Peter Akaro
Kinachosubiriwa kutoka kwa watu hawa maarufu kutoka kiwanda cha burudani Bongo ni ndoa baada ya kuingia hatua ya uchumba kwa kuvishana pete.
Hivyo basi, kwa maana nzuri tunaweza kufananisha na wale wanaobeti, muda wowote mkeka unaweza kuchanika lakini hawa wafuatao tayari mkeka wao wa kwanza umetiki. Karibu.
1. Vanessa Mdee
Mwimbaji huyu ambaye kwa sasa ni mama wa watoto wawili, Desemba 2020 ndipo alivishwa pete na mpenzi wake Rotimi ambaye ni msanii wa filamu na muziki mwenye asili ya Nigeria.
Wawili hawa kwa sasa wanaishi wote nchini Marekani, mtindo wa maisha yao umekuwa maarufu mtandao na kuvutia vijana wengi, ndoa yao inatazamiwa kuwa tukio litakalovuta hisia za wengi kutokana na nguvu ya ushawishi walionayo. Hivyo basi inasubiriwa kwa hamu
2. Darassa
Rapa huyu toka Classic Music Group (CMG), Agosti 2021 naye alipiga goti na kuweka pete kwenye kidole cha mpenzi wake wa siku nyingi ambaye tayari ni mzazi mwenziye kwa sasa.
Tukio hilo lilifanyika wakati Darassa akifanya mazoezi na band yake pamoja na msanii Marioo, huku kukiwa na watu wake wengine wa karibu kama Prodyuza Abbah ambaye ametengeneza ngoma zake nyingi.
3. Stamina
Hapo Agosti 2021 Stamina toka kundi la Rostam alimvisha pete mrembo ambaye tayari wamejaliwa mtoto mmoja, licha ya kuweka hilo wazi Rapa huyu sasa amekuwa na mtindo wa kufanya siri zaidi maisha yake ya mahusiano.
Awali Stamina alikuwa ameshaoa lakini ndoa yake hakudumu hata mwaka mmoja ikawa imevunjika, ni jambo alilolieleza kwa machungu mengi katika wimbo wake 'Asiwaze ' uliotoka Januari 9, 2020 na kuwa gumzo kubwa kutokana na maudhui yake.
4. Dogo Janja
Mara baada ya Dogo Janja kuachana na aliyekuwa mke wake, Irene Uwoya ambaye walifunga ndoa Novemba 2017, aliamua kubadili mapishi kwa kutafuta mrembo mwingine toka nje ya tasnia ya burudani Bongo.
Hapo Februari 2020 Janjaro alimvisha petempenzi wake, Queen Linah ambaye ni Mjasiriamali wakiwa wanakula bata visiwani Zanzibar mbele ya marafiki kadhaa waliokuwa nao ndani ya boti, naye bado mashabiki wanasubiri ndoa yake.
5. Shilole
Msanii na mfanyabiashara maarufu, Zuwena Mohammed 'Shilole', alivishwa pete ya uchumba na mpenzi wake mpya Desemba 23,2024.
Tukio hilo lilitokea katika sherehekea ya kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa. Iwapo Shilole ataolewa hii itakuwa ndoa yake ya tatu, baada ya ndoa zake mbili za awali kuvunjika. Ndoa yake ya pili ilivunjika rasmi Juni 2024.

Leave a Reply