweza kuchana? Ndipo wakampa mistari ya ngoma 'Tanga Kunani'. Ludigo akakubali muziki.
9. Wakati wanaingia MJ Production wasanii waliowakuta ambao tayari walikuwa wameanza kufanya vizuri walikuwa ni kundi la Gangwe Mobb lililoundwa na Inspector Haroun na Luteni Kalama.
Basi, punde tu wakaingia studio B pale MJ Production kipindi hicho wakarekodi ngoma hiyo. Unaambiwa pale studio kila mtu alikuwa anacheka kutokana na mtindo wao wa rap. Ilikuwa ladha mpya ndani ya Bongofleva.
10. Baada ya Master J kusikia wimbo wa Wagosi wa Kaya, 'Tanga Kunani' uliorekodiwa na Prof Ludigo aliwarudishia fedha yao ya kurekodi na kufungua lebo, ndipo ikaanzishwa MJ Records na wasanii wa kwanza kusainiwa walikuwa Wagosi.
Hivyo Wagosi wa Kaya hawakuhitaji kurekodi nyimbo mbili au tatu ili waweze kutoka kimuziki, bali ni wimbo mmoja tu 'Tanga Kunani' ambao uliwaweka kwenye ramani ya Bongofleva kutokana na utofauti mkubwa.

Leave a Reply