Baada ya kushika kasi kwa njia za kusambaza na kuuza muziki kidijitali, wasanii wengi nchini hasa wale wa Bongo Fleva wamerudisha utamaduni wa kutoa albamu ila sasa wameongeza na kitu kingine kinachoshabihiana na albamu, nacho ni EP.
Inaelezwa albamu hujumuisha nyimbo kuanzia nane na kuendelea ambazo kwa ujumla zinakuwa na dakika kati ya 30 hadi 80, huku EP ikiwa na nyimbo kuanzia nne hadi nane ambazo kwa ujumla huwa dakika kati ya 10 hadi 30.
Katika Bongo Fleva sasa, Extended Play (EP) ndizo zinatoka kwa wingi kuliko albamu, mathalani Rayvanny ndani ya miaka miwili pekee aliweza kutoa EP nne, Flowers (2020), New Chui (2021), Flowers II (2022) na Unplugged Session (2022).
Utakumbuka kwa miaka mingi nyuma wasanii wengi waliachana na utamaduni wa kutoa albamu kutokana na mabadiliko ya kidijitali na kushamiri kwa uharamia kwenye soko ambapo wajanja wachache ndiyo waliokuwa wananufaika zaidi.
“Teknolojia imebadilika na wasanii wanaenda na teknolojia, huwezi ukauza kanda wakati sasa hivi redio za kanda siyo biashara tena, dunia ya sasa inawalazimu kwenda kwenye dijitali na kote ndivyo wanavyofanya.” alisema Soggy Doggy mwenye albamu tano.
Kwa mujibu wa data za gazeti la Mwananchi, tangu 2020, kila mwaka nchini wasanii hutoa albamu na EP zaidi ya 10, huku Harmonize akiwa ndiye msanii aliyetoa albamu nyingi kwa kipindi hicho ambapo ni tano.
Ndani ya muda huo, Diamond Platnumz na H. Baba, EP zao zilikuwa na idadi kubwa ya nyimbo, First of All (2022) yake Diamond ilitoka na nyimbo 10, na Duku Duku (2022) ya H. Baba ilitoka na nyimbo 12 kitu kinachotajwa kuwa siyo sahihi.
Hivyo kumekuwepo na mjadala unaodai kuwa baadhi ya EP zinazotoka nchini hazina sifa hiyo bali zinapaswa kuwa Long-Playing Record (LP), pia baadhi ya albamu hazina sifa hiyo bali zinapaswa kuwa Mixtape.
Kabla ya Diamond na H. Baba hakuna msanii aliyewahi kutoa EP yenye nyimbo 10 au zaidi, EP ya Ravanny ‘Flowers’ ndiyo ilikuwa inashikilia rekodi ya kuwa na nyimbo nyingi ambazo ni nane, huku EP ya K2ga, Safari (2021) ikiwa na nyimbo chache ambazo ni tatu.
Wakizungumza na gazeti la Mwananchi, mwanamuziki G Nako na Mkurugenzi Mtendaji wa Fahamu Muziki, Frank Daxx wamekuwa na maoni yanayoshabihiana kuhusu utofauti wa albamu, EP, LP na mixtape.
Frank Daxx ambaye amekuwa akitumia mitandao kueneza uelewa wa muziki, amesema kwa kawaida albamu, EP na mixtape zinatofautishwa kwa idadi ya nyimbo, dakika za nyimbo zote kwa ujumla na lengo kuu la kimaudhui.
Albamu inatakiwa iwe na nyimbo kuanzia nane na kuendelea, muhimu zaidi inapaswa kuwa na mtiririko wa kimaudhui unaoshabihiana toka wimbo wa kwanza hadi mwisho. Msikilizaji anakuwa kama anasoma kitabu kinachoelezea jambo fulani kuanzia ukurasa wa mwanzo hadi wa mwisho.
“Sasa wasanii wetu wanakusanya nyimbo zao kadhaa kali wanatoa anasema ni albamu, ukisikiliza hakuna muunganiko kati ya wimbo na wimbo, pia unakuta hakuna intro wala untro, maana intro anakuelezea hii albamu inazungumzia kipi hasa.” anasema Frank.
Kutokana na albamu kuwa na vigezo hivyo kinachowabana wasanii, ndipo wengi wamekimbilia kutoa EP na mixtape ambazo haziwabani kivyovyote vile.
