Olipa Assa
Mchekeshaji na msanii wa Muziki wa Singeli, Tabu Mtingita kama kuna kitu kinamfanya azungumziwe zaidi katika mitandao ya kijamii nje na kazi za sanaa anazozifanya ni mahusiano yake.
Msanii huyo amekuwa akifanya vizuri kwenye mitandao ya kijamii kutokana na aina yake ya maisha jambo ambalo limemfanya apate wafuasi wengi.
Mwananchi limefanya mahojiano Mtingita anayejivunia kuingia katika mahusiano hii ikiwa awamu ya tatu na wanaume aliyowazidi umri ili mradi akili zao ziwe zimekomaa.
MUZIKI WA SINGELI
Anasema muziki wa singeli umekuwa mkubwa duniani, lakini unatakiwa kuzingatia maadili ya kuepusha maneno ya matusi ndani ya mashairi kwa baadhi ya wasanii wanaofanya hivyo.
“Muziki huu kwa sasa unafanyiwa chalenji hadi Ulaya, hiyo ni fursa kwetu kuimba nyimbo zinazofunza na kupunguza maneno ya kihuni, tofauti na zamani ambapo ulionekana wa kihuni na masela zaidi,” anasema Tabu ambaye kabla ya kuwa mchekesha alikuwa muimbaji katika bendi ya Shirika la Bandari Mtwara.
Anasema anaujua vizuri muziki ndiyo maana anaimba na siyo kuongea kama ilivyo kwa wasanii baadhi wenye majina makubwa ambao wanabebwa na upepo wa majina yao.
Anasema wimbo ambao umemtambulisha katika muziki huo ni Mashangazi ambao ulipokelewa kwa ukubwa katika mitandao ya kijamii.
“Niliimba wimbo wa Mishangazi kutokana na wakati tuliopo, jamii inawachukulia kama watu wa hovyo kumbe sivyo ilivyo badala yake ni watu wazuri ambao wanafuata mioyo yao inataka nini bila kujali maneno ya watu ambao hata ya kwao yamewashinda,” anasema Mtingita na kuongeza;
“Wimbo wa Mishangazi ulilenga kuelimisha jamii ili kuacha dharau na kujua mapenzi hayana umri pia wimbo huo unanihusu maana mume wangu nimemzidi umri na sijawahi kulificha hilo.
“Siwezi kumuita mume wangu kibenteni badala yake namuita kiposongo lenye maana ya mume, hivyo mashangazi tuna akili timamu na tunaishi maisha halisi ambayo wengine wanayakataa hadharani ila wanayodhani wamewazidi umri wanawatesa.”
Anasema japokuwa anapata shoo sehemu mbalimbali kama Mafia, Ikwiriri, Chamanzi,Geita Mwanza, lakini bado anajitafuta kutengeneza jina lake kubwa kama ambavyo anajulikana katika komedi.
“Nina nyimbo mbalimbali zinazofanya vizuri katika mitandao ya kijamii kama Penzi Jipya Ft Classic, Ex Ft Sizo Ng’avanga, Mawifi, Kiposongo Ft Kinata Mc, Mashangazi, Inasikitisha ambayo maudhui yake ni kukemea ukatili wa kijinsia katika jamii na Watoto wa 2000 kwa kifupi zipo nyingi,” anasema.
Kutokana na kufanya sanaa tofauti anaelezea anavyougawa muda wake kutengeneza video za vichekesho na kwenda kurekodi studio:” Nina kipaji kikubwa sijakurupuka, nikienda studio narekodi nyimbo halafu nakaa nazo, nafanya vichekesho pia natulia navyo, hivyo ukifika muda wa kuziachia kazi zangu nafanya hivyo wakati naendelea na majukumu mengine ya MC.”
ANAVYOONA KOMEDI ZA SASA
Anasema baadhi ya wasanii wa komedi wa sasa wanakurupuka kufanya vitu ambavyo havielimishi jamii, akitofautisha na wa zamani ambao maudhui yao yalibeba mafunzo na kuburudisha.
“Japokuwa ni mkongwe nimeanza komedi mwaka 2018, hivyo nina miaka nane, nikiwasikiliza wa sasa ukiwa na watu wa unaowaheshima ama watoto huwezi maana ndani yake zina matusi ambayo yanapotosha na siyo kujenga,” anasema na kuongeza;
“Kitu kingine cha kushangaza wengine wameshindwa maisha ni watu wazima unakuta miaka 60 anadhani komedi ni kichaka cha kufanya vitu vya hovyo ambavyo jamii inashindwa kuelewa, vema watambue kwamba ni sanaa ya heshima.”
