Mashabiki Wanasema Nini Kuhusu Dogo Rema

Mashabiki Wanasema Nini Kuhusu Dogo Rema

Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii ametawala msanii mpya, Dogo Rema aliyetambulishwa na muhamasishaji wa mtandaoni Dotto Magari. Ambapo mashabiki wamempokea msanii huyo kwa namna tofauti tofauti.

Wapo ambao wamekubali uwezo wake na kumtia moyo, lakini wapo ambao hawajaridhishwa na uwezo wake wa kuimba na kufanya muziki. Leo Mwananchi Scoop imekusogezea baadhi ya maoni ya mashabiki kutoka mtaani namna wanavyo mzungumzia msanii huyo.

Akizungumza na Mwananchi Scoop, Nadi kutokea mtaa wa Tabata jijini Dar es Salaam amesema Dogo Rema kwenye muziki bado ila mashabiki wanafurahia vituko vyake.

"Dogo Rema kwenye muziki bado na sio kwamba hajui kidogo, yaani hajui kabisa. Cha msingi sisi mashabiki tunaangalia vituko vyake sio kwamba uimbaji hapana. Ni vituko na minguo yake ambayo anatuvalia kwa hiyo tunafurahia kuangalia ile minguo yake ila hatufurahii muziki wake," amesema Nadi.

Amesema mashabiki wamempokea na kumuonesha sapoti kwa sababu amekuja kitofauti hususani ni uvaaji wake wa kipekee ukilinganisha na wasanii wengine.

"Mashabiki wamempokea kwa sababu amekuja na njia ya kitofauti hakuna msanii amewahi kuvaa minguo kama ile maana yake amekuja na mtindo wake wa vituko mimi hata nikikutana naye nashangaa zile nguo sio kuimba kwake," amesema Nadi.

Kwa upande wake Fami Innocent, ambaye ni mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam amesema Dogo Rema anajitahidi na anafanya vizuri kikubwa apambane bila kusikiliza maneno ya mashabiki wanaomponda.
"Dogo Rema anajitahidi na anafanya vizuri, kikubwa aongeze juhudi apambane na asisikilize shabiki anaongea nini. Mwingine anaongea anakuponda kikubwa ni asimamie mambo yake tu.

“Muziki ulivyo unaweza kukuta msanii anaonekana anapuyanga lakini ndiyo anatembea hivyo lakini mimi naona ana kitu. Japo meneja wake Dotto Magari muongeaji sana lakini Dogo Rema tayari ameshakubali matokeo," amesema Fami.

Naye mwanadada Naomi Kane mkazi wa Makumbusho jijini Dar es Salaam amesema Dogo Rema kipaji chake cha muziki ni kidogo lakini anatakiwa apambane bila kukata tamaa kwani wasanii wengi wakubwa walianza kama yeye.

"Dogo Rema kweli kipaji chake ni kidogo lakini anatakiwa apambane wengi wametokea huko huko wamejitafuta mpaka sasa wamekuwa wasanii wakubwa kwa hiyo asikatishwe tamaa na maneno ya watu. Anatakiwa asimamie misingi yake kama anataka kutoka zaidi na afanye muziki wake vizuri Mungu atamjalia na watu watamuelewa,"amesema Naomi Kane.

Amesema namna ambavyo meneja wa msanii huyo, Dotto Magari anavyofanya naye maudhui ya mtandaoni sio kumuaibisha bali anamsaidia ili mashabiki waendelee kumfuatilia zaidi.

"Hapana hamuaibishi pia hiyo ni moja kati ya maudhui na njia yao huwezi jua inamuongezea watazamaji na watu kumfuatilia zaidi kwenye muziki wake na mitandao ya kijamii," amesema Naomi Kane.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags