Sio Mchezo! Afande Sele Na Mahari Ya Sh5 Milioni, Ng’ombe

Sio Mchezo! Afande Sele Na Mahari Ya Sh5 Milioni, Ng’ombe

Rhobi Chacha

Safari ya kukamilisha ndoto ya Mfalme wa Rhymes, rapa mkongwe, Seleman Msindi 'Afande Sele' ilianza wiki iliyopita Agosti 5, baada ya tukio la kipekee la kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake wa muda mrefu Iman Makongoro.

Afande Sele amedhamiria kutimiza ndoto yake hiyo baada ya kuwa nje ya mahusiano kwa miaka zaidi ya 10 tangu kifo cha mkewe, Mama Tunda, kabla ya sasa kuanza safari hiyo akimpata wa ubavu wake ambaye ni mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited.

Tukio hilo la kumvisha pete lilikuja siku chache tangu alipopokea tuzo katika jukwaa la heshima ya Bongo Fleva na amesema ameamua kufanya hivyo baada ya kuchoka kuishi mwenyewe.



Dakika 5 Na... ilimtafuta mwasısı huyo wa makundi ya Ghetto Boyz na Watu Pori aliyetamba na nyimbo kama Darubini Kali, Mkuki moyoni na nyingine kali na kumpongeza kwa tukio hilo na maandalizi ya harusi na kufichua moja ya mambo yaliyomchosha ni kuosha vyombo licha ya kuwa anajua sana kupika.

"Najua hili hulifahamu, mimi ni mtaalamu sana wa kupika ila mvivu kuosha vyombo, hapa natamani sana kuoa nimechoka kuishi mwenyewe. Nataka kupata mwanamke mwema, msikivu na mwenye kuwapenda watoto wangu, kiufupi tupendane," anasema Afande Sele.

MAHARI YA KISHUA

Afande amefichua amelipa ng'ombe, mbuzi na Sh5 milioni kama mahari kwa ajili ya mchumba wake huyo, Imani.
"Nashukuru sana kwa pongezi zako, nashukuru pia jambo hili la kuvalisha pete kwa mke wangu mtarajiwa Imani limepita.
Kwa sasa tuko kwenye maandalizi ya ndoa na tutafunga Desemba, 2025, mjini Morogoro.

Jambo ambalo wengi hawalifahamu ni sijakurupuka kutaka kufunga ndoa na Imani. Nipo naye kwenye mahusiano miaka mitatu sasa, hivyo tumesomana tabia na kuona tunafaa kuwa mke na mume.

"Kuhusu ndoa, itafungwa serikalini, sababu mke wangu mtarajiwa ni msabato na mimi dini ninayoiamini ni upendo na ndiyo sababu ya ndoa yangu haifanyiki kidini. Hadi sasa nimeshamtolea mahari siku niliyomvisha pete nyumbani kwa kaka yake anayeitwa Gaspar Makongoro, Kibaha, Pwani na mahari ni Sh5 milioni ambazo kwa mila za Kijita ilitakiwa pia ngombe sita, mbuzi wanne, sufuri moja, majembe mawili, blanket la babu na vitenge vya bibi.



Mchumba wako unaona anaweza kuwa msaada kwenye muziki?
"Sahihi kabisa, sababu ni mwanahabari mzoefu na anafahamu sanaa na mambo mengi ya jamii. Nikuambie tu, kitu kimoja wapo kilichomvutia kwangu ni kazi yangu ya sanaa, hivyo natarajia makubwa kwake kwenye kusimamia kazi zangu, ushauri wake kuhusu sanaa na uzuri waandishi na wasanii huwa kama pacha, tunategemeana."

Ni wimbo upi unagusa maisha yako?

"Mimi nyimbo zangu nyingi huwa zinagusa maisha, sababu ninapo zitunga huwa nafikiria jamii lakini kuna baadhi ya nyimbo kama 'Mkuki Moyoni' iliyokuwa imebeba Albamu yangu ya kwanza ile kwa asilimia kubwa imegusa maisha yangu."

Umejipangaje kufanya muziki kipindi cha mitandao ya kijamii kushika kasi?

"Sisi tulianza kabla ya mitandao ya kijamii, Kwa hiyo kipindi hiki cha mitandao ya kijamii nitaendelea kujipanga kwa kile tulichokuwa tumekifanya kwa miaka yote na hata inavyoonekana maadili yameshuka kwenye muziki ni huu muziki wa kipindi hiki cha mitandao ya kijamii, unaweza kuwalazimisha watu wakusikilize hata kama umefanya kitu kibaya, Kwa hiyo nimejipanga kujihusisha na mitandao ya kijamii sababu ndiyo watu waliko.

Unaonaje vipaji vya chipukizi?

Wanafanya vizuri, ukizungumzia chipukizi wale waliokuja nyuma yetu, kama Diamond Platnumz, Harmonize, kwa upande wa Singeli kuna Dulla Makabila hawa siwezi kuwaita tena chipukizi sababu washakuwa wa wakubwa na wanafanya vizuri, lakini wale waliokuja nyuma yetu hasa upande wa kuimba hip hop, hakuna anayefanya vizuri, japo wapo, sema hawapewi nafasi, wanaopewa nafasi ni wale ambao hawafanyi vizuri ila kijumla muziki unakwenda vizuri."

Wasanii gani unakubali uandishi wao kwenye muziki?

"Wapo wanamuziki wengi kwenye R&B, Hip Hop, bongo Fleva, Singeli wanaandika vizuri, kama Dulla Makabila na wengine wengi, halafu mimi sio mshabiki wa nyimbo za matusi na wanaoandika vizuri kwenye muziki wa ndio wale ambao hawapati nafasi kwa sababu tumeilazimisha jamii wakiamini ukiimba matusi ndiyo utapata nafasi, kwa hiyo wale wanaoandika matusi kwenye bongo Fleva ndio wanapata nafasi sana ya kufanyiwa promotion."

"Sasa kwangu mimi wale sio wanaandika vizuri na kuna baadhi ya wanahabari wengi wamekuwa wakitoa kipaumbele kwa wale wanaoimba matusi, wanatukana kwenye nyimbo zao ili waweze kupata kiki, wanatumia lugha za wazi sana na mamlaka husika haikemei na ndiyo kwanza kwenye sherehe za kitaifa wanaitwa hao hao wenye kuimba matusi wanakwenda kufanya shoo."



Nani angestahili Ufalme wa Rhymes baada yako?

"Wapo wengi, kama Chidi Benz na kuna mtu anaitwa Roho Saba, anaweza sana ila hapati nafasi, hapewi kipaumbele kwa jamii, sababu jamii inapenda vitu vya kijinga hawapendi usiriasi.Wapo pia Niki Mbishi, Roma, Stamina, hawapewi nafasi kwenye media.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags