Universal Music Group imewasilisha ombi la kufutwa kwa kesi ya Drake dhidi yao ikihusisha wimbo wa 'Not Like Us' wakidai rapa huyo alishiriki majibizano ya nyimbo kwa hiari yake mwenyewe.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama zilizopatikana Jumatatu Machi 17, 2025 kampuni ya UMG inamtaka jaji kuitupilia mbali kesi ya Drake, ambayo inaishutumu kampuni hiyo kwa kuanzisha mpango usio halali wa kuongeza namba ya wasikilizaji ili kuupa umaarufu wimbo wa "Not Like Us" wa Kendrick Lamar.
“ Drake msanii aliyefanikiwa muda wote alipoteza pambano la rap ambalo alichochea na kushiriki kwa hiari yake mwenyewe. Badala ya kukubali kushindwa kama msanii, ameamua kuishitaki lebo yake mwenyewe kwa lengo la kufuta machungu yake, inapaswa kutupiliwa mbali,” imesema UMG
Utakumbuka, Januari 14, 2025, Drake alifuta kesi aliyoifungua dhidi ya Spotify na Universal Music Group UMG aliyoifungua Novemba 2024. Lakini baada ya Onesho La Super Bowl 2025, mawakili wake waliifungua tena wakidai UMG ilimruhusu Lamar kutumbuiza Not Like Us, jambo waliloliona kama mwendelezo wa kashfa dhidi ya Drake.
Hata hivyo, Universal Music Group walitoka hadharani na kupinga madai hayo ambapo walisema hakuna kitu kama hicho kwani kila msanii anapata anachostahili kimkataba na hakuna njia za udanganyifu na madai yake aliyoyafungua kwa mara ya pili bado wanayapinga na kutaka mahakama kutupilia mbali.

Leave a Reply