“EP inatakiwa iwe nyimbo kuanzia tatu hadi nne, ukizidisha sana ni tano au hata sita, LP inakuwa ndefu kuliko EP ya kawaida. Hiyo ya Diamond nasema ni LP kwa sababu ina nyimbo nyingi halafu ina dakika zaidi ya 30, zipo kama 33 hivi,” anaeleza.
Anasema mixtape inakuwa na mchanganyiko wa nyimbo zisizo na idadi maalumu na haina lengo kuu la kimaudhui, bali ni sehemu ya msanii kuonesha ubora wake, pia haimbani hivyo anaweza kusampo nyimbo za wasanii wengine na ni gharama nafuu kuiandaa.
“Ndiyo maana huwa nasema kila mara kuwa ile ‘Afro East’ ya Harmonize siyo albamu bali ni mixtape kwa sababu amesampo nyimbo nyingi na haina mtiririko maalumu, kila wimbo upo kivyake tu,” anasema Frank.
Utakumbuka albamu hiyo ya Harmonize, Afro East (2020) imechukua vionjo kutoka kwenye nyimbo kama ‘Bachelor’ wake Squeezer, ‘Malaika’ wake Miriam Makeba, ‘Show Me the Way’ wake Papa Wemba n.k.
Alisema mara nyingi EP na mixtape huwa zinatoka kwa muktadha wa utambulisho wa albamu na siyo kibiashara, kwa nchi ambazo muziki wao umepiga hatua, EP na mixtape huwa wanatolewa bure kwa mashabiki, ni wachache sana huwa wanauza.
“Ukisoma historia za wasanii kama kina Lil Wayne utakuta wana mixtape nyingi lakini wewe huzijui kwa sababu wanatoa kwa ajili ya watu wa mitaani na wanafanya hivi kwa zile nyimbo ambazo wanaona siyo nzuri kibiashara ila zinasikilizika,” anasema.
Kwa upande wake G Nako kutoka kundi la Weusi amesema albamu ni jambo kubwa mno ambalo msanii anatakiwa kuwa amejipanga zaidi kimaudhui tofauti na ilivyo upande wa EP.
“Albamu kwangu mimi inasimama kama kitabu, hivyo inatakiwa ibebe maudhui yaliyojikita sehemu moja, labda unataka kuzungumzia siasa, itabidi utulie katika eneo hilo pekee.” anasema G Nako na kuongeza.
“Kwa hiyo ni kitu ambacho unatakiwa ukitengeneze kwa ustadi na kutulia zaidi, tofauti na EP ambayo inakuwa ni mchanganyiko wa nyimbo zenye maudhui tofauti tofauti. Halafu kuna mashabiki wanataka kukusikia kwenye wimbo zaidi ya mmoja halafu huwezi kutoa albamu, ndiyo unaachia EP.”
Baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva ambao tayari wametoa albamu kwa mwaka huu wa 2024 ni pamoja na Roma ‘Nipeni Maua Yangu’, Jay Melody ‘Therapy’, Harmonize ‘Muziki wa Samia’, Young Lunya ‘Mbuzi’ n.k.
Ikumbukwe wasanii wa muziki waliotoa albamu nyingi ni Mr. II Sugu (10), Lady Jaydee (8), Nikki Mbishi (7), Soggy Doggy (5), Juma Nature (5) Harmonize (5), Professor Jay (4), Mh. Temba (3), Fid Q (3), Diamond Platnumz (3), Alikiba (3), Barnaba (3), Navy Kenzo (3) n.k.
Tangu 2020 wasanii wengine waliotoa EP ni Nandy (Wanibariki, Taste & Maturity), Ibraah (Steps & Karata), Zuchu (I Am Zuchu), Lulu Diva (The 4 Some), Lava Lava (Promise), Belle 9 (Baba Boss TV), Ibra Nation (Addicted), Dayna Nyange (ELO), Izzo Bizness (The Capricorn), Mac Voice (My Voice).
Wengine ni Damian Soul (Mapopo), Quick Rocka (Love Life), Mwasiti (The Black Butterfly), Maua Sama (Cinema), Hamisa Mobetto (Yours Truly EP), Mbosso (Khan), P Mawenge (Simu na Matukio), Stamina (Love Bite), Killy (The Green Light), Mansu-Li (Love Life), Yammi (Three Hearts), Kusah (Kusah), Abigail Chams (5), Professor Jay (Nusu Kuzimu Nusu Peponi)
Leave a Reply