Mwanaume mmoja kutoka Afrika Kusini ambaye hajawekwa wazi jina lake ameripotiwa kuwasilisha kesi ya talaka mahakamani baada ya mke wake kupiga picha yenye utata na mkali wa R&B kutoka Marekani Chris Brown.
Kulingana na nyaraka zilizowasilishwa katika mahakama iliyopo jijini Durban, Mume huyo amedai kuwa picha hiyo iliyoonesha Brown akimbusu mkewe shavuni imeleta migogoro mikubwa isiyorekebishika katika ndoa yake.
Aidha mwanaume huyo aliweka wazi kuwa mkewe amemuonesha dharau na kumdhalilisha yeye na familia yake kwani sio sahihi kwa mwanamke aliyeolewa kupiga picha ya aina hiyo.
Picha hiyo, iliyozua migogoro mikubwa katika familia hiyo ilipigwa baada ya tamasha la hivi karibuni la Brown lililofanyika katika Uwanja wa FNB nchini Afrika Kusini.
Mke huyo alihudhuria katika tamasha hilo la Brown lililoshika vichwa vya habari duniani kote lililofanyika wiki mbili zilizopita ambapo mwanamke huyo alilipia tiketi ya VIP iliyojumuisha kupiga picha na msanii huyo bure liitwalo ‘Meet and Greet’.
Leave a Reply