Upo umuhimu wa kutengeneza Documentaries kwa wasanii

Upo umuhimu wa kutengeneza Documentaries kwa wasanii

Sekta ya muziki nchini Tanzania imekuwa kwa asilimia kubwa katika miaka ya hivi karibuni, huku baadhi ya wasanii kama Diamond, Harmonize, Zuchu, Jaiva, Nandy, Jay melody na wengine wakitambulika kimataifa, lakini sekta hiyo bado iko nyuma katika kipengele kimoja muhimu cha kufanya Documentaries (filamu fupi ya historia ya msanii).

Documentaries ni mpangilio wa matukio au rekodi za kihistoria ya maisha ya kazi za msanii ambayo yanaonesha moja kwa moja mapambano, mafanikio na uzoefu wa msanii katika muziki. Kwa mfano kundi la The Beatles wao mwaka 2016 walifanikiwa kutoa ‘Siku nane za wiki’ iiyoongozwa na Ron Howard ambayo ilieleza historia ya kundi la Beatles kutoka mwanzo mpaka kupata umaarufu.

Ukiachilia mbali kundi hilo wapo wasanii mbalimbali nchini Marekani ambao wamefanikiwa kutoa Documentaries kama Justin Bieber, Taylor Swift, Beyoncé huku msanii Usher naye akitarajia kuachia documentary yake nyingine itakayoonesha nyuma ya pazia wakati wa show yake aliyoifanya kwenye fainali ya ‘Super Bowl’.

Jambo hili kwa Usher na wasanii ambao wamewahi kutoa documentaries linawafanya kuendelea kuishi maishani mwa watu kwani matukio na historia zao zitakuwa zinatambulika miaka na miaka.

Ukiangalia kwa Tanzania wapo wasanii ambao walifanya vizuri lakini watu na wadau mbalimbali wa muziki hawatambua mchango wao katika sekta ya muziki mfano 20 Percent, Mr Nice, Kitime, Bendi ya Msondo Ngoma na wengineo, ukitazama kwa undani utagundua kuwa majina ya wasanii hao ni kama yamekufa kutokana na hakuna shabiki wala mdau anayetambua harakati zao katika sekta ya muziki.

Baada ya kuona umuhimu kutengeneza documentaries kwa wasanii Mwananchi Scoop ikaamua kufanya mahojiano na wadau mbalimbali kuhusiana na mtazamo wao katika hili.

Meneja wa msanii Mussa Mabumo Bando ‘Bando Mc’, Godfrey Abel ameweka wazi kuwa kuna umuhimu mkubwa kwani kwa upande wake yeye na msanii wake wamejipanga kutoa documentarie kwa siku zijazo.

“Kuna umuhimu mkubwa kutoa Documentaries ya msanii kwani kutamfanya aishi kwenye fikra na midomoni mwa watu maisha yote, hapo awali sikuwaza kabisa kufanya hivyo lakinbi baada ya Kanye kutoa documentarie yake nikaona kuna haja ya kufanya hivyo kwa msanii wangu kwani nina baadhi ya video za matukio ya msanii wangu zinazonesha harakati zake toka anatoka kwao Shinyanga,”amesema Abel.

Naye mwanamuziki mkongwe nchini John Kitime ameeleza maoni yake katika hili kwa kuweka wazi kuwa sio lazima kufanya Documentaries ili kuweza kutambulika vizazi na vizazi bali wanatakiwa kutoa nyimbo ambazo zitaishi milele.

“Wapo wasanii ambao wamewahi kufanya Documentaries (filamu fupi) mfano Remi Ongala aliwahi kufanyiwa filamu fupi yenye gharama zaidi kuliko msanii mwingine yoyote hapa nchini, lakini kitu ambacho kimeendelea kumtambulisha mjini ni nyimbo zake kwa hiyo Documentaries sio ishu wapo baadhi ya wasanii wa Marekani wanatambulika kupitia kazi zao na sio filamu fupi,” amesema John Kitime

Aidha aliongezea kuwa kwa upande wake yeye atakachoweza kukifanya ni kukusanya kazi za wasanii mbalimbali ambazo zitakuwa zinapatikana katika ofisi yake.

“Kwanza mimi ninachokifanya ni kukusanya historia ya muziki wa Tanzania kwa hiyo kuanzia sasa ukija ofisini kwangu utakuta miziki kuanzia ya mwaka 1992, kwa hiyo njia ya kuyabakiza majina ya wanamuziki wa zamani na hata wasasa ni kuwa na makumbusho ya muziki ambacho mimi ndio ninachokifanya,” amemalizia Mzee Kitime

Hatukuishia hapo pia tulifanikiwa kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwanamuziki mkongwe nchini Stara Thomas ambaye aliwahi kutamba na vibao kama ‘Mimi Na Wewe’, ‘Nipigie’ na nyinginezo ambapo aliweka wazi kuwa kuna umuhimu wa kufanya filamu fupi kwani ndio zinazoendelea kuwatambulisha.

“Upo umuhimu wa kufanya Documentaries kwa sababu filamu fupi ni ni fasihi iliyopo kwenye andishi na simulizi kwa hiyo inadumu kwa sababu wengi waliyowahi kufanya hivyo ambao wapo na walitangulia bado zinaendelea kuwatambulisha, lakini pia inatengemea na msanii sio msanii yoyote tuu anaweza kufanya hivyo ni msanii ambaye amefanya makubwa kwenye sekta ya muziki,” amesema Stara Thomas.

Aidha alimalizia kwa kuweka wazi kuwa kwa upande wake ana mpango wa kutengenza Documentaries ambayo itamuelezea Stara Thomas kwa undani pamoja na harakati zake za kimuziki mpaka kufikia sasa huku akiwataka mashabiki zake kukaa mkao wa kula kwani anakuja na kitu kizuri kwa ajili yao.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post