Siri Namba Zinazotajwa Na Mastaa Wa Singeli, 45, 32, 26

Siri Namba Zinazotajwa Na Mastaa Wa Singeli, 45, 32, 26


Kama ni mfuatiliaji wa muziki wa singeli ambao asili yake ni uswahili. Ni hakika umewahi kusikia wasanii wa muziki huo na mashabiki wakijinadi kuhusu namba. Wapo wanaojitambulisha kama 45,32 na wengine hujiita 26.

Watu wengi wameshindwa kutambua maana ya namba hizo na wengine wakihisi hazina maana yoyote. Lakini kwa wenyeji wa maeneo ya uswahilini na wapenzi wa muziki huo wanasema kila namba ambayo inatajwa huwa na maana yake.

Akielezea maana ya namba hizo mwanamuziki wa Singeli Jay Combat ameiambia Mwananchi namba hizo ni tambo zinazotumika mitaani.

“ Watu wanaojiita 27 ni watafutaji usiku na mchana, 31 ni wazee wa bakora . Kuna wengine 45,32, 55, kuna 47 hao wanajiita ‘Makapelo Kufunika’ mtaani kuna namba nyingi kila mtu anatetea upande wake kwenye kutafuta mashabiki wake.

“Hao wenye namba 47 ni kama magensta na mara nyingine huwa wanavaa kapelo zina namba zao kabisa ambazo wakizivaa zinafunika hadi macho,” amesema Jay

Jay Combat ni kati ya wasanii wa muziki wa singeli wanaofanya vizuri kwenye gemu kwa sasa, hasa kupitia wimbo wake ‘Wivu’.

Utakumbuka kutokana na wimbo huo kufanya vizuri uliweza kufanyiwa remix na Dj Mushizo akiwa na Jay Combat wakiwashirikisha wasanii kama Ibraah na Baddest 47 .

Hadi sasa video ya ‘Wivu’ imetazamwa zaidi ya mara milioni nne huku ikiwa na miezi minne tangu kuachiwa kwake.

Mbali na Jay mdau wa muziki wa singeli Baraka Lucas, ambaye ni mkazi wa Gongo la Mboto anasema wamekuwa wakitumia namba hizo zikiwa na maana ndani yake.

"Tukianza na namba 45 hawa wengi wanakuwa ni watu wazima wenye umri mkubwa kuanzia miaka 30-45 ambao wao hujiita masela wa zamani yaani wameshafanyaga vurugu zao miaka hiyo na sasa wameamua kupoa.

"Lakini kwa upande wa 32 hawa mara nyingi ni vijana tuu wa rika tofauti tofauti ambao sasa wao wanausela mwingi kukinukisha ni muda mchache sana," anasema Baraka.

Baraka anaongezea kuwa chimbuko la namba hizo ni kutoka uswahilini maeneo kama Vingunguti, Gongo la Mboto Temeke n.k. Lakini kutokana na kuendelea kwa namba hizo hadi wanawake nao wanazitumia kwa sasa.

Aidha ameitaja namba 26 ambayo imekuwa ikipendwa kutumiwa na msanii wa singeli Balaa Mc, ‘26 Kipaji’. Baraka anasema 26 ni watu watulivu ambao hawana makuu na mtu.

"Namba 26 inawakilisha watu fulani hivi ambao wamepoa, yaani hawana ule usela. Mara nyingi unaweza kuwakuta wamependeza tu. Umri wao wanakuwa kuanzia miaka 20 mpaka 30 na watu hao utakuta wana kazi zao mtaani au hata sehemu fulani na wanapenda kula bata”,anasema Baraka.


Baraka anaongezea kuwa sio lazima kila mtu kuwa na namba yaani 'CODE' ila kutokana na maisha mapya vijana wengi wamejikita humo na kujipachika namba hizo.
Anaongezea kwa kusema inaruhusiwa msanii au mtu kubadili namba kutokana na umri wake kusogea mbele. Mfano mtu mwenye namba 32 anaweza kusogea mpaka 45 lakini lazima awe ameacha matukio ya usela yanayofanywa na watu wa namba 32.
"Unaruhusiwa kusogea kwa sababu 45 ni umri fulani hivi wa makaka kama wasanii Fid Q yule ni 45 kabisa. Lakini kwa wasanii ambao bado ni wahuni wana matukio ya ajabu ajabu huyo anabaikia 32," anasema Baraka.
Anaendelea kusema unaweza kuwa namba 45 lakini sio mtu mzima, hiyo ni kwa sababu licha ya kuishi uswahilini lakini umejiepusha na matukio ya 32.
"Heshima ipo kwa sababu unakuta 45 wengine wamewahi kuwa na usela huko nyuma kwa hiyo lazima 45 asimame kama kiongozi wa kukemea tabia za uovu wa 32 kwenye jamii," anasema Baraka.

Utakumbuka hata katika wimbo wa Diamond ‘Nitafanyaje’ uliotoka wiki mbili zilizopita huku video yake ikiwa imetazamwa zaidi ya mara 3.3 milioni. Mwishoni mwa wimbo huo wenye mahadhi ya singeli na mchiriku msanii huyo Diamond anasikika akiziimba namba,
"Wahuni wana namba zao zinaitwa 45,
Wahuni wana namba zao zinaitwa 32,
Masela wana namba zao zinaitwa 26
Ila wengine hawana namba ila chokoza kitimtim,"ameimba Diamond kwenye wimbo wake huo.

Hivyo basi kupitia namba hizo ambazo kwa sasa zinatumiwa sana na wasanii, zimekuwa zikitumika kuwarusha au kuwachezesha mashabiki wa aina mbalimbali katika shoo zao.

Kutajwa kwa namba hizo huwafanya mashabiki wenye tabia husika ya namba kuhisi kuthaminiwa na msanii hivyo huingia kati kucheza na wengine kuonesha mbwembwe zao






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags