Peter Akaro
Akiwa na rafiki yake wakitazama runinga katika chumba cha hoteli, David Beckham (50), alimuona Victoria (51), katika video ya wimbo wa kundi lake la Spice Girls, muda huo huo alivutiwa naye na kusema anataka kumuoa mrembo huyo.
Wawili hao kwa mara ya kwanza walikutana mwaka 1997 kipindi Beckham akicheza Manchester United, Victoria alienda uwanjani kutazama mechi na kutano lao la ya pili alifika hadi katika vyumba vya kupumzikia wachezaji na walizungumza kwa saa moja.
Mwaka uliofuatia wakachumbiana na kufikia Machi 4, 1999 wakapata mtoto wao kwanza Brooklyn ambaye sasa ameoa, kisha wakafuata wengine wawili wa kiume, Romeo (2002) na Cruz (2005), na mmoja wa kike, Harper (2011).
Julai 4, 1999 ndipo Beckham, mchezaji wa zamani wa Real Madrid alifunga ndoa na Victoria ambaye ni mwanamitindo na mwimbaji wa zamani wa Spice Girls kutoka Uingereza waliotamba na wimbo wao, Wannabe (1996).
"Beckham ni muungwana sana, ndiye mume mzuri zaidi kwangu na baba mwenye msukumo wa kweli kwetu sote. Yeye ni mchapakazi, nina bahati kuwa naye kama mwenzi wangu kimwili na kiroho," Victoria aliiambia The View hapo Oktoba 2019.
Hata hivyo, ndoa yao ilitabiriwa na wengi kutofika mbali kwa kile kilichodaiwa walioana kwa vile wote ni maarufu, hivyo chapa zao zingewasaidia katika biashara zao ila sasa ni miongo miwili wapo pamoja wakiwazodoa walimwengu waliosema hivyo.
Je, ni kwa namna gani wanawazodoa walimwengu?, Juni 2015 kulikuwa na tetesi kuwa wawili hao walikuwa na shida katika ndoa yao ingawa Victoria wakati akiongea na Grazia, jarida la kila wiki la wanawake alisema ni uvumi tu usiokuwa na maana.
"Mimi na Beckham hatuna chochote cha kudhibitisha, kila mmoja anampenda na kumjali mwenzake na tuna nguvu kama wenzi na wazazi wa watoto wanne," alisema.
"Mume wangu mara kwa mara hunitia moyo na kuniongoza. Amefanya kazi nzuri sana kwangu, ninamtazama kwa heshima na pongezi kwa yote ambayo amefanikisha."
Wakati akipokea tuzo ya Glamour kama Mwanamke Bora wa Mwaka 2015, Victoria alieleza jinsi mumewe amekuwa na mchango mkubwa katika safari yake ya mafanikio kama mama, mwanamitindo, mshawishi wa chapa na mfanyabiashara.
"Kuendesha biashara na kazi yangu wakati huo nikiwa kama mama, haingewezekana bila Beckham. Sio tu kwamba yeye ndiye baba mzuri zaidi, lakini ananiunga mkono na ni mtu ambaye ananipenda na kunitia moyo kila siku," alisema Victoria.
Lakini kitendo cha Victoria kufuta tattoo ya Beckham aliyochora katika mkono wake, kiliibua maneno kuwa wawili hao hawaelewani ila akiongea na Hoda Kotb katika kipindi cha Today hapo Oktoba 2022 alitaja sababu ya kufanya hivyo.
Victoria aliyetambulika kama Posh ndani ya Spice Girls, alisema aliamua kuondoa tatoo zake kadhaa za zamani kwa sababu zilikuwa zimefifia na kubadilika rangi kutoka nyeusi hadi bluu hivyo akawa hana budi kuzifuta.
"Nafikiri kwamba vyombo vya habari vilianza kubahatisha kuhusu ukweli wa hili kwa kuhisi kama nimemuacha mume wangu. Hapana, nilichoshwa tu na tattoo hiyo, hakuna kingine zaidi ya hicho," alisema Victoria.
Akizungumza na BBC Radio hapo Januari 2017, Beckham alifichua kwamba yeye na mkewe walirudia viapo vyao vya ndoa, hiyo ni baada ya kutuhumiwa kuwa na uhusiano na msaidizi wake Rebecca Loos mwaka 2003.
Hata hivyo, ndoa hiyo ya pili ilikuwa ya faragha zaidi, ni watu kama sita tu kutoka katika familia yao walioshuhudia tukio hilo na haikuwa na sherehe kama ile ya kwanza mwaka 1999.
Katika mahojiano hayo, pia David alikanusha madai ya miaka mingi kuwa ndoa yao ipo kwa misingi ya kibiashara na sio familia, alisema wapo pamoja kwa sababu ya upendo na sio chapa zao kama inavyodaiwa.
"Tunafahamiana vizuri kuliko mtu yeyote, watu wamezungumza na kuhoji kama tupo pamoja kwa sababu ni chapa?, bila shaka sivyo. Tunaishi pamoja kwa sababu tunapendana, kwa sababu tuna watoto wa kupendeza," David aliiambia BBC.
Ila walimwengu hawakuishia hapo, Juni 2018 ulizuka uvumi kuwa ndoa yao imekalia kuti kavu na wapo mbioni kupeana talaka lakini mwakilishi wao akiongea na tovuti ya People alisema jambo hilo halina ukweli wowote.
Mwezi uliofuatia Victoria aliliambia jarida la Vogue Uingereza kuwa uvumi kama huo umekuwepo kwa miaka 20 ya uhusiano wao kiasi kwamba wameshazoea na kuona ni kitu cha kawaida hivyo hawana budi kusonga mbele.
"Watu wamekuwa wakitengeneza mambo kuhusu uhusiano wetu kwa miaka 20, hivyo Beckham na mimi tumezoea kupuuza upuuzi wao na kuendelea na mambo yetu ila mambo haya yamekuwa na athari kubwa kwa watu wanaotuzunguka, kwa hiyo sio haki," alisema.
Beckham katika mahojiano na Lisa Wilkinson katika kipindi cha The Sunday Project kilichoruka Oktoba 2018, alifichua siri ya ndoa yao kudumu kwa muda mrefu na kusema ni matokeo ya jitihada za pande zote mbili.
"Kuwa kwenye ndoa kwa muda tulionao, unajua ni kazi ngumu na kila mtu anajua hilo lakini unailazimisha ifanye kazi. Unakuwa na mpango kama kusafiri kwenda mbali au kila mmoja kuwa mbali na mwenzake kwa kipindi fulani, hiyo inasaidia," alisema.
Victoria alipofikisha umri wa miaka 50 hapo Aprili 20, 2024, Beckham alimwandalia tafrija fupi huko London na kuwaalika marafiki wake wote wa karibu, wakiwemo Eva Longoria, Salma Hayek-Pinault na Spice Girls.
"Bado siamini jinsi ulivyonifanya nijisikie wa pekee jioni hii, siku yangu ya kuzaliwa, wiki hii nzima na miaka yetu yote ya miujizi tukiwa pamoja!, Asante, nakupenda sana!," aliandika Victoria Instagram akimshuruku Beckham kwa tafrija hiyo.
Ikumbukwe Julai 2007 Beckham aliposaini mkataba wa kuichezea L.A. Galaxy, yeye na familia yake walihamia Marekani ambapo waliishi katika jumba la kifahari lenye thamani ya Dola22 milioni huko Beverly Hills, California hadi 2013 waliporejea kwao London.
Leave a Reply