Simulizi:  Sehemu ya pili Kwa Udi na Uvumba

Simulizi: Sehemu ya pili Kwa Udi na Uvumba

Na Innocent Ndayanse

SIKU Panja alipotoka gerezani, fikra zake zote zilikuwa juu ya Kipanga. Hakuchukua zaidi ya nusu saa nyumbani, Kinondoni ‘A’ jirani na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Usharika wa Kinondoni kabla hajarudi kituoni ambako alipanda daladala lililompeleka Kariakoo kwa Kipanga. Na alimkuta.

“Ni siku njema sana,” Kipanga alisema. Ni muda mfupi tu uliopita alikuwa akivuta bangi huku akijihisi yu huru kuliko alivyokuwa akibahatika kuvuta kwa siri wakati alipokuwa gerezani.

Papohapo akamkabidhi Panja msokoto wa bangi kutoka kabatini. Panja hakuwa mvutaji mkongwe wa bangi, tabia hii aliianza wakati yuko kifungoni.

“Vuta upate akili, tuzungumze kiutu-uzima,” Kipanga alimwambia.

Dakika chache baadaye bangi ilizimwa. Wakatazamana.

“Vipi, una pesa?” Kipanga alirusha swali.

“Pesa!” Panja alimtazama kwa mshangao wa mbali. “Una maana gani?”

“N’na maana una pesa za kuitwa PESA? Au una vijisenti vya nauli ya daladala? Kama una kilo nne, tano hivi, naweza kusema ni pesa za kutambia hata kwa wanaume wenzako.”

Kilo nne, tano zilizotajwa na Kipanga ni usemi uliomaanisha shilingi laki tano. Panja alimwelewa na papohapo akamjibu, “Sina. Nina pesa kidogo sana.”

Kiasi gani?”

“Ni aibu. Hazifiki hata alfu kumi.”

Kipanga aliguna kidogo kisha akamponda kwa kusema, “Kwa kifupi sema huna pesa. Alfu kumi hata ishirini si’o pesa za kutosha hata kwa kuhonga demu.” 

Panja alikosa hoja, akaishia kutabasamu, tabasamu ambalo halikutoa taswira yoyote kama ni la furaha au huzuni.

Kipanga akaendelea, “Muda huu ni saa saba. Saba na robo. Najua una uchovu kidogo. Lakini we’ ni mwanamume, haupaswi kulemaa. Kuna kazi. Kazi ya pesa, na inabidi ifanyike leo. Uko tayari?”

“Hata sasa hivi, mwanangu.”

“Poa,” Kipanga alisema. Akaongeza. “Ni vizuri tusilaze kazi. Wewe una vijipesa kidogo, mie nina shombo ya sarafu. Lakini kwa sasa nenda nyumbani, kapumzike, urudi hapa saa mbili usiku. Unahitaji muda kidogo wa kupumzika kabla ya kupumzika kwa starehe huku kitu kama milioni tatu au  nne hivi zikiwa kibindoni.”

“Dili lenyewe linafanyikia wapi?” Panja alihoji kabla ya kunyanyuka.

“Tutaongea ukisharudi. Lakini ni hapahapa town.”

SAA saba usiku, Panja na Kipanga walikuwa wakitoka ndani ya chumba maalum katika nyumba ya Kipanga. Mkakati ambao Kipanga alimpa Panja tangu walipokutana saa tatu na dakika kadhaa, ulimpa ujasiri mkubwa Panja. Wakatembea wakikata mtaa huu na ule, kwa hadhari na kwa kujiamini, bangi waliyovuta usiku huo ikawaongezea hali ya kujiamini.

Walipofika Mtaa wa Libya, Kipanga akamnong’oneza Panja: “Subiri kidogo.”

Panja alisimama kando ya barabara, akamwona Kipanga akilifuata jengo moja ambako alinong’ona na mlinzi mmoja kwa takriban dakika mbili kisha akarudi. “Una silaha yoyote?”

