Rais wa FIFA, Gianni Infantino amethibitisha rasmi mabadiliko makubwa ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo, kutakuwa na burudani ya muziki katika kipindi cha mapumziko.
Machi 5, 2025 kupitia ukurasa wa Instagram wa Infantino, alitoa taarifa hiyo iliyosisimua mashabiki wa muziki na mpira akithibitisha kuwepo kwa tukio hilo la kihistora kwenye fainali za kombe la dunia 2026.
“Ninaweza kuthibitisha onyesho la kwanza kabisa la muda wa mapumziko kwenye fainali za kombe la dunia la FIFA, kwa ushirikiano na Global Citizen. Huu utakuwa wakati wa kihistoria kwa Kombe la Dunia na FIFA na onyesho linalolingana na tukio kubwa zaidi la michezo ulimwenguni,” aliandika Infantino.
Tukio hilo linalosubiriwa kwa hamu litafanyika kwenye Uwanja wa 'MetLife' huko New Jersey Julai 19, 2026. Hata hivyo, Onyesho hilo la kihistoria la wakati wa mapumziko litaandaliwa na FIFA kwa kushirikiana na Global Citizen, huku Chris Martin na Phil Harvey kutoka bendi ya Uingereza ya Coldplay ndio wameachiwa jukumu la kuteuwa wasanii watakaotumbuiza siku hiyo.
Kwa kawaida muda wa mapumziko ya mpira wa miguu huwa dakika dakika 15, lakini mpaka sasa FIFA bado haijathibitisha kama wataongeza muda ili kushughulikia burudani hiyo au itabaki kama ilivyo, japo kwa upande wa Half Time Show za Super Bowl hutumia dakika 13 pekee za mapumziko.
Zaidi ya hayo, Infantino alifichua kuwa FIFA itachukua nafasi ya matangazo Times Square kwa wikendi ya mwisho ya Kombe la Dunia la 2026, wakati wa fainali hiyo kubwa.
Mashindano hayo ya Kombe la dunia 2026, yatakayoandaliwa yakijumuisha nchi tatu ambao ni wenyeji Marekani, Canada, na Mexico yatakuwa ya kwanza kuwa na tamasha kama hilo la burudani ndani ya mchezo.
Maendeleo haya katika Half Time za kombe la dunia yanaashiria mabadiliko makubwa kwa Kombe la Dunia, ambalo kihistoria limekuwa likionyesha matukio ya burudani ya muziki kabla ya mechi lakini haijawahi kutokea wakati wa mapumziko ya mchezo wenyewe.
Kombe la dunia la 2026 linaelezwa kuwa ndio shindano litakalo kuwa na mechi nyingi zaidi kuwahi kutokea kwenye historia ya kombe la dunia, ambapo litashuhudia michezo 104 ikichezwa katika miji 16 inayohusisha mataifa 48 mwenyeji wa mashindano hayo akiwa Canada, Mexico na Marekani.
Hatua hii ya FIFA kutumia muda wa mapumziko kutoa burudani ya muziki kwenye fainali za kombe la dunia 2026 limekuja kufuatia Super Bowl Half Time Show ya mwaka 2025 aliyopafomu Kendrick Lamar kuacha alama kubwa kwenye ulimwengu wa burudani huku ikiongeza thamani ya mchezo husika.
Unadhani nani atapanda jukwaani kwenye kipindi cha mapumziko ya fainali za kombe la dunia?

Leave a Reply