Sababu Iliyopelekea Frida Amani Kuacha Kuwa Rapa Wa Kawaida

Sababu Iliyopelekea Frida Amani Kuacha Kuwa Rapa Wa Kawaida

Mwanamuziki wa Hip Hop nchini Frida Amani ameeleza njia anazozifanya ili kuwa bora katika muziki huo kila siku akitaja kuwa ni kujifunza, kufanya kazi kila siku pamoja na kuwekeza zaidi katika yeye.

Akizungumza wakati akiwa kwenye tamasha la Hip Hop Asili amefunguka moja ya changamoto anayokutana nayo katika muziki huo huku akiweka wazi kudharauliwa na baadhi ya watu wakidai kuwa hafai kwenye hip hop.

“Kwa hiyo, jambo la kwanza nililolazimika kujifunza haraka sana ni kwamba lazima nijifunze kila siku. Nilihitaji kuelewa. Wakati mwingine najiona mjinga sana (samahani kwa lugha kali), lakini hilo halijalishi kwa sababu kuna watu wengi pia ambao ni wazuri sana.

Mimi ni binti, na hili linauma sana, kitu cha kwanza ambacho hukutana nacho kila siku ni watu kukuambia, ‘huwezi’ Kila nikisema kuwa nipo kwenye muziki wa HipHop, watu wanaona ni kwamba ‘hufai’. Kwa hiyo inanilazimu kufanya zaidi ili watu waelewe kuwa naweza kufanya haya,”amesema Frida

Aidha ameongezea kwa kueleza “Lakini kwa wanaume, hiyo ni moja ya baraka mliyonayo unaweza tu kuonekana kwa muonekano fulani na watu wakasema, huyu ni msanii wa HipHop,”

Mbali na hilo ameeleza changamoto nyingine kubwa ambayo ipo katika sekta ya muziki wa Hip Hop akitaja kuwa ni watu kudai kuwa muziki huo hauuzi.

“Unaweza kufanya makubwa, lakini bado utakuta mtu mahali anasema, ‘HipHop haiuzi’. Hapo ndipo nguvu yangu ya kibiashara hupungua hasa ninapokutana na mtu mpya kwa sababu kitu cha kwanza anachofikiria ni, tutauzaje kitu ambacho hakitauzika?.

Hili ni jambo ambalo nimekuwa nikijitahidi kulikabili kwa muda mrefu, na hata sasa bado nalikabili, lakini kwa sababu najifunza kila siku na kuwaelewa watu, nimeanza kuunda kitu kipya chenye umuhimu kwetu sote,”amesema

Aidha licha ya kujifunza msanii huyo ameeleza kuwa jambo jingine analolifanya ili kuendelea kumuweka kwenye mstari ni kutamka kuwa Hip Hop ipo ndani yake na kutafuta namna ya kuifanya iwe bora.

SABABU ILIYOPELEKEA KUACHA KUWA RAPA WA KAWAIDA

“Tangu siku nilipoanza kuambiwa, hiki kitu hakiwezekani, hakiuzi, na hakitakupeleka kokote, ndiyo siku ambayo imenipeleka sehemu kubwa sana maishani. Kitu kingine nilichojifunza ni kwamba, pale njia moja inapofungwa, nilihitaji kutafuta njia nyingine.

Ndipo nilipoamua kuacha kuwa rapa wa kawaida tu nikaongeza thamani yangu. Ukiwa unakutana nami, unakutana na mtu mwenye ubora mwingine, mtu anayejifunza kila siku, anayefanya mambo, ambaye hajawahi kukata tamaa, mtu ambaye amewekeza kwenye kazi yake kwa kiwango kikubwa sana, mimi binafsi niliamua kuwekeza kwenye uweledi (professionalism) na hicho ndio kinanitofautisha na wengine,”amesema Frida

Akizungumza kuhusu uwekezaji ameeleza kuwa mbali na uwekezaji wa msanii binafsi lakini pia kuna umuhimu wa kuwekeza kwa watu wengine.

“Jambo jingine ni kuwekeza kwenye wewe mwenyewe, lakini pia kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza kwa watu wengine walio katika nafasi mbalimbali. Uwekezaji huu ni mkubwa unaenda kwa vyombo vya habari, wasanii wenzako, na hata madansa, kwa kifupi, hayo ndiyo mambo ambayo nimekuwa nikiyafanya na yamenisaidia sana.

Baada ya kuwekeza kwenye hayo yote, nimeongeza jambo moja la ziada kwamba kila mwaka natengeneza kitu kipya. Kwa mfano, mwaka jana ulikuwa unaniona nafanya rap peke yangu, basi mwaka unaofuata utaniona nafanya rap na DJ. Mwaka mwingine nitakuwa nimewekeza kwenye bendi. Mwaka unaofuata, utaniona nimeunganisha na vitu vingine,”amemalizia






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags