Peter Akaro
Kwa sasa kiu ya Harmonize, staa wa Bongo Fleva kutokea Konde Music Worldwide, ni kushinda tuzo kubwa zaidi za muziki duniani, Grammy. Ni ndoto ambayo ameizungumza kwa muda mrefu na hata hivi karibuni alipotangaza kukamilika kwa albamu yake mpya, kairejea tena.
Harmonize anaamini albamu yake ijayo ambayo itakuwa ya sita kutoka kwake, ina vigezo vyote vya kuiwezesha kuchaguliwa kuwania tuzo hizo na hata kushinda kutokana maandalizi yake yamefanyika ipasavyo.
Kauli ya Harmonize ilikuja siku moja baada ya meneja wake wa kimataifa, George Beke kuidhinishwa kuwa mwanachana wa Recording Academy, hivyo sasa ataweza kuwasilisha kazi za wasanii kuwania Grammy na hata kupiga kura.
"Kupitia uanachama huu mpya, Beke sasa ana mamlaka ya kuwasilisha muziki kwa ajili ya kuzingatiwa kwenye tuzo za Grammy, kupiga kura kwenye tuzo hizo, na kutetea masilahi ya wabunifu barani Afrika na duniani kote."
"Hii siyo tu hatua ya mafanikio binafsi, bali ni ushindi kwa muziki wa Afrika na hatua kubwa ya kusonga mbele kwa utamaduni wetu. Tunaadhimisha tukio hili kama mafanikio makubwa kwa Konde Music Worldwide na harakati nzima ya ubunifu tunayoisimamia," sehemu ya taarifa ya Konde Music ilieleza.
Wanachana wa Recording Academy, ni kundi la watu wenye uelewa mkubwa wa muziki wakiwemo wasanii, watunzi wa nyimbo, watayarishaji na wahandisi ambao hupita mchakato maalamu kabla ya kupata nafasi hiyo muhimu ya maamuzi.
Ikumbukwe tuzo za Grammy zilianza kutolewa hapo Mei 4, 1959, wakati huo zikifahamika kama Gramophone Awards, huku lengo lake kuu likiwa ni kutambua mafanikio katika tasnia ya muziki duniani.
Hadi sasa, Beyonce Knowles, mwanachama wa zamani wa kundi la Destiny's Child, ndiye mwanamuziki aliyeshinda tuzo nyingi zaidi za Grammy duniani kwa muda wote, akishinda mara 35.
Mzaliwa huyo wa Houston, katika Grammy 2025 ukiwa ni msimu wa 67, alishinda kipengele cha Albamu Bora kwa mara ya kwanza baada ya kuwania mara nne bila mafananikio. Ushindi huo uliletwa na albamu yake ya nane, Cowboy Carter (2024) wenye nyimbo 27 huku akishirikisha wakongwe kama Dolly Parton, Willie Nelson na Linda Martell.
Harmonize anaamini kama sio albamu, basi moja ya nyimbo kutoka katika albamu hiyo itamfanya kuingia katika orodha ya wasanii wachache kutoka Afrika walioshinda Grammy.
Tayari ameachia kionjo cha wimbo mmoja kutoka katika albamu hiyo, Lala (2025) akishirikiana na Abigail Chams ukiwa ni wimbo wao wa nne baada hapo awali kutoa; Closer (2022), Leave Me Alone (2022) na Me Too (2025).
Utakumbuka Harmonize tangu ametoka kimuziki kupitia wimbo wake, Aiyola (2015) chini ya WCB Wasafi, tayari ametoa albamu tano, Afro East (2020), High School (2021), Made For Us (2022), Visit Bongo (2023) na Muziki wa Samia (2024).
Harmonize anajaribu bahati yake Grammy 2026 kupitia albamu ya sita ambayo ipo mbioni kutoka. Hajachelewa kwani Burna Boy kutokea Nigeria alishinda Grammy yake ya kwanza na ya pekee hadi sasa kupitia albamu yake ya tano, Twice as Tall (2020).
Kabla ya hapo alikuwa ameshatoa albamu kama L.I.F.E (2013), On a Spaceship (2015), Outside (2018) na African Giant (2019), kisha hiyo, Twice as Tall (2020), na baadaye, Love, Damini (2022), I Told Them... (2023) na No Sign of Weakness (2025).
Angelique Kidjo kutokea Benin ambaye ndiye mwanamuziki Afrika aliyeshinda Grammy nyingi zaidi, naye alisubiri kwa muda mrefu sana kwani Grammy ya kwanza aliipata kupitia albamu yake ya nane, Djin Djin (2007) iliyoshinda kama Albamu Bora ya Muziki Duniani.
Baadaye akaja kushinda tuzo nyingine nne katika kipengele hicho kupitia albamu zake nne tofauti ambazo ni Eve (2014), Angelique Kidjo Sings with the Orchestre Philharmonique Du Luxembourg (2015), Celia (2019) na Mother Nature (2021).
Hadi sasa wasanii wa Afrika walioshinda Grammy kupitia kazi zao wenyewe ni Miriam Makeba (Afrika Kusini) 1966, Sade Adu (Nigeria) 1986, Ali Farka Toure (Mali) 1994, Cesaria Evora (Cape Verde) 2004, Youssou N'Dour (Senegal) 2005.
Wengine ni Angelique Kidjo (Benin), RedOne (Morocco) 2010, Tinariwen (Mali) 2012, Burna Boy (Nigeria) 2021, Black Coffee (Afrika Kusini) 2022, Tyla (Afrika Kusini) 2024 na Tems (Nigeria) 2025.
Ni wazi kiu ya Harmonize kushinda Grammy imeongezeka baada ya kuanzisha kipengele kwa ajili ya muziki na wasanii wa Afrika pekee (Best African Music Perfomance) ambacho hadi sasa kimetoa washindi wawili, Tyla 2024 na Tems 2025.
Ikiwa Harmonize atashinda Grammy 2026 kupitia kipengele hicho, ataweka rekodi kama mwamuziki wa kwanza wa kiume Afrika kufanya hivyo. Albamu yake ya sita ndio itakayoamua hilo. Je, atafanikiwa kama anavyojitapa mtandaoni?, muda ndio utakaotupa jibu sahihi.
Leave a Reply