Baadhi ya waimbaji wa Bongofleva wanasifika kwa utunzi wa nyimbo nzuri za mapenzi ila Mbosso amefanikisha katika tungo zake za namna hiyo kutokana na kuimba vitu tunavyoviishi kila siku.
Mathalani nyimbo zake nyingi za mapenzi anapenda kuzihusisha na vyakula (misosi) hasa vya Kitanzania ambavyo kila siku lazima tuvitafute na kuvila. Baadhi ya nyimbo alizofanya hivyo, ni hizi zifuatazo:
1. Nadekezwa - Biriani ya ngamia

Kufuatia kutoswa na mpenzi wake kisa hali ngumu kiuchumi, Mbosso alimpata ‘Baby’ mwingine ambaye anamlisha vinono kama biriani ya ngamia hadi kumtungia wimbo ‘Nadekezwa’ (2018).
“Nalishwa vitamu vinono najilia, biriani ya ngamia, penzi twadalikana poo kidali.” Mbosso katika wimbo huo uliotoka mwaka wake wa kwanza ndani ya WCB Wasafi iliyomtambulisha hapo Januari 2018. Video yake ni kali ikiongozwa na Director Kenny akifanya katika vituo vya kitalii huko Kaskazini mwa Tanzania maeneo kama Ngorongoro Crater, Meru Waterfalls, Mlima Meru, Ziwa Manyara na jijini Arusha.
2. Alele - Supu ya mapupu
Huku katika wimbo, Alele (2018) Mbosso ndipo kaimba misosi kibao, kuanzia mihogo ya fukwe za koko, Dar es Salaam hadi supu ya mapupu ambayo pele Vingunguti maeneo ya machinjio hata kwa bei ya Sh500 tu unaipata.
“Leo tule nini mihogo ya koko... Chumvi kwa kikopa, wali maini ndizi nyama... Naomba nipate supu ya nyama laini kama mapupu.” anaimba Mbosso katika wimbo huo ambao ni watano kutoa chini ya Wasafi.
Na katika wimbo huu Mbosso anajitambulisha kama Mhindi wa Kusini na kumueleza mpenzi wake ingawa kwao Kibiti hakuna madini, basi sio vibaya wakiwinde telele.
3. Maajab - Chapati za alizeti

Katika wimbo wake, Maajab (2019), Mbosso anamtaka mpenzi wake kumlisha chapati za alizeti ili anone, kwa kifupi kuna chapati, halafu kuna chapati za alizeti, yaani kuna picha fulani anakutengenezea kichwani kwako. “Nikila nilishe chapati za alizeti ninone, tuwafungishe midomo uzi cement tuwashone.” anaimba Mbosso katika wimbo huo ambao video yake imefanyika nchini Morocco katika jangwa la Sahara ambalo ndilo kubwa zaidi duniani. Katika wimbo huu ndipo pia anasema anaoshwa mwili kwa maji ya madafu.
Ndiyo madafu, yale ambayo nyie mnakunywa, mwenzenu Mbosso ndio anaogeshewa na mpenzi wake. Sasa jiulize ni madafu mangapi yanatumika hadi tupate walau maji ndoo moja ya kuogea!.
4. Fally - Chuzi kwa matandu
Kwa ajili ya kumpa pole ‘dear ex’ akimueleza kuwa ameshasahau zama za kuumizwa, Mbosso akatoa wimbo, Fall (2020) ambapo anaeleza alipo sasa anakula vizuri, chuzi kwa matandu ndio mpango mzima. “Nakula kwa raha zangu nyama mpaka mfupa.... Huba tulisosomole chuzi kwa matandu.” Mbosso katika wimbo ‘Fall’ uliotengenezwa na Watayarishaji wawili, S2Kizzy na Lizer Classic.
Mbosso anaongeza kuwa penzi lake hii sio la kudokoa, bali anakula kwa kunyofoa, kama embe analipopoa, huku wakijifotoa!.
5. Tamba - Mchuzi wa nguru
Kabla ya kufanya vizuri na albamu yake, Definition of Love (2021), Mbosso alitamba na wimbo, Tamba (2020), huku napo kazungumzia misosi ila awamu hii anataka tu mchuzi wa nguru. “Nguru usimtoe chumvi ndio ladha yake, muunge tu nipe na chuzi na nyama yake.” Mbosso katika wimbo huo uliotengenezwa na Nusder Venom, huku Lizer Classic akihusika katika mixing.
Wimbo huu uliosadifu maisha halisi ya uswahilini, hadi sasa ni moja ya nyimbo za Mbosso ambazo zilipata mapokezi makubwa ukiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 27.8, ni video ya sita kwake kutazamwa zaidi YouTube kwa muda wote.
6. Yalah - Togwa na biriani
Licha ya kupewa upofu na penzi hili, bado Mbosso anakiri kuwa wanaanzia jikoni hadi varandani wakinywa togwa, pia wakila maboga, uyoga, biriani na mboga kama anavyoeleza katika wimbo wake, Yalah (2021).
“Tungezaliwa zamani ningesema penzi togwa, tulinywe kibarazani tukitafuna maboga. Nimekipanda uani kibustani cha uyoga, tukishiba biriani baby tule mboga mboga,” anaimba Mbosso.
Huu ni wimbo namba tano ndani ya albamu, Definition Of Love (2021) yenye nyimbo 12 akishirikiana na wasanii kutoka nchi za Tanzania (Diamond Platnumz, Njenje, Baba Levo, Darassa na Rayvanny), Nigeria (Mr. Flavour na Liya) na Uganda (Spice Diana).
7. Mtaalam - Kachumbari kwa ugali
Akijitambulisha kama Mtanzania halali ila mwenye chembechembe za India, Mbosso kupitia wimbo wake, Mtaalam (2021) anasema ingawa hana kitu ila uhusiano na mpenzi wake unanoga kama kachumbari kwa ugali.
“Sitakuhonga magari ila mahaba utasanzia, penzi kachumbari kwa ugali na pilipili ya kushagia.” anaimba Mbosso katika wimbo huo ambao video yake ina ‘views’ zaidi milioni 20 YouTube.
8. Umechelewa - Hataki vya mafuta, bali nazi
Baada ya kumpata mpenzi mpya, Mbosso kupitia wimbo, Umechelewa (2024) anamueleza mateso aliyopitia zamani ikiwa ni pamoja na kulishwa misosi ya mafuta wakati yeye anataka ya nazi.Ukiachana na hizo, nyimbo nyingine za mapenzi ambazo Mbosso amesifia au kutaja misosi ni pamoja na Hodari (2018), Tamu (2018), Nipepee (2018), Huyu Hapa (2023), Amepotea (2023) na kadhalika.
Leave a Reply