ANATAMANI KOLABO NA HARMONIZE
Anasema kama kuna msanii mkubwa anayetamani kufanya kolabo naye ni Harmonize hasa kwa lafudhi ya Kimakonde kama wimbo wake wa Kila Munu Ave na Kwao.
“Ikija kutokea fursa hiyo atakufa kipa ama beki studio, namkubali aina ya uimbaji wake na anafanya vizuri, ipo siku hilo litatimia,”anasema Tabu ambaye anakiri komedi iliyomtoa ni ya Muna alivyofiwa na mtoto wake Patrick alivyokuwa anajielezea kwa Kiswahili akawa anatafsiri kwa Kimakonde.
“Japokuwa kichekesho hicho kilitafsiriwa kama nakejeli msiba, kiukweli niliumia na nilitamani watu wajitokeze kwa wengi kumzika Patrick na baada ya msiba Muna alinitafuta na sasa ni marafiki na akisafiri huwa ananiletea zawadi, tunashauriana mambo ya kimaisha,” anasema.
Anasema kuna komedi nyingine anazifanya za kuwasema wasanii, hana maana ya kuwachukia isipokuwa anawapa chalenji ya kufanya vitu vyao kwa usahihi ama wakati mwingine anawapongeza.
“Wazazi wangu walikuwa wasomi na uwezo kifedha, hivyo walikuwa hawapendi kuniona nafanya komedi nikiwa mdogo walitamani nisome zaidi, ila nilikomaa niliamini katika kipaji changu nitafanikiwa na hilo limetimia natamani wazazi wangu wangekuwa hai wangefaidi kidogo ninachokipata,”anasema.
MAHUSIANO
Anasema kuishi na mwanaume aliyemzidi umri hajawahi kuogopa kwa sababu havunji sheria na ndiyo maana hajawahi kukamatwa na polisi:”Tangu nije Dar es Salaam nina mahusiano matatu, ila sijawahi kuishi na waliyo na umri kuanzia 30 kushuka chini, wanaanzia miaka 32 kwenda juu ambao wamekomaa kiakili na wanajua wanachokifanya.
Anaongeza:”Mume wangu wa sasa ana umri wa miaka 35, kwa hiyo siyo mtoto mdogo vinginevyo ningekaa katika magereza mbalimbali, wanachotakiwa kunielewa watu nazingatia amani yangu ya moyo.
“Huko nyuma nilipotoka nimewahi kuwa na mahusiano na watu wazima kama wa miaka 60 lakini wana mambo yale yale, visirani, magomvi, nilichojifunza ni kuvumiliana ili kuishi kwa muda mrefu, mkishindwana mnaachana unatulia kisha unapata mtu mwingine maisha yanaendelea.”
Mtingita anasema anapokutana na vijana hao wanakuwa wembamba akiwalisha miili inaanza kunawiri, hivyo waliyokuwa wanamsema wanagundua kwamba walikuwa wanasumbuliwa na lishe na wanapunguza maneno na kumuacha na maisha yake.
“Ninayeishi naye ana kazi zake Mafia huwa anakwenda kuzisimamia, anakuja nakwenda hivyo maisha yetu yana furaha na amani,”anasema Mtingita ambaye anasema hapendi mpira isipokuwa mume wake ambaye ni Yanga ikicheza rimoti anashika yeye mwanzo mwisho.
UBONGE UNAZEESHA
“Unene unazeesha nilipotoka Mtwara kuja Dar es Salaam mwili ulijaa, nilikuwa napumua hovyo, nakoroma, nyonga zilikuwa zinanishika nikienda hospitali kupima UTI sina, pingili za mgongo zilikuwa zinagoma, ukilala ni staili moja hiyo hiyo, nimepungua kwa sababu nafanya dayati nimeacha vitu vitamu na kuna dawa natumia kwa sasa ni mwepesi,” anasema Mtingita na kuongeza;
“Kabla ya kupungua nikakaa mkoa wa kula chipsi ilikuwa sahani tatu na mayai sita ila kwa sasa sili kabisa hivyo vitu, nimepungua nikivaa nguo napendeza, nimekuwa binti na najiamini mbele za watu na siumwi tena ingawa changamoto inayosumbua ni pumu ambayo inanibana mara chache.
“Nilikuwa na kilo 127 kwa sasa nacheza na 80 wakati mwingine 70 na bado naendelea kupungua nifike hadi 60.
MAFANIKIO YA USANII
Anasema anamiliki gari, kajenga nyumba ya kuishi, ana viwanja, anawasaidia ndugu zake wanapohitaji msaada wake.

Leave a Reply