“Sina,” Panja alijibu haraka.

“Shika hii,” alikabidhiwa kisu kisha ikafuata amri nyingine,

“Nifuate.”

Wakatoka, hatua zao zikiwa za asteaste, Kipanga akiwa na bastola mkononi, Panja akiwa na kisu. Wakafunguliwa geti na  yule mlinzi na kuingia ndani, Kipanga mbele, Panja nyuma.

Dakika kumi baadaye, milipuko miwili ilisikika. Panja na Kipanga walikuwa kazini, na walipotoka humo ndani waliiacha maiti ya mzee wa Kihindi ikivuja damu shingoni.

Nje ya geti, Kipanga aliyekuwa na fuko kubwa la nailoni lililojaa noti alimnong’oneza yule mlinzi: “Uje home asubuhi.”

NYOTA ya jaha ilikuwa imemshukia Panja. Tangu azaliwe na kufikia umri wa kuweza kutambua thamani ya pesa, hakuwa na kumbukumbu ni lini aliwahi kumiliki shilingi laki moja. Usiku huu baada ya mgawo alijikuta akimiliki milioni tatu na robo.

Zilikuwa ni pesa nyingi kwake kiasi cha kujiona yu tajiri mdogo wa Dar, na kwamba ni pesa ambazo kamwe zisingekwisha. Kwa mantiki hiyo, starehe alizipa kipaumbele katika ratiba zake za kila siku. Leo aliingia baa hii, kesho baa ile na keshokutwa, ile. Kote huko hakukosa kuondoka na mwanamke mwenye mvuto mkali.

Hakuhitaji kutongoza, pesa zilizungumza. Na hakuwa na mkataba na mwanamke yeyote; leo akimchukua Zainabu, kesho atambeba Zinduna. Alichojali ni uwezo wa anayechukuliwa; uwezo wa faraghani.

Ni katika bebabeba hiyo ndipo alipokumbana na Hilda, lakini huyu hawakukutana baa bali katika kituo cha daladala, Posta Mpya katikati ya Jiji la Dar es Salaam, wote wakisubiri usafiri wa Kinondoni 

Kwa kumtazama harakaharaka, Panja alivutiwa na umbo la Hilda. Ndiyo, Hilda alikuwa ni mzuri kiasi cha kumlinganisha na Sofia, mwanamke aliyeishi mtaa mmoja na Panja na akawa ni mwanamke ambaye, kichwani mwa Panja alipewa nafasi ya kwanza kwa uzuri wa sura na umbo.

Naam, Panja alihisi kamwona pacha wa Sofia. Akajaribu kuzikumbuka siku mbili ambazo walijichimbia gesti wakifanya hivi na vile katika kuzikonga nyoyo zao. Siku ya kwanza Sofia alionekana kalewa sana hali iliyomfanya Panja ajenge hisia kuwa huenda ndiyo maana hakujishughulisha inavyostahili katika starehe iliyowakutanisha. Akamsamehe.

Siku ya pili, wote hawakulewa, walikunywa bia mbilimbili tu baada ya kuyajaza matumbo yao chakula kizito. Kisha wakachukuana tena hadi gesti. Ni siku hiyo ndipo Panja alimjua vizuri Sofia, kwamba pamoja na dosari nyingine, pia alikuwa  mbumbumbu wa kutupwa katika fani hiyo. Asubuhi ya siku ya tatu alimtema kama kapi la muwa.

Lakini, pamoja na hayo, Panja hakutaka azihamishie kasoro za Sofia kwa mwanamke huyu mrembo maradufu. Hapana. Aliamini kuwa kufanana sura na umbile si kufanana nguvu na maarifa katika kila nyanja. Ni hilo lililomfanya ajikute anapanda daladala ambalo Hilda alipanda japo kwa wakati huo hakujua Hilda alikuwa akielekea wapi.

Itaendelea…………..

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post