MX Carter awataka Billnass, Gara B kumlipa fidia ya mamilioni kwa madai ya kumchafua

MX Carter awataka Billnass, Gara B kumlipa fidia ya mamilioni kwa madai ya kumchafua

Mwanasheria wa msambazaji wa kazi za wasanii Kidigitali, Michael Mlingwa 'MX Carter', Hassan Yaseen, amefafanua sababu ya mteja wake kuwafungulia mashitaka na kutaka kulipwa fidia kutoka kwa msanii wa Bongo Fleva, Billnass na mshereheshaji Mc Garab.

Utakumbuka, hivi karibuni Billnass aliandika ujumbe wa madai kuhusu namna ambavyo msimamizi wa kazi za wasanii Kidigitali, 'MX Carter' amekuwa akifanya vitendo vya dhuluma kwake na kwa wasanii kupitia kampuni yake ya Slide Visual, kitu ambacho kiliwaibua wasanii wengine kama Baraka Da Prince, Dayna Nyange na mdau wa sanaa Mc Garab.

Akizungumza na Mwananchi, mwanasheria huyo amesema mteja wake amewafungulia mashitaka Billnass na Mc Garab kwasababu wamemchafulia jina lake na la biashara yake.

"Mteja wangu amewawajibisha hawa jamaa kwa kumchafulia jina lake pamoja na biashara anayoifanya kwakuwa biashara anayoifanya ni usambazaji wa muziki kupitia majukwaa na watu wana mikataba na wanalipwa kutokana na kile wanachokipata kwenye hayo majukwaa, walipaswa wafuate taratibu sahihi za kudai hizo fedha.

"Sisi tumejiridhisha na tumeona kabisa, hususani Billnass na Mc Garab wamemchafua kwenye mitandao, mfano Billnass amezungumzia dhuluma kuhusu MX Carter ilihali anajua hawana mkataba lakini yeye ana mkataba na Slide Digital kwaajili ya kufanya kazi na masuala ya malipo yanafanyika kwa utaratibu, kwa kuomba ripoti zake na ameshatafutwa afuate pesa zake," amesema Yaseen na kuongeza.

"Nadhani wasanii wanaamini wanahitaji kulipwa pesa zaidi ya kile ambacho wanakiona, lakini hawana elimu ya biashara ya usambazaji wa muziki, ukimuuliza msanii mtu mmoja akisikiliza wimbo wake Spotify anapaswa aingize shilingi ngapi na hela inakatwaje, hajui, lakini akishaona namba zimefika milioni mbili au tatu anajua lazima alipwe kiasi kikubwa kutokana na kile anachokiona kwenye mitandao bila kujua hesabu ipoje, wanaingia mikataba hawatafuti ushauri wa kibiashara, hawatafuti ushauri wa wanasheria, ikifikia hatua wana shida ya kufanya kazi wanamfuata msambazaji wanaazima pesa nyimbo zikitoka, wakikatwa wanaona kama wanaonewa."

Hata hivyo, amesema hilo sio tukio la kwanza la madai kwa mteja wake, MX Carter kwani hivi karibuni kuna msanii alimshitaki kwa madai ya kutumia kazi zake za muziki vibaya.

"Alikuwa akidai fidia kuhusu kazi zake kutumika vibaya, alikuwa akidai kama Sh700 milioni, nashukuru Mungu tumeshinda, kwa kuwa bado ana haki ya kukata rufaa akikata tusubiri tuone, lakini kimsingi ni kwamba wasanii wanatakiwa waamke na wajue namna ya kufanya kazi hizi kwa weledi," amesema Yaseen.

Katika mashitaka hayo, Mx Carter amewataka wawili hao kumlipa fidia kwa kumchafulia jina, akimtaka Billnass amlipe dola 60,000 (takribani Sh157 milioni za Kitanzania) huku Garab akitakiwa kulipa dola 20,000 (takribani Sh522 milioni za Kitanzania).

Kwa upande wake Mc Garab, amekiri kupokea taarifa ya mashitaka hayo, huku akifafanua kwamba alichozungumza ni kitu ambacho amekipitia na hajazungumza peke yake.

"Nikweli nimepata, kwasababu mimi nina akili zangu timamu, na nimesema vile bahati mbaya au nzuri sio mmoja ambaye amezungumza, kila mtu amezungumza ambavyo ameguswa, kwa hiyo mwisho wa siku ameenda kwenye masuala ya kisheria nafikiri haki itapatikana," amesema Garab.

Ameongezea kuwa, malalamiko hayo yana muhusu MX Carter moja kwa moja kwa sababu yeye ndiye mkurugenzi wa kampuni ya usambazaji wa kazi Kidigitali ya Slide Visual.

"Sawa lakini digital si ya Mx Carter? Kwa hiyo mwisho wa siku sisi tulikuwa tunaongea na mkurugenzi wa kampuni na yeye ndiye alikuwa anatakiwa kutoa msaada, hawezi kujitenga kwenye hilo," amesema Garab.

Amesema aliwahi kupitia changamoto za kutopokea mapato ya kidigitali kwa msanii wake aliyekuwa anamsimamia ambapo kazi zake zilikuwa zikisambazwa kwenye majukwaa ya digitali na kampuni hiyo ya Slide Visual.

"Bahati mbaya mimi nina vitu vingi, hata wakati ninamsimamia msanii kuna mtu nilimuweka awe anafuatilia mambo ya haki zake kwa sababu muda nilikuwa nakosa, nilikutana na Mx nikafanya naye mazungumzo nikamkabibidhi kwa msanii lakini yule mtu aliyekuwa anafuatilia hakuwa anapewa ushirikiano, mimi nikipiga simu kwa Mx tunazungumza kishikaji lakini hamna kinachotendeka, mimi nilipata nafasi ya kuzungumza kama wengine walivyozungumza.

"Msanii ana ngoma inaitwa Dunia na Saa, zote tulipeleka pale kwa msambazaji wa kidigitali na ukiangalia japo sio msanii mkubwa lakini kuna vinamba alikuwa anapata, sasa kwenye namba ndogo kama zimeingiza hata laki mbili tungeiona, lakini hakuna," amesema Garab.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Masoud Kofii


Latest Post

Latest Tags