Usiyoyajua kuhusu Izzo Bizness

Usiyoyajua kuhusu Izzo Bizness

Rapa Izzo Bizness kutokea Mbeya ana miaka zaidi ya 15 ndani ya Bongo Fleva, ametoa EP moja, The Capricorn (2021), huku akifanya shoo kubwa na miradi mikubwa kwenye tasnia kama kushiriki Coke Studio Africa.

Huyu ni msanii wa Hip Hop Bongo ambaye alitoka kwa kishindo kwa ngoma kali kutokea MJ Records na alikuwa amesaini lebo ingawa kabla ya hapo tayari alikuwa ameachia nyimbo kadhaa. Fahamu zaidi.

1. Kipindi anaingia katika tasnia ya muziki alianza kwa kujiita Izzo B, hiyo ‘B’ ilisimama kama herufi ya mwanzo kutokea kwenye jina la Baba yake mzazi, baadaye ikaja kusimama kama ‘Bizness’ ambayo inatumika hadi sasa.

2. Wimbo wake, Bizness (2010) ambao ndio ulimtoa kimuziki, ulirekodiwa saa saba usiku akiwa ametokea kwenye shoo Mwanza, kufika saa nane ndipo Suma Lee akaingia MJ Records na kuimba chorus ya ngoma hiyo iliyorekodiwa na Marco Chali.

Huyu alikuwa amesainiwa MJ Records kama ilivyokuwa kwa Quick Rocka ambaye alitoka kupitia ngoma yake, Bullet (2010) ambayo ilitayarishwa na Marco Chali na Master J.

3. Izzo Bizness huwa anaachia wimbo kila ifikapo Desemba 25 ya kila mwaka kwani ndio tarehe yake ya kuzaliwa, nyimbo hizo mara nyingi huwa zinabeba maudhui ya sikukuu ya Christmas kama lilivyo jina lake la Emmanuel.

4. Mbali na muziki, fedha nyingi za Izzo Bizness anazielekeza kwenye familia yake na hata kwenye mkono wake amechora tattoo na kundiaka; “Family Over Everything” kuonyesha mkazo wa hilo. 

Sasa rapa huyo anaishi Marekani na familia yake, akiungana na mastaa wengine Bongo kama Vanessa Mdee, Roma n.k ambao nao wanaishi huko.

5. Izzo alikutana na Abela Music mtandaoni, mrembo huyo alipokuja Tanzania akitokea Marekani ndipo wakaunda kundi lao la The Amaizing. Abela amefanya sound track katika filamu ya Bongo Land ambayo Baba yake ndiye Director.

Sasa Izzo na Abela mwenye asili ya Bukoba, walishirikiana karika nyimbo kama Balaa (2016), Umeniweza (2016), Tumeoana (2017) na Rafiki (2017), kazi hizi zilifanya vizuri na kutabiriwa kufika mbali.

6. Kitu ambacho anakipenda zaidi Izzo Bizness akiwa nyumbani kwake ni kusikiliza redio na anapokuwa na mpenzi wake wanapenda kutazama filamu ingawa ni vigumu kuitazama hadi mwisho bila kushika simu.

7. Mdukuzi ambaye alidukua ukurasa wa Instagram wa Izzo Bizzness ulikokuwa na wafuasi (followers) zaidi ya milioni 1.5 na kutokomea nao moja kwa moja, ilihitaji Sh16 milioni ili aweze kumrudishia kitu ambacho Izzo kagoma na kufungua ukurasa mwingine.

Hata hivyo, Izzo Bizzness sio staa wa kwanza Bongo kwa ukurasa wake wa Instagram kudukuliwa, kuna Linah, Beka Flavour, Gigy Money, Mkude Simba n.k.

Vitu ambavyo hapendi Izzo Bizzness kwenye mitindao ya kijamii ni umbea, huku watu wanaofanya mambo makubwa kama kuisadia jamii kutozingatiwa kama wanaoendekeza umbea na mambo mengine ya hovyo. 

8. Video ambayo ilimpa wakati mgumu zaidi Izzo Bizzness wakati wa kushuti ni ya wimbo wake, Rafiki (2017) aliomshirikisha Abela Music, kilichompa ugumu ni kumshika nyoka mkubwa na kumweka shingoni.

9. Mdundo wa wimbo wa Izzo Bizness, Utarudishwa (2012) akimshirikisha Belle 9, umetengenezwa na rapa One The Incredible ambaye alivuma kimuziki chini ya M Lab (Music Laboratory) kupitia albamu yake ya kwanza, Soga za Mzawa (2012). 

10. Kipande alichoimba Shaa kwenye wimbo wa Izzo Bizzness, Kidawa (2015) kimeandikwa na Barnaba ambaye amewaandikia nyimbo wasanii kama Vanessa Mdee, Lulu Diva, Ruby na Mimi Mars.

Utakumbuka Shaa ambaye ni mshindi wa Coca-Cola Popstar 2004 akiunda kundi la Wakilisha, ndiye msanii wa kwanza wa kike kusainiwa MJ Records na baadaye alifanya kazi na menejimenti ya Mkubwa na Wanae, kisha kuanzisha lebo yake, SK Music.

Imeandikwa na Peter Akaro






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags