Tombwe Njere ambaye ni mama mzazi wa mkali wa Bongo Fleva, Alikiba, ameeleza historia ya jina la nyota huyo. Huku akiweka wazi kuwa jina “Kiba” halikutokea kwa bahati mbaya bali alipewa tangu akiwa tumboni.
“Kwanza jina lenyewe la Kiba lilitolewa na jirani yangu, nilikuwa na kitumbo changu mwenyewe cha Kiba. Jirani yangu anaitwa Mohamed Mawamba alikuwa ni rafiki sana wa mume wangu alikuwa ni kijana mdogo lakini alikuwa akifundishwa kazi na mume wangu.
"Sasa akawa ananifanyia utani mama kibanio mama kibanio, na hilo kibanio lilitokana na meli ilikuja hapo bandarini iliandikwa kibanio. Sasa yeye akawa ananitania mama kibanio. Basi hivyo hivyo siku nimejifungua Ally jina likaamia kwa mtoto akawa anaitwa kibanio na Ally mwenyewe kwenye swaga zake akakata ile kibanio ikabakia Kiba,”amesema mama Kiba
Aidha mbali na hilo ameeleza kuhusiana na nyota huyo kuonesha kitu cha tofauti siku saba baada ya kuzaliwa kwake.
“Alikuwa ndio kwanza ana siku saba, baba yake alimletea tenga. Basi siku hiyo baba yake akamuweka kwenye kile kitenga akawa amelala. Lakini baba yake alikuwa anapenda sana taarabu za Juma Balo alivyoplay tu ile taarabu mtoto akaanza kucheza.
"Sijakariri ule mwimbo ambao alimuwekea lakini ulikuwa wa Juma Balo. Basi mtoto akawa anatingisha kichwa watu tukajazana kushangaa mtoto anacheza, kwa hiyo mtu na chake alipewa tokea akiwa mdogo,”ameongezea mama Kiba
Kwa sasa Alikiba anajifua kutumbuiza katika show ya miaka 20 ya Alikiba ambayo itafanyika Aprili 19, 2025 Kendwa visiwani Zanzibari.

Leave a Reply