Mwanamuziki wa Bongo Fleva nchini ambaye anatamba na Ep yake ‘Room Number 3’ Mbosso ameweka wazi kuwa baada ya miaka nane kupita hatimaye amekutana tena na msanii mwenzake Aslay.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Mbosso ameeleza kuwa yeye na Aslay walikuwa tuu wakiwasiliana kwenye simu bila kuonana kwa takribani miaka nane.
“Imagine mara ya mwisho tumekutana ni mwaka 2017 na tumekuwa tukiwasiliana bila kuonana. baada ya miaka takribani 8 jana ndo tumekutana tena na kwa bahati mbaya tu kila mtu akiwa kwenye mihangaiko yake yakwenda kutafuta rizki, was nice to see you my legendary brother,”ameandika Mbosso.
Ikumbukwe wawili waliwahi kufanya kazi katika Kundi moja la muziki ‘Yamoto Band’ lililoongozwa na Mkubwa Fella ambapo kundi hilo lilisambaratika mwaka 2017 huku wakitamba na ngoma mbalimbali ikiwemo Cheza kwa Madoido, Ya Moto, Nisambazie Raha, Mama, Niseme na nyinginezo.
Kundi la Yamoto liliunganisha mastaa kama na Aslay, Mbosso, Beka Flavour na Enock Bella ambao kwa sasa kila mmoja anafanya kazi peke yake.

Leave a